HALIMA BULEMBO AONGOZA KURA ZA MAONI UBUNGE UVCCM KAGERA

Na Allawi Kaboyo Bukoba.

Mchakato wa uchaguzi wa kura za maoni ndani ya Chama Cha Mapinduzi umeendelea leo julai 30 mwaka huu ili kuwapata wagombea watakao peperusha bendera ya chama hicho katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika oktoba 28 mwaka huu.

Jumuiya ya umoja wa vijana CCM nchini wamefanya uchaguzi wa kuwapata wagombea wa uwakilishi wa ubunge viti maalumu vijana ambapo kwa mkoa wa Kagera uchaguzi huo umefanyika katika ukumbi wa shule ya sekondari Bukoba ukiwajumuisha watia nia 19 huku wajumbe halali wa mkutano huo wakiwa 48.

Akitangaza matokeo ya uchaguzi huo msimamizi mkuu wa uchaguzi ambaye amekuja kwa niaba ya mkuu wa mkoa Geita Said Nkumba mkuu wa wilaya ya Bukombe amemtangaza Mhe. Halima Abdallah Bulembo mbunge aliyemaliza muda wake kuwa ameongoza kura za maoni kwa kupata kura 35 akifatiwa na Bi. Joanfaith Kataraia ambaye amepaata kura 9 na Bi.Koku Fatuma Ruta ambaye amepata kura 2, Doris Robert kura 1 na Jacrine Elias kura 1 huku wengine waliobaki wakiambulia kura 0.

Nkumba ameongeza kuwa uchaguzi huu ni mchakato wa kura za maoni hivyo mchakato mwingine unaendelea vikiwemo vikao na kuwaasa wagombea wote kushikamana na kutokata tamaa kwa matokeo huku walioongoza wasishangilie maana mchakato bado unaendelea.

Baada ya kutangazwa kwa matokeo wagombea wote wamepewa nafasi ya kushukuru ambapo wote wameahidi kutoa ushirikiano kwenye uchaguzi mkuu ambao upo mbele yao ambapo Halima Bulembo amesema kuwa yeye kama mbunge aliyemaliza muda wake na kuendelea kutetea nafasi yake kuwa ataendelea kuwatetea vijana kwenye bunge na kuhakikisha haki za vijana zinapatikana.

Awali akiongea kwenye mkutano huo mkuu wa wilaya Bukoba Deodatus Kinawiro amewasihi vijana kutunza nidhamu ya chama na kulinda misingi ya chama chao na kuhakikisha wanashinda katika uchaguzi ujao.

Kinawiro amewataka vijana hao kutotumika vibaya katika uchaguzi huu na kupelekea kujenga picha mbaya ya chama na kuwakemea kutojihusisha na vitendo vya Rushwa na kusimamia haki huku wakiwaunga mkono wagombea wote watakao letwa na chama chau kwenye uchaguzi mkuu.

“Vijana ni jeshi kubwa kwenye chama chetu na ni viongozi wa sasa na viongozi wajao, viongozi wengi mnaotuona tumepikwa kwa kupitia umoja wa vijana sasa itakuwa ni aibu kubwa kumuona kijana wa CCM akijihusisha na vitendo vya Rushwa, uvunjifu wa Amani na matukio ya hovyo.” Amesisitiza Kinawiro

Aidha Kinawiro amewataka vijana waliowawakilisha vijana wenzao kwenye uchaguzi huu kuwa wawakilishe wazuri na kuwa mfano wa kuigwa kwa vijana wa vyama vingine vya siasa.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post