Maazimio Ya Mkutano Wa SADC Wa Baraza La Mawaziri Wa Fedha Na Uwekezaji


1.        Jopo la mapitio ya viashiria vya uchumi mpana linalohusisha Mawaziri wa SADC wenye dhamana ya Fedha na Uwekezaji na Magavana wa Benki Kuu, walikutana kwa njia ya mtandao tarehe 15 Julai 2020.

2.        Dhumuni la mkutano huo ambao umefanyika kwa njia ya mtandao lilikuwa ni kupitia hatua iliyofikiwa na nchi wanachama kuhusu mafanikio yaliyofikiwa kuelekea malengo ya uchumi mpana yaliyokubaliwa pamoja na kubainisha changamoto za mwelekeo wa kiuchumi katika kanda na kushauri hatua za kisera za kukabiliana na changamoto hizo. Wakati huo huo, jopo limepokea taarifa kuhusu athari za janga la COVID-19 kwa nchi wanachama wa SADC pamoja na taarifa ya utekelezaji wa hatua za kufikia malengo ya uchumi mpana.

3.        Jopo pia lilipitia na kujadili taarifa ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambapo hii ni mara ya pili kwa nchi hizi mbili kufanyiwa mapitio tangu mfumo wa SADC wa nchi moja kuifanyia tathimini nchi nyingine kuzinduliwa mwezi Mei 2013, Maputo, Jamhuri ya Msumbiji.

4.         Jopo lilibaini yafuatayo:-

Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo
4.1         Katika miaka michache iliyopita, uchumi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo umekuwa ukiimarika, na hivyo kuiwezesha nchi kufikia malengo ya msingi na upili (primary and secondary targets) yaliyokubaliwa na nchi wanachama. 
4.2         Ukuaji wa Pato la Taifa uliimarika kutoka asilimia 2.4 mwaka 2016 hadi asilimia 3.7 mwaka 2017 na asilimia 5.8 mwaka 2018, lakini ulipungua na kufikia asilimia 4.6 mwaka 2019 hususan kutokana na kushuka kwa uzalishaji wa madini uliopelekea kuzorota kwa bei ya bidhaa.
4.3         Mfumuko wa bei ulishuka kwa kasi na kufikia asilimia 7.2 mwaka 2018 na asilimia 4.6 mwaka 2019 na inategemewa kufikia asilimia 5.0 mwaka 2020.
4.4         Wakati huo huo, mfumo wa usimamizi wa malipo taslim umewezesha Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kuwa na ziada kwenye bajeti ya asilimia 0.2 ya pato la taifa katika kipindi cha mwaka 2016 na 2018, na kupungua kufikia nakisi ya asilimia 0.2 ya pato la taifa kwa mwaka 2019.
4.5         Mwaka 2019, deni la taifa la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo lilifikia asilimia 13.3 ya pato la taifa, uwiano ambao upo ndani ya lengo lililowekwa na nchi wanachama wa SADC usiozidi asilimia 60 ya pato la taifa.

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

4.6         Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeendelea kutekeleza mapendekezo ya Jopo la Mapitio la Viashiria vya Uchumi Mpana kutokana na mapitio ya awali yaliyofanyika mwaka 2017.
4.7         Hivyo, uchumi wa nchi ulishuhudia ukuaji wa uchumi wa wastani wa asilimia 6.9 katika kipindi cha mwaka 2016 – 2018 ambao unaendana na shabaha ya Jopo la viashiria vya uchumi mpana la SADC wa angalau asilimia 7.
4.8         Kiwango cha Mfumuko wa bei kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kilikua wastani wa asilimia 4.4 kwa miaka minne iliyopita, ambapo kimebakia ndani ya shabaha za SADC ya asilimia 3 – 7 na chini ya shabaha ya muda wa kati ya asilimia 5.
4.9         Nakisi ya bajeti kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania iliongezeka  katika kipindi cha mapitio kutoka asilimia 1.4 ya pato la taifa mwaka 2016 hadi asilimia 2.5 mwaka 2018 na kuimarika hadi kufikia asilimia 2.3 mwaka 2019. Aidha, deni la Serikali lilifikia wastani wa asilimia 40 ya pato la taifa kati ya mwezi Juni 2016 na Juni 2019, uwiano ambao uko ndani ya ukomo uliowekwa na nchi wanachama wa SADC wa asilimia 60.

5.            Jopo lilijadili na kuidhinisha taarifa na mapendekezo ya kisera ya timu ya wataalam kwa ajili ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Vilevile, Jopo liliridhika na utayari wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kutekeleza mapendekezo hayo.
6.            Katika kuhitimisha, Jopo liliipongeza Falme ya Eswatini na Jamhuri ya Msumbiji kwa kuifanyia mapitio Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na Jamhuri ya Madagascar kwa kuifanyia mapitio Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
7.            Jopo lilikubaliana kuwa nchi za Angola, Namibia, Shelisheli na Zimbabwe zitakuwa nchi wanachama zitakazofuata kufanyiwa mapitio katika kipindi cha mwaka 2020/2021.
8.            Jopo lilitoa shukran zao za dhati kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mwenyekiti wa SADC, kwa maandalizi mazuri yaliyofanywa wakati wa mkutano.

Sekretarieti ya SADC
15 Julai 2020


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments