BALOZI MONGELLA: ZAMA ZA ADUI WA MWANAMKE NI MWANAMKE MWENZAKE ZIMEPITWA NA WAKATI


Na Yusuph Ludimo - Mwanza
Wanawake nchini wametakiwa kuondoa dhana potofu iliyojengeka katika jamii ya kuamini kuwa mwanamke hawezi kusonga mbele bila kumkwamisha mwanamke mwenzake.

Rai hiyo imetolewa na Balozi Gertrude Mongella wakati akizungumza na wanawake kutoka viunga mbalimbali vya wilaya ya Ilemela jijini Mwanza ambapo amewataka kupendana, kusaidiana na kuungana pamoja ili kufikia malengo ya kuwa na nafasi sawa katika vyombo vya maamuzi ili waweze kujikomboa katika ukandamizaji wa kijinsia na kujiletea maendeleo.

"Mwanamke unapoona mwanamke wenzako amesimama mlangoni anataka kuingia ndani, Usimvute nje, Unachotakiwa kufanya ni kumsukuma ndani ili wote muingie, Ukimvuta nje wote mtadondoka wa nyuma yenu watawakanyaga", alisema.

Aidha Balozi Mongella amewapongeza wanawake viongozi wanaoshika nafasi mbalimbali nchini akiwemo Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto Mhe Ummy Mwalimu kwa kusimama kidete katika vita dhidi ya janga la Covid-19 na Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe Dkt Angeline Mabula kwa kusimamia vizuri sekta ya Ardhi nchini.

Akimkaribisha mgeni rasmi wa kongamano hilo, Mbunge wa Jimbo la Ilemela Mhe Dkt Angeline Mabula amewaasa wanawake walioshiriki kuhakikisha wanajitokeza kugombea nafasi mbalimbali za uongozi na kushiriki katika zoezi la kupiga kura ili kufikia lengo la kuwa na usawa katika maamuzi maarufu kama hamsini kwa hamsini pamoja na kuunga mkono jitihada za Serikali ya awamu ya tano chini ya Rais Mhe Dkt John Magufuli kwa kujadili wanawake na kuwaamini kwa Kuwateua katika nafasi mbalimbali za uongozi sanjari na kutatua changamoto zinazowakabili.

Kwa upande wake Mjumbe wa baraza la wadhamini wa CCM na Mwenyekiti mstaafu wa Umoja wa wanawake wa CCM Mhe Anna Abdallah mbali na kuelezea historia ya viongozi wanawake waliowahi kuwepo nchini, amewataka wanawake wanaojitokeza kugombea nafasi mbalimbali za uongozi kuzingatia maadili, kuwa waadilifu na kuzitendea haki nafasi wanazowania ili kuleta taswira chanya kwa jamii juu ya kuondoa dhana mbovu ya kutoamini wanawake kwa kuwaona hawawezi kufanya lolote bila ya uwepo wa mwanaume.

Akihitimisha Mkurugenzi wa shirika lisilo la KiSerikali la Kivulini lililopo jijini Mwanza Ndugu Yassin Ally amesema kuwa kongamano la kujadili nafasi ya mwanamke katika uongozi wa kisasa nchini limeandaliwa na wanawake wa wilaya ya Ilemela kwa kushirikiana na taasisi ya Kivulini likiwa na lengo la kuhamasisha mshikamano wa kuunga mkono wanawake wanaogombea, kuweka mikakati ya kuongeza nafasi za wanawake wagombea kuelekea uchaguzi mkuu na kushirikishana fursa na changamoto za uongozi wa kisasa nchini huku likipambwa na Kauli Mbiu ya MSHIKAMANO WETU, USHINDI WETU, CHUKUA HATUA

Kongamano hilo pia lilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wanawake kutoka maeneo tofauti ya mkoa wa Mwanza akiwemo akiwemo mwenyekiti wa UWT mkoani humo Mhe Hellen Bogohe na mwenyekiti wa UWT wilaya ya Ilemela Mhe Salome Kipondya na mada mbalimbali zikiwasilishwa na mchambuzi wa masuala ya kijinsia Dr Geoffrey Chambua.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527