WAZIRI MKUU KASSIM MAJALIWA ATIA SANI KITABU CHA MAOMBOLEZO KIFO CHA NKURUNZIZA

WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa leo Juni 17, 2020 ametia saini kitabu cha maombolezo ya kifo cha aliyekuwa Rais wa Burundi Pierre Nkurunziza na kutoa pole kwa wananchi wa nchi hiyo kwa niaba ya Rais Dkt. John Pombe Magufuli.


“Kwa niaba ya Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli nimekuja hapa kutoa pole na salamu za rambirambi kwa Serikali na wananchi wa Burundi kufuatia kifo cha aliyekuwa rais wa nchi ya Burundi. Mheshimiwa Rais na Watanzania wote tumepokea kwa mshituko na masikitiko makubwa taarifa za kifo chake.”

Waziri Mkuu ameyasema hayo leo (Jumatano, Juni 17, 2020) akiwa katika Ofisi za Ubalozi wa Burundi, Upanga jijini Dar es Salaam baada ya kusaini kitabu cha maombolezo ya kifo cha aliyekuwa Rais wa Burundi, Pierre Nkurunziza aliyefariki Juni 9, 2020 kutokana na mshituko wa moyo.

Amesema Tanzania na Burundi ni nchi zenye historia ndefu na mshikamano wa muda mrefu, hivyo ametumia fursa hiyo kuwasihi wananchi wa Burundi wawe watulivu katika kipindi hiki cha majonzi. “Serikali ya Tanzania itaendelea kudumisha umoja na mshikamano kati yake na Burundi.”

Awali, Balozi wa Burundi nchini Tanzania, Balozi Abayeho Gervais ametumia fursa hiyo kumshukuru Rais wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli kwa ushirikiano mkubwa anaoutoa kwa Taifa hilo na kwamba anatarajia umoja na mshikano huo utadumu milele na milele.

“Tunamshukuru Rais wa Tanzania amepeleka ujumbe mkubwa Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan na Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete nchini Burundi kwa ajili ya kushuhudia uapishwaji wa Rais wa Burundi Evariste Ndayishimiye ambaye anatarajiwa kuapishwa kesho Juni 18.

Akizungumzia kuhusu kifo cha aliyekuwa rais wa nchi hiyo Balozi Gervais amesema wamepokea kwa mshtuko mkubwa kwa sababu alikuwa bado ni kijana akiendelea kufanya shughuli zake. “Hii yote ni mipango ya Mwenyezi Mungu na sote tupo safarini.”

Mwisho.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post