POLISI MWANZA WAFANIKIWA KUZUIA TUKIO LA UJAMBAZI / WIZI KATIKA BANK YA CRDB


Tukio hili limetokea usiku wa tarehe 05.07.2020 majira ya 02:00hrs katika bank ya crdb, tawi la igoma, wilaya ya nyamagana, mkoa wa mwanza, baada ya kundi la wahalifu/majambazi kuvunja kwa nyuma eneo la jengo la bank hiyo ambayo imepakana kwa karibu na majengo mengine na kufanikiwa   kukata bati la paa na dari (ceiling board) na kupata mwanya wa kuingia ndani ya benki hiyo.

Askari polisi waliokuwa lindo katika eneo hilo walibaini  kuwepo kwa  mazingira yasiyo ya kawaida, walipozungukia jengo hilo kuchunguza kwa kina walibaini kuwepo kwa mmoja wa majambazi aliyekuwa tayari ndani akijaribu  kutoka kupitia sehemu waliyovunja wakati wakiingia.

 Askari walimuamuru ajisalimishe lakini alikaidi amri hiyo halali na walimrushia risasi iliyomjeruhi  mkono  na  bega la kulia  akalazimika kurudi ndani ya bank na akakamatwa huku akiwa katika hali mbaya .

Mtuhumiwa alikimbizwa hospitali ya mkoa ya sekou toure kwa matibabu lakini kwa bahati mbaya alifariki  dunia akiwa bado  njiani,   mwili wa marehemu umehifadhiwa hospitalini hapo kusubiri uchunguzi wa daktari na utambuzi.

Uchunguzi wa awali uliofanyika eneo la tukio kwa kushirikiana na maneja wa bank hiyo umebaini kuwa licha ya wahalifu hao kuingia ndani ya bank na kuvuruga droo za ofisi hizo lakini hawakuweza kufanikiwa kuiba fedha zilizokuwa zimehifadhiwa sehemu maalum. Jeshi la polisi linaendelea na ufuatiliaji mkali wa kuhakikisha watuhumiwa wengine waloshiriki  kupanga na kujaribu kutenda tukio hili  wanakamatwa.

Jeshi la polisi mkoa wa mwanza linaendelea kutoa onyo kali kwa baadhi ya watu wanaojihusisha na vitendo vya uhalifu kutojaribu au kufanya vitendo hivyo kwani hatua  za kisheria ikiwa ni pamoja na kukamatwa zitachukuliwa dhidi yao. Pia kitendo kilichofanywa na marehemu (muhalifu) licha ya kuwa ni kosa kisheria lakini ni dharau na kejeli kwa jeshi la polisi anbalo limeapa kutovumilia vitendo vya namna hiyo.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527