UCHAGUZI MKUU TANZANIA KUFANYIKA JUMATANO...RAIS MAGUFULI KUITANGAZA TAREHE OKTOBA 28,2020 KUWA SIKU YA MAPUMZIKO!!

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Magufuli

Leo Julai 22, 2020 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Magufuli amezindua Jengo la ghorofa nane la Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) 'UCHAGUZI HOUSE' lililopo eneo la Njedengwa jijini Dodoma, huku akiweka wazi kuwa siku ya Jumatano Oktoba 28, 2020 itatangazwa kuwa siku ya mapumziko kwa ajili ya zoezi la uchaguzi mkuu wa Rais, wabunge na madiwani.

Rais Magufuli ameiomba Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kuhakikisha inausimamia uchaguzi huo kwa haki, sheria na kufuata katiba ya nchi, huku akivihasa vyama vya siasa kushiriki kwa amani na kuepusha vurugu kwani vurugu hazijengi bali zinabomoa.

"Nina imani mambo yatakwenda vizuri, wananchi wajitokeze kwenye kampeni za siasa kusikiliza sera, na washiriki pia kwa wingi kwenye zoezi la upigaji kura.

"Siku ya uchaguzi (Jumatano Oktoba 28, 2020) itakuwa siku ya mapumziko, tutaitangaza rasmi," amesema.

Katika hatua nyingine, Rais Magufuli ameitaka NEC kuhamishia vifaa vilivyopo Dar es Salaam kwenda Dodoma zikiwemo Kompyuta, mafaili na vitu vingine vinavyohitajika.

"Pangeni vizuri kwenye hili jengo viongozi wa vyama vya siasa nao wapate vyumba kwasababu ni jengo la watanzania, bila kubagua wawe na ofisi ambapo wanaweza kufanya mambo yao kwa uhuru," amesema.

Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jaji Rufaa (Mst) Semistocles Kaijage, jengo hilo la ghorofa nane lilianza kujengwa Januari mwaka huu na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) na limegharimu Sh Bilioni 13.4.

"Ujenzi huu wa jengo la NEC ulipangwa kutekelezwa kwa awamu mbili ambapo jumla kuu mradi umegharimu takribani Sh Bil. 13.4, Tume hii tangu kuanzishwa kwake haijawahi kuwa na jengo lake, mradi unatarajiwa kukamilika August 30, 2020.

“Uzinduzi wa jengo hili linalojengwa na JKT unaashiria kuanza rasmi kwa shughuli za Tume hapa Dodoma, kila kitu kikienda kwa muda uliopangwa shughuli za Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani zinatarajiwa kufanyika hapa,” amesema Jaji Kaijage.

Via Shinyanga Press Club Blog

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post