WAZIRI UMMY ARIDHISHWA NA KASI YA UJENZI WA HOSPITALI YA RUFAA MTWARA


Na WAJMW-Mtwara
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu ametembelea ujenzi wa Hospitali mpya ya Rufaa ya Mikoa ya kusini iliyopo mkoani Mtwara na kuridhishwa na kasi ya ujenzi wa Hospitali hiyo.

Waziri Ummy ameonekana kuridhidhishwa na ujenzi wa Hospitali hiyo ambao umefikia asilimia 80 na inagharimu Shilingi Bilioni 15.8 mpaka kukamilika kwake.

"Kukamilika kwa Hospitali hii kutasaidia kupunguza rufaa kwa wananchi wa mikoa ya kusini kwenda kutafuta huduma za kibingwa Muhimbili, MOI au JKCI, huduma zote zitakua zinapatikana hapa". Amesema Waziri Ummy.

Waziri Ummy amesema lengo la Wizara ya Afya ni kuona huduma zinaanza kutolewa katika Hospitali hiyo kabla ya kuanza kampeni za uchaguzi mwaka huu kwani ilikua ni ahadi ya Rais Dkt. John Pombe Magufuli alipopita mwaka 2015 kuomba kura na Hospitali hiyo ipo kwenye utekelezaji wa ilani ya Chama cha Mapinduzi.

"Hatutaki watu wa Mtwara na mikoa ya kusini kwa ujumla muende Dar Es Salaam kwa ajili ya kufuata huduma za CT-Scan, huduma za madaktari bingwa ikiwemo upasuaji wa mifupa, mishipa ya fahamu, Madaktari wa watoto na uzazi. Huduma zote hizi zitapatikana hapa mara baada ya ujenzi wa Hospitali hii kukamilika". Amesema Waziri Ummy.

Waziri Ummy amesema kwa ujumla hali ya sekta ya Afya mkoani Mtwara ni nzuri ambapo katika kipindi cha miaka mitano Hospitali mpya za Wilaya tatu zimejengwa ambazo ni Nanguluwe, Nanyamba pamoja na Masasi. Aidha, vituo vya Afya vinane vimejengwa katika Mkoa huo katika kipindi hicho na kufanya idadi kufikia vituo 23 kutoka 15 wakati Rais Magufuli anaingia madarakani.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527