TAARIFA YA HALI YA UCHUMI WA TAIFA KWA MWAKA 2019 NA MPANGO WA MAENDELEO WA TAIFA WA MWAKA 2020/21 WAWASILISHWA BUNGENI

UTANGULIZI


1.          Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja kwamba Bunge lako Tukufu lipokee na kujadili Taarifa ya Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2019 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2020/21. Pamoja na hotuba hii ninawasilisha vitabu vya Taarifa ya Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2019 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2020/21. Taarifa hizi ndiyo msingi wa bajeti ya Serikali kwa mwaka 2020/21 nitakayowasilisha hapa Bungeni leo jioni.  


2.          Mheshimiwa Spika, awali ya yote nichukue fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuendelea kutujalia afya njema. Aidha, naendelea kumshukuru kwa kulijalia Taifa letu amani, utulivu na mshikamano na kutuwezesha kukutana katika mkutano huu wa 19 na wa mwisho wa Bunge la 11 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ili kujadili namna ya kuharakisha maendeleo ya Taifa letu.

3.          Mheshimiwa Spika, naomba nimpongeze kwa dhati Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa jinsi anavyoendelea kuliongoza vema Taifa letu. Kwa kipindi hiki cha miaka minne na nusu ya utawala wake tumeshuhudia kuimarika kwa uchumi, mfumuko wa bei umedhibitiwa, miradi mikubwa ya maendeleo inatekelezwa, uwajibikaji katika utumishi wa umma umeimarika na kero za wananchi wanyonge zinatatuliwa. Kipekee napenda kumshukuru Mheshimiwa Rais kwa kuniamini kuongoza Wizara ya Fedha na Mipango tangu mwanzo wa uongozi wake hadi sasa.

4.          Mheshimiwa Spika, vile vile, napenda kuwapongeza Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa (Mb), Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambao kwa uongozi wao mahiri wameendelea kumshauri vema Mheshimiwa Rais katika kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi mkubwa.

5.          Mheshimiwa Spika,Napenda pia kuwapongeza Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), kwa kuteuliwa na Mheshimiwa Rais kuwa Waziri wa Katiba na Sheria pamoja na Mheshimiwa Dkt. Godwin Aloyce Mollel (Mb), kwa kuteuliwa na Mheshimiwa Rais kuwa Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto.

6.          Mheshimiwa Spika, napenda pia nitumie nafasi hii kutoa salamu za pole kwako, Waheshimiwa Wabunge na Wananchi wote kwa ujumla kwa kuondokewa na Mheshimiwa Rashid Ajali Akbar, aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Newala Vijijini (CCM), Mheshimiwa Mchungaji  Dkt. Getrude Pangalile Rwakatare, aliyekuwa Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Mheshimiwa Richard Mganga Ndassa, aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Sumve (CCM), na Mheshimiwa Balozi Dkt. Augustine Philip Mahiga, Mbunge wa kuteuliwa (CCM) aliyekuwa Waziri wa Katiba na Sheria. Mwenyezi Mungu azilaze roho za marehemu mahali pema peponi. Amina!

7.          Mheshimiwa Spika, nchi yetu imepata mvua nyingi zilizo juu ya wastani hali iliyopelekea kutokea kwa mafuriko katika maeneo mbalimbali. Mafuriko haya yamesababisha uharibifu mkubwa wa mazao ya wakulima, mali na miundombinu hususan barabara, reli na madaraja. Mafuriko hayo yameathiri utelekelezaji wa miradi ya maendeleo na kuongeza gharama za ukarabati wa miundombinu iliyoharibika. Kwa msingi huo, katika mwaka 2020/21 kipaumbele ni kukarabati miundombinu iliyoharibika.

8.          Mheshimiwa Spika, kama unavyofahamu, nchi yetu na dunia kwa ujumla ilikabiliwa na mlipuko wa ugonjwa wa homa kali ya mapafu unaojulikana kama COVID - 19 inayosababishwa na virusi vya Corona. Ni dhahiri kuwa ugonjwa huu umeathiri uchumi wa nchi nyingi duniani kutokana na vifo, kuongezeka kwa gharama za utoaji huduma katika sekta ya afya na kuathiri shughuli za biashara na uzalishaji hususan kwa nchi zinazotegemea utalii.

9.          Mheshimiwa Spika, jambo jema ni kuwa nchi yetu haikuathirika sana na ugonjwa huu kutokana na hatua madhubuti zilizochukuliwa na Serikali ya Awamu ya Tano chini ya uongozi imara wa Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kama Taifa tuliendelea kumtegemea Mwenyezi Mungu, kuchukua tahadhari za kiafya kama inavyoshauriwa na wataalam pamoja na kufanya kazi kwa bidii. Aidha, Serikali imeendelea kuchukua hatua mbalimbali za kukabiliana na ugonjwa huu ambapo hadi sasa Serikali imetoa kiasi cha shilingi bilioni 15.49 kwa  ajili ya ununuzi wa vifaa tiba na kinga. Hatua nyingine ni pamoja na: kutolewa msamaha wa kodi kwa aina 15 za vifaa vya kupambana na COVID – 19; kutoa elimu ya jinsi ya kujikinga na maambukizi; kutenga maeneo maalum kwa ajili ya uangalizi kwa wasafiri wanaoingia nchini na wanaobainika kuwa na dalili za ugonjwa huu; na kuanzishwa kwa huduma ya namba maalum ya kupiga simu bila malipo kwa ajili ya msaada wa kiafya. Vile vile, Serikali kupitia Benki Kuu ya Tanzania imechukua hatua mbalimbali za Sera ya Fedha ili kulinda na kuimarisha uchumi zikijumuisha: kushusha kiwango cha chini cha kisheria cha sehemu ya amana kinachotakiwa kuwekwa Benki Kuu ya Tanzania kutoka asilimia 7 hadi 6; kushusha kiwango cha riba kinachotozwa kwa benki kukopa Benki Kuu kutoka asilimia 7 hadi 5; kupunguza kiwango cha dhamana za Serikali kutoka asilimia 10 hadi 5 kwa dhamana za muda mfupi na kutoka asilimia 40 hadi 20 kwa hati fungani; na kuzielekeza kampuni zinazotoa huduma za fedha kwa njia ya mtandao kuongeza kiwango cha miamala kwa siku kwa mteja kutoka shilingi milioni 3 hadi 5 na kiwango cha akiba kwa siku kwa wateja kutoka shilingi milioni 5 hadi 10.

10.      Mheshimiwa Spika, kutokana na hatua madhubuti zilizochukuliwa na Serikali, hivi sasa hali imeimarika ambapo shughuli za kiuchumi na kijamii zinaendelea kufanyika kama awali. Serikali imeruhusu vyuo vikuu vimefunguliwa, wanafunzi wa kidato cha sita wamerudi shuleni kujiandaa na mitihani, shughuli za michezo yote zimeruhusiwa,  anga limefunguliwa ambapo ndege za mizigo na abiria zinaendelea kuingia nchini na hivyo kupokelewa kwa watalii kutoka nchi mbalimbali. Hii ni ishara dhahiri ya uongozi imara wa Mheshimiwa Rais kwa Taifa hususan katika kipindi cha majanga na misukosuko mikubwa kwa dunia kama ugonjwa huu.

11.      Mheshimiwa Spika, Taarifa ya Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2019 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2020/21 zimezingatia dhana ya ushirikishwaji mpana wa wadau katika hatua za uandaaji na maamuzi katika ngazi zote Serikalini. Nitambue mchango mkubwa wa Bunge lako Tukufu chini ya uongozi wako Mheshimiwa Job Yustino Ndugai, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na Mheshimiwa Dkt. Tulia Ackson, Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Aidha, napenda kumshukuru Mheshimiwa Mashimba Mashauri Ndaki (Mb), Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti na wajumbe wote wa Kamati hiyo kwa ushauri makini waliotupatia. Ushauri wao umezingatiwa kikamilifu katika uandaaji wa taarifa nilizowasilisha mbele ya Bunge hili.

12.      Mheshimiwa Spika, maandalizi ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2020/21 yamezingatia vipaumbele vya Serikali ya Awamu ya Tano vilivyoainishwa katika Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2016/17 – 2020/21, Ilani ya CCM ya Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2015 na ahadi za Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alizotoa wakati akifungua rasmi Bunge la Kumi na Moja. Aidha, katika mwaka 2020/21 msukumo mkubwa utawekwa katika kukamilisha utekelezaji wa miradi inayoendelea ili kupata matokeo tarajiwa.

MWENENDO WA HALI YA UCHUMI 2019

Uchumi wa Dunia

13.      Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa taarifa ya Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) ya Aprili 2020, uchumiwa dunia ulikua kwa asilimia 2.9 mwaka 2019. Aidha, uchumi wa dunia unakadiriwa kuporomoka na kufikia ukuaji wa asilimia hasi 3.0 mwaka 2020 ambao kwa kiasi kikubwa utachangiwa na athari za mlipuko wa ugonjwa wa COVID - 19. Katika mwaka 2021 uchumi wa dunia unatarajiwa kuimarika na kufikia ukuaji wa asilimia 5.8 kutokana na matarajio ya kutoweka kwa virusi vya Corona katika nusu ya pili ya mwaka 2020 na hatimaye, kuimarika kwa shughuli za kiuchumi duniani ikijumuisha biashara na uzalishaji viwandani na utekelezaji wa sera za kuongeza ukwasi katika nchi mbalimbali.

Uchumi wa Afrika na Kikanda

14.      Mheshimiwa Spika, kwa upande wa nchi za Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara, kasi ya ukuaji wa uchumi ilifikia asilimia 3.1 mwaka 2019. Matarajio ya ukuaji wa uchumi ni kupungua na kufikia wastani wa asilimia hasi 1.6 mwaka 2020 kutokana na athari za mlipuko wa ugonjwa wa COVID – 19. Aidha, ukuaji wa uchumi katika nchi za ukanda huo, unatarajiwa kuimarika na kufikia wastani wa asilimia 4.1 mwaka 2021. Ongezeko hilo litatokana na jitihada za kupambana na ugonjwa wa COVID – 19, matarajio ya kuongezeka kwa misaada kutoka nchi zilizoendelea kwa ajili ya kupambana na ugonjwa huo na matarajio ya utulivu wa bei ya nishati ya mafuta katika soko la Dunia.

15.      Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2019, uchumi wa nchi za ukanda wa Jumuiya ya Afrika Mashariki uliendelea kuimarika ambapo Tanzania ilikuwa na ukuaji wa asilimia 7.0, Rwanda asilimia 9.4, Uganda (asilimia 4.9) na Kenya asilimia 5.4. Aidha, kutokana na athari za COVID-19, ukuaji wa uchumi wa ukanda wa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki unatarajiwa kupungua kidogo kwa mwaka 2020 na hatimaye kuanza kuimarika mwaka 2021 kutokana na juhudi zinazochukuliwa na nchi wanachama katika kupambana na athari za COVID-19 zikiwemo hatua za kifedha na kibajeti pamoja na utekelezaji wa miradi mikubwa ya maendeleo katika sekta za uchukuzi (reli, barabara na madaraja) maji, nishati, elimu na afya.

Uchumi wa Taifa

Pato la Taifa

16.      Mheshimiwa Spika, mwaka 2019, Pato la Taifa lilikua kwa asilimia 7.0 kama ilivyokuwa mwaka 2018. Ukuaji huu ulitokana na uwekezaji hususan katika miundombinu ikiwemo: ujenzi wa barabara, reli na viwanja vya ndege; kutengamaa kwa upatikanaji wa nishati ya umeme; kuimarika kwa huduma za usafirishaji; kuongezeka kwa uzalishaji wa madini hususan dhahabu na makaa ya mawe; na kuongezeka kwa uzalishaji wa mazao ya kilimo. Sekta zilizokua kwa viwango vikubwa katika kipindi hicho ni pamoja na uchimbaji madini na mawe (asilimia 17.7), ujenzi (asilimia 14.8), sanaa na burudani (asilimia 11.2), na usafirishaji na uhifadhi mizigo (asilimia 8.7). Kwa mwaka 2020, ukuaji wa Pato la Taifa unatarajiwa kupungua kidogo kutoka maoteo ya awali ya asilimia 6.9 hadi 5.5 kutokana na hatua madhubuti zilizochukuliwa na Serikali ya Awamu ya Tano chini ya uongozi wa Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hususan kuhimiza wananchi waendelee kufanya kazi wakati wanachukua tahadhari dhidi ya corona kama inavyoelekezwa na wataalam wa afya pamoja na matarajio ya kuimarika kwa uchumi wa kikanda na dunia.

17.      Mheshimiwa Spika, mwaka 2019, Pato la wastani la kila mtu lilikuwa shilingi 2,577,967 ikilinganishwa na shilingi 2,452,406 mwaka 2018, sawa na ongezeko la asilimia 5.1. Vile vile, Pato la wastani kwa kila mtu katika dola za Marekani liliongezeka hadi kufikia dola za Marekani 1,121 mwaka 2019 kutoka dola za Marekani 1,078 mwaka 2018.

Mwenendo wa Bei

18.      Mheshimiwa Spika, mwaka 2019, mwenendo wa mfumuko wa bei uliendelea kubaki katika wigo wa tarakimu moja ambapo ulifikia wastani wa asilimia 3.4 ikilinganishwa na wastani wa asilimia 3.5 mwaka 2018. Mfumuko wa bei za nishati umeendelea kupungua na kufikia asilimia 4.1 Aprili 2020 kutoka asilimia 13.3 Aprili 2019 kutokana na kupungua kwa bei za nishati ya mafuta katika soko la dunia.

Utekelezaji wa Sera ya Fedha 2019/20

19.      Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Benki Kuu imeendelea kutekeleza sera ya fedha ya kuongeza ukwasi kwenye uchumi ambayo imesaidia kupunguza viwango vya riba katika masoko ya fedha hususan riba za mikopo na amana. Wastani wa riba za mikopo ya benki kwa ujumla katika kipindi cha Julai 2019 hadi Aprili 2020 ulipungua hadi asilimia 16.85 ikilinganishwa na wastani wa asilimia 17.16 katika kipindi kama hicho mwaka 2018/19, na riba za mikopo ya kipindi cha mwaka mmoja zimepungua na kufikia wastani wa asilimia 16.24 kutoka asilimia 17.79. Vile vile, wastani wa riba za amana kwa ujumla ulikuwa asilimia 7.02 katika kipindi cha Julai 2019 hadi Aprili 2020, ikilinganishwa na wastani wa asilimia 7.62 katika kipindi kama hicho mwaka 2018/19. Aidha, riba za amana za kipindi cha mwaka mmoja ziliongezeka na kufikia wastani wa asilimia 8.77 katika kipindi cha Julai 2019 hadi Aprili 2020 kutoka wastani wa asilimia 8.21 katika kipindi kama hicho mwaka 2018/19.

Ujazi wa Fedha na Karadha

20.      Mheshimiwa Spika, Katika kipindi cha Julai 2019 hadi Aprili 2020, wastani wa ukuaji wa ujazi wa fedha kwa tafsiri pana zaidi (M3) uliongezeka kwa asilimia 9.9 na kufikia shilingi trilioni 28.8 mwezi Aprili 2020 kutoka shilingi trilioni 25.6 mwezi Aprili 2019. Ongezeko hili la ujazi wa fedha ni matokeo ya utekelezaji thabiti wa sera ya fedha, ongezeko la mikopo kwa sekta binafsi pamoja na rasilimali fedha za kigeni katika sekta ya benki.

Mwenendo wa Mikopo kwa Sekta Binafsi

21.      Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha Julai 2019 hadi Aprili 2020, wastani wa ukuaji wa mikopo kwa sekta binafsi ulikuwa asilimia 8.7 kufikia shilingi trilioni 19.7 ikilinganishwa na shilingi trilioni 18.6 Aprili 2019. Sehemu kubwa ya mikopo ilielekezwa kwenye shughuli binafsi (asilimia 31.1) ikifuatiwa na shughuli za biashara asilimia 17.6, uzalishaji viwandani asilimia 11.0 na kilimo asilimia 7.7.

Sekta ya Nje

22.      Mheshimiwa Spika, hadi Aprili 2020, urari wa jumla wa malipo ulikuwa na ziada ya dola za Marekani milioni 897.1 ikilinganishwa na nakisi ya dola za Marekani bilioni 1.1 katika kipindi kama hicho mwaka 2019. Hii ilichangiwa na kupungua kwa nakisi ya urari wa biashara ya bidhaa, huduma na uhamisho wa mali nchi za nje kulikotokana na kuongezeka kwa mauzo ya bidhaa nje ya nchi.

23.      Mheshimiwa Spika, nakisi kwenye urari wa biashara ya bidhaa, huduma na uhamisho mali nchi za nje ulipungua hadi kufikia dola za Marekani milioni 333.3 mwezi Aprili 2020, ikilinganishwa na nakisi ya dola za Marekani bilioni 1.6 katika kipindi kama hicho mwaka 2019. Kupungua huku kulitokana na kuongezeka kwa mauzo ya bidhaa nje ya nchi, hususa katika bidhaa asilia na zisizo asilia kama vile dhahabu.

24.      Mheshimiwa Spika, hadi Aprili 2020, mauzo ya bidhaa na huduma nje yaliongezeka kufikia dola za Marekani bilioni 8.6 ikilinganishwa na dola za Marekani bilioni 7.3 Aprili 2019. Hii ilichangiwa na kuanzishwa kwa masoko ya madini nchini kulikopelekea kuongezeka kwa mauzo ya dhahabu sanjari na ongezeko la bei katika soko la dunia. Thamani ya uagizaji bidhaa na huduma kutoka nje ya nchi ilikuwa dola za Marekani bilioni 8.6, ikilinganishwa na dola za Marekani bilioni 8.7 katika kipindi kama hicho mwaka 2019. Sehemu kubwa ilitumika katika uagizaji mafuta na bidhaa za mitaji ikiwemo mitambo na mashine inayotumika katika utekelezaji wa miradi mikubwa ya miundombinu ya reli, barabara, madaraja na uzalishaji umeme.

Akiba ya Fedha za Kigeni

25.      Mheshimiwa Spika, hadi Aprili 2020, akiba ya fedha za kigeni ilifikia dola za Marekani bilioni 5.3, kiasi kinachotosheleza kulipia uagizaji wa bidhaa na huduma kutoka nje ya nchi kwa kipindi cha miezi 6.1. Kiwango hiki ni zaidi ya lengo la nchi la miezi 4.0, ambayo ni juu ya lengo la nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki la miezi isiyopungua 4.5 na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika la miezi isiyopungua 6.0.

Mwenendo wa Thamani ya Shilingi

26.      Mheshimiwa Spika, thamani ya shilingi ya Tanzania dhidi ya sarafu nyingine kubwa duniani imeendelea kuwa tulivu kwa kipindi chote cha mwaka 2019/20. Katika kipindi cha Julai 2019 hadi Aprili 2020, dola moja ya Marekani ilibadilishwa kwa wastani wa kati ya shilingi 2,299.3 na shilingi 2,302.7 katika soko la fedha la jumla ikilinganishwa na wastani wa kati ya shilingi 2,276.4 na shilingi 2,300.9 kwa dola moja ya Marekani katika kipindi kama hicho mwaka 2018/19.

Deni la Serikali

27.      Mheshimiwa Spika, hadi Aprili 2020, deni la Serikali lilifikia shilingi trilioni 55.43. Kati ya kiasi hicho, deni la nje lilikuwa shilingi trilioni 40.57 na deni la ndani shilingi trilioni 14.85. Deni la Serikali lilichangiwa na kupokelewa kwa mikopo mipya kwa ajili ya kugharamia miradi mbalimbali ya maendeleo inayochochea kasi ya ukuaji wa uchumi. Matokeo ya tathmini ya uhimilivu wa deni iliyofanyika Desemba 2019, imeonesha kuwa deni la Serikali ni himilivu katika kipindi cha muda mfupi, wa kati na mrefu.

Utafiti wa Sekta Isiyo Rasmi    

28.      MheshimiwaSpika, mwaka 2019/20, Serikali ilifanya utafiti wa Sekta Isiyo Rasmi mkoani Dar es Salaam kwa lengo la kubaini mchango wa sekta hiyo kwenye Pato la Taifa kwa kutumia makadirio ya mapato na ongezeko la thamani ya uzalishaji wa bidhaa na huduma kutoka shughuli za kilimo na zisizo za kilimo; tija katika uwekezaji; kiwango cha ukuzaji mtaji; kutambua mahali biashara zilipo; thamani ya uzalishaji kwa kila mtu; ajira na mgawanyo wake; na mahusiano kati ya Sekta Isiyo Rasmi na sekta nyingine za kiuchumi.

29.      MheshimiwaSpika, matokeo ya utafiti huo yanaonesha kuwa: Mkoa wa Dar es Salaam una wamiliki wa shughuli za Sekta Isiyo Rasmi wapatao 1,023,520 ambapo asilimia 47.6 wanajihusisha na biashara ya jumla na rejareja pamoja na matengenezo ya magari na pikipiki;   uwekezaji wa mitaji katika sekta isiyo rasmi ni shilingi bilioni 901.5 kwa mwaka 2019; jumla ya ongezeko la thamani kwa mwaka katika bidhaa na huduma zinazozalishwa katika sekta isiyo rasmi ni shilingi trilioni 6.2; na ajira katika sekta isiyo rasmi kwa watu wenye umri wa miaka 15 au zaidi imepungua kutoka watu 1,208,250 (asilimia 61.5) mwaka 2014 hadi 1,154,336 (asilimia 55.2) mwaka 2019. Hii inatokana na juhudi kubwa za Serikali ya Awamu ya Tano katika kupanua wigo wa kujenga uchumi wa viwanda ambao matokeo yake ni kukuza upatikanaji wa kazi zenye staha (decent work) na kuongezeka kwa ajira katika sekta rasmi.

30.      Mheshimiwa Spika, maelezo ya kina kuhusu hali ya uchumi yapo katika Aya ya 9 hadi 26 ya hotuba yangu na kitabu cha Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2019.

MAFANIKIO YA UTEKELEZAJI WA MPANGO KWA KIPINDI CHA 2016/17 – 2019/20

31.      Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha miaka minne na nusu ya utawala wa Serikali ya Awamu ya Tano (2016/17 – 2019/20), yamepatikana mafanikio mbalimbali katika utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo yakiwemo:

(i)          Ukuaji wa Uchumi: uchumi wa Taifa uliendelea kuimarika ambapo ulikua kwa wastani wa asilimia 6.9 na mfumuko wa bei kuendelea kupungua na kubaki katika wigo wa tarakimu moja, chini ya wastani wa asilimia 5.0;(iii)        Mradi wa Kuzalisha Umeme wa Julius Nyerere – MW 2,115: Kazi zilizokamilika ni pamoja na ujenzi wa miundombinu wezeshi ya mradi (njia ya kusafirisha umeme, barabara kwa kiwango cha changarawe, mfumo wa maji, mawasiliano ya simu na nyumba za makandarasi); ujenzi wa daraja la muda namba 2; utafiti wa miamba na udongo; na uchimbaji wa mtaro wa chini kwa chini (adit tunnel) wenye urefu wa mita 147.6 na mtambo wa kuchakata kokoto namba moja ambapo utekelezaji wa mradi wote umefikia asilimia 10.74. Aidha, jumla ya shilingi trilioni 1.42 zimetumika kugharamia mradi na ajira zipatazo 3,897 zimezalishwa;

(iv)       Nishati: kukamilika kwa mradi wa njia ya kusafirisha umeme wa Msongo wa kV 220 kutoka Makambako – Songea ambapo shilingi bilioni 160.1 zimetumika; kuendelea na ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme wa kV 400 kutoka Singida – Arusha – Namanga ambapo utekelezaji umefikia asilimia 67 na shilingi bilioni 219.4 zimetumika; kuendelea na utekelezaji wa miradi ya usambazaji umeme vijijini kupitia REA ambapo shilingi trilioni 2.27 zimetumika jumla ya vijiji 9,112 kati ya vijiji 12,268 vya Tanzania Bara vimeunganishwa umeme, sawa na asilimia 74.3. Hadi Mei 2020, kiwango cha upatikanaji wa umeme (overall electricity access rate) kimefikia asilimia 84.6 kutoka asilimia 67.8 mwaka 2016;

(v)        Kuboresha Shirika la Ndege Tanzania: Serikali imeendelea kuboresha Shirika la Ndege kwa kununua ndege mpya 11. Kati ya hizo, ndege nane (8) zenye thamani ya shilingi trilioni 1.27 zimepokelewa na malipo ya awali ya shilingi bilioni 85.7 kwa ajili ya ununuzi wa ndege nyingine mpya tatu (3) yamefanyika ambapo ndege mbili (2) ni aina ya Airbus A220-300 na moja (1) ni aina ya De Havilland Dash 8-400;

(vi)       Viwanja vya Ndege: kukamilika kwa ujenzi na ukarabati wa viwanja vya Ndege vya Mwanza awamu ya kwanza, Nachingwea na Kilimanjaro (KIA); kuendelea na ujenzi na ukarabati wa viwanja vya Geita (asilimia 78) na Songea (asilimia 34). Aidha, ujenzi wa Jengo la Tatu la Abiria katika Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere umekamilika na kuanza kutumika ambapo kiasi cha Euro milioni 276 sawa na takribani shilingi bilioni 722.1 zilitumika;

(vii)      Bandari: kukamilika kwa ujenzi wa Gati Na.1, 2, 3, 4 na Gati la kupakia na kupakua magari (Ro-Ro) katika bandari ya Dar es Salaam; ujenzi wa gati lenye urefu wa mita 300 katika bandari ya Mtwara umefikia asilimia 61; na kukamilika kwa uongezaji wa kina cha bandari ya Tanga na ujenzi wa Gati namba 2 umefikia asilimia 60. Aidha, kwa upande wa Bandari za Maziwa Makuu: katikaZiwa Victoria - ujenzi wa magati ya Lushamba, Ntama,  Nyamirembe, Magarine na Gati la majahazi Mwigobero umekamilika; kununuliwa kwa vifaa vya kuhudumia mizigo na meli; na ukarabati wa majengo na ofisi za bandari. Ziwa Tanganyika - uboreshaji wa Gati la Kagunga umekamilika; ujenzi wa Gati la Sibwesa umefikia asilimia 98; ujenzi wa miundombinu na Gati la Bandari ya Kabwe umefikia  asilimia 56; na ujenzi wa miundombinu na Gati la Bandari ya Lagosa umefikia asilimia 53. Ziwa Nyasa - ujenzi wa sakafu ngumu kwa ajili ya maegesho katika bandari ya Kiwira; na ujenzi wa Gati la Ndumbi umekamilika;

(viii)    Ujenzi na Ukarabati wa Meli katika Maziwa Makuu: kukamilika kwa ujenzi wa meli moja mpya yenye uwezo wa kubeba abiria 200 na mizigo tani 200 katika Ziwa Nyasa, ukarabati wa meli ya MV Victoria katika ziwa Victoria na meli ya mafuta ya MT. Sangara katika Ziwa Tanganyika; kukamilika kwa asilimia 98 ya ujenzi wa Chelezo na MV Butiama asilimia 98; na kuendelea na ujenzi wa meli mpya (MV Mwanza) yenye uwezo wa kubeba abiria 1,200 na tani 400 za mizigo katika Ziwa Victoria ambapo utekelezaji umefikia asilimia 60;

(ix)       Barabara na Madaraja: ujenzi wa Barabara:kukamilika kwa ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami zenye urefu wa jumla ya kilometa 2,624.27 na kuendelea na ujenzi wa barabara kuu kwa kiwango cha lami zenye urefu wa kilometa 1,298.44; barabara ya njia nane kutoka Kimara hadi Kibaha (km 19.2) umefikia asilimia 80; na ujenzi wa Ubungo Interchange umefikia asilimia 77. Madaraja: kukamilika kwa ujenzi wa madaraja ya Mfugale (Dar es Salaam), Magufuli katika mto Kilombero (Morogoro), Momba (Rukwa), Sibiti (Singida), Mara (Mara), Lukuledi (Lindi), Mangara (Manyara) na Kavuu (Katavi); kuendelea na ujenzi wa madaraja ya Kitengule (Kagera) asilimia 50, Ruhuhu (Ruvuma) asilimia 86, Msingi (Singida) asilimia 40, New Wami (Pwani) lenye urefu wa mita 513.5 na barabara unganishi zenye kilomita 4.3 umefikia asilimia 39 na daraja jipya la Selander lenye urefu wa kilomita 1.03 na barabara unganishi zenye kilomita 5.2 umefikia asilimia 38.2; na kuanza kwa ujenzi wa daraja la Kigongo – Busisi (Mwanza) lenye urefu wa kilomita 3.2  ambapo malipo ya awali ya shilingi bilioni 61.4 yamefanyika.

(x)         Kilimo, Mifugo na Uvuvi: katika Kilimo,miche bora ya korosho 12,252,197 imezalishwa na mbolea tani 519,813 imesambazwa katika mikoa 26 ya Tanzania Bara; na kuongezeka kwa upatikanaji wa mbegu bora za mahindi, ngano, maharage, mpunga, soya, alizeti, mtama, ufuta, viazi mviringo na mazao ya bustani kufikia tani 49,040.66. Aidha, kupitia Mradi wa Kuongeza Uzalishaji wa Mpunga (ERPP), shughuli zifuatazo zimetekelezwa: ukarabati wa miundombinu ya umwagiliaji katika skimu za Kigugu -  Mvomero (hekta 200) asilimia 50, Mvumi - Kilosa (hekta 249) asilimia 84, Kilangali – Kilosa (hekta 600) asilimia 51, Msolwa Ujamaa - Kilombero (hekta 675) asilimia 40 na Njage - Kilombero (hekta 325) asilimia 84. Mifugo: kuendelezwa kwa mashamba matano (5) ya kuzalisha mitamba; kuzalishwa na kusambazwa kwa mitamba 15,097 ya ng’ombe wa maziwa; kununuliwa na kusambazwa kwa lita 8,823.53 za dawa aina ya Paranex ya kuogesha mifugo; kukarabatiwa kwa majosho 1,129; na kutolewa kwa chanjo ya ndigana kali (east coast fever) kwa ng’ombe 70,260. Uvuvi: uzalishaji wa vifaranga 15,041,401 vya samaki; na kuongezeka kwa uvunaji wa samaki (maji ya asili) kufikia tani 470,309.23;

(xi)       Miradi ya Afya: ujenzi na uboreshaji wa miundombinu ya vituo  vya kutolea huduma za afya ya msingi nchini ikijumuisha vituo vya afya 487, hospitali za wilaya 71, hospitali za rufaa za mikoa 10 na zahanati 1,198; kuongezeka kwa bajeti ya dawa, vifaa, vifaa tiba na vitendanishi kutoka shilingi bilioni 31 mwaka 2015/16 hadi shilingi bilioni 269 mwaka 2019/20; kujenga na kuboresha miundombinu ya hospitali za rufaa za Njombe, Simiyu, Mara, Geita, Songwe, Katavi, Sekou Toure (Mwanza), Burigi - Geita, Mwananyamala – Dar es Salaam na hospitali za rufaa za kanda ya kusini Mtwara, kanda ya nyanda za juu kusini Mbeya, hospitali ya Kibong’oto na ujenzi wa Kituo Maalum cha kutenga wagonjwa wa magonjwa yanayoambukiza (Isolation Centre) katika hospitali ya Taifa Muhimbili, Temeke, na Maabara ya Taifa Mabibo; na ununuzi wa dawa, chanjo, vifaa, vifaa tiba na vitendanishi ikijumuisha vifaa tiba vya kisasa katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete.

(xii)      Miradi ya Elimu: kukamilika na kuanza kutumika kwa Maktaba ya Kimataifa yenye uwezo wa kuhudumia wanafunzi 2,600 kwa wakati mmoja katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam; kuendelea na ujenzi wa maabara ya masomo ya Sayansi katika Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (Kampasi ya Solomon Mahlangu), ujenzi wa hosteli za Dkt. John Pombe Joseph Magufuli Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na hosteli za wanafunzi na Maktaba katika Chuo Kikuu Mzumbe (kampasi ya Mbeya); utoaji wa mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu kutoka shilingi bilioni 365 mwaka 2015/16 hadi shilingi bilioni 450 mwaka 2019/20; uimarishaji wa vyuo vya VETA na kukuza ujuzi kwa vijana nchini; na ukamilishaji wa maboma 364 ya nyumba za walimu wa shule za msingi kwenye maeneo yenye mazingira magumu na kuendelea kugharamia elimumsingi bila ada ambapo shilingi trilioni 1.03 zimetumika kuanzia mwaka 2015 hadi Mei 2020.

(xiii)     Miradi ya Maji Mijini na Vijijini: Serikali imeendelea kuboresha huduma za maji safi na salama vijijini na mijini ambapo miradi 1,423 (vijijini 1,268 na mijini 155) imetekelezwa na kukamilika kati ya mwaka 2015 na 2019. Miradi hiyo inajumuisha: mradi wa kutoa maji kutoka Ziwa Victoria hadi miji ya Isaka, Tinde, Kagongwa, Tabora, Igunga, Uyui na Nzega ambapo ujenzi wa matanki 17 na ulazaji wa mabomba makubwa ya kusafirisha maji kutoka kijiji cha Solwa – Nzega – Tabora – Igunga (km 290.7) umekamilika. Utekelezaji wa miradi ya maji umewezesha kiwango cha upatikanaji wa maji kufikia asilimia 70.1 vijijini na asilimia 84 mijini;

(xiv)    Madini: Mafanikio yaliyopatikana ni pamoja na marekebisho ya sheria na mikataba ya uwekezaji katika sekta ya madini na hivyo kuanzishwa kwa Kampuni mpya ya Twiga Minerals Corporation Limited inayomilikiwa kwa ubia kati ya Serikali (hisa asilimia 16) na Kampuni ya Barrick (hisa asilimia 84); na kufanyika kwa malipo ya fidia ya dola za Marekani milioni 100 kutoka Kampuni ya Barrick ikiwa ni sehemu ya kwanza  ya kiasi cha makubaliano ya awali ya kulipa fidia ya dola za Marekani milioni 300. Aidha, marekebisho ya Sheria yamewezesha kuanza kwa majadiliano baina ya Serikali na Makampuni yote makubwa ya madini kwa lengo la kupata asilimia 16 ya hisa kwa Serikali. Mafanikio mengine ni kuanzishwa kwa masoko 28 na vituo 25 vya ununuzi wa madini nchini; kukamilika kwa ujenzi wa vituo vinne (4) vya umahiri katika maeneo ya Bukoba, Handeni, Bariadi na Musoma; kukamilika kwa ujenzi wa viwanda viwili (2) vya mfano vya kuchenjua dhahabu vya Lwamgasa na Katente; kukamilika kwa ujenzi wa one stop center Mirerani, kuimarika kwa udhibiti wa madini ikijumuisha ujenzi wa ukuta wa Mirerani uliowezesha  kupungua kwa utoroshaji madini;  na kuongezeka kwa maduhuli ya Serikali kutoka shilingi bilioni 196 mwaka 2015/16 hadi zaidi ya shilingi bilioni 470 mwaka 2019/20;  na

(xv)     Uendelezaji wa Viwanda: kufanikisha ujenzi wa viwanda vipya 8,477 ambapo viwanda vikubwa ni 201, vya kati 460, vidogo 3,406 na vidogo sana 4,410. Mafanikio mengine ni pamoja na upanuzi wa Kiwanda cha Ngozi na Bidhaa za Ngozi cha Karanga (Moshi) na kuimarisha Shirika la Nyumbu (Pwani).

32.      Mheshimiwa Spika, maelezo ya kina kuhusu mafanikio ya utekelezaji wa Mpango yapo katika Aya ya 32 na 33 ya hotuba yangu na Taarifa ya Utekelezaji wa Miradi ya Maendeleo kwa Kipindi cha Mwaka 2016/17 hadi 2019/20.

MPANGO WA MAENDELEO WA TAIFA WA MWAKA 2020/21

Shabaha na Malengo ya Uchumi Jumla kwa Mwaka 2020/21
33.      Mheshimiwa Spika, Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2020/21 umezingatia shabaha kuu za uchumi jumla zifuatazo:

(a)        Ukuaji wa Pato Halisi la Taifa unatarajiwa kupungua kutoka maoteo ya awali ya asilimia 6.9 na kufikia asilimia 5.5 mwaka 2020 ikilinganishwa na asilimia 7.0 mwaka 2019. Hii ni kutokana na athari za ugonjwa wa COVID-19 ulioenea katika nchi nyingi ambazo ni washirika wetu wakubwa wa kibiashara;
(b)        Kuendelea kudhibiti kasi ya mfumuko wa bei na kuhakikisha kuwa unabaki katika wigo wa tarakimu moja kati ya wastani wa asilimia 3 hadi 5 kwa mwaka 2020/21;
(c)         Mapato ya ndani kufikia asilimia 14.7 ya Pato la Taifa mwaka 2020/21 kutoka matarajio ya asilimia 14.0 mwaka 2019/20;
(d)        Matumizi ya Serikali yanatarajiwa kuwa asilimia 22.1 ya Pato la Taifa mwaka 2020/21;
(e)        Nakisi ya bajeti (ikijumuisha misaada) kuwa asilimia 2.6 mwaka 2020/21 ikiwa ni chini ya asilimia 3.0 kuendana na makubaliano ya nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki; na
(f)          Kuwa na akiba ya fedha za kigeni kwa kiwango kinachokidhi mahitaji ya uagizaji wa bidhaa na huduma kutoka nje kwa kipindi kisichopungua miezi 4.0.

Miradi ya Kipaumbele 2020/21

34.      Mheshimiwa Spika, mwaka huu nchi yetu imepata mvua nyingi zilizosababisha uharibifu mkubwa wa miundombinu. Katika mwaka 2020/21, Serikali itaweka kipaumbele katika ukarabati wa miundombinu ya kiuchumi na kijamii iliyoharibiwa na mvua ikijumuisha barababara na madaraja, reli, nguzo za umeme, mabwawa ya maji na majengo ya taasisi za afya na elimu;

35.      Mheshimiwa Spika, miradi na shughuli za kipaumbele kwa mwaka 2020/21 ni kama ifuatavyo:

(a)        Viwanda vya Kukuza Uchumi na Ujenzi wa Msingi wa Uchumi wa Viwanda: Katika eneo hili mkazo utawekwa kwenye ujenzi wa viwanda vinavyotumia malighafi zinazopatikana kwa wingi nchini. Miradi mahsusi katika eneo hili ni pamoja na:

(i)          Uendelezaji wa Viwanda ikijumuisha kuendeleza vituo vya utafiti wa teknolojia na bidhaa za viwandani vya CAMARTEC, TIRDO, TEMDO na SIDO; kuboresha Shirika la Nyumbu; na uendelezaji wa maeneo maalumu ya uwekezaji ya Bunda, Manyoni, Tanga, Mtwara, Dodoma, Bagamoyo na Benjamin William Mkapa;

(ii)         Kilimo: kuboresha utafiti na miundombinu ya utafiti katika kilimo; kuongeza tija katika uzalishaji kwa kuwezesha upatikanaji wa mbegu bora na pembejeo, huduma za ugani, maghala na masoko kwa mazao ya kimkakati ya michikichi, kahawa, pamba, chai, tumbaku na miwa; kujenga na kukarabati miundombinu ya skimu za umwagiliaji; na kuboresha huduma za ushauri kuhusu utafiti, mafunzo na usambazaji wa taarifa za kilimo;

(iii)        Mifugo: kuimarisha tiba na udhibiti wa magonjwa ya mifugo; ujenzi wa majosho; kuboresha miundombinu ya uhifadhi wa chanjo; kuimarisha vituo vya uhimilishaji Kitaifa na Kikanda; na kuboresha mazingira ya biashara ya mifugo;

(iv)       Uvuvi: kujenga na kukarabati miundombinu ya ufugaji wa viumbe maji; kuboresha Shirika la Uvuvi Tanzania (TAFICO); kujenga na kukarabati miundombinu ya mialo na masoko ya uvuvi; na ujenzi wa bandari ya uvuvi; na

(v)        Madini: kujenga ofisi nane (8) za maafisa madini na kituo cha umahiri; kujenga ghala la kuhifadhi sampuli za miamba choronge (core shed); kununua vitendea kazi kwa ajili ya shughuli za utafiti wa ikolojia; na kununua vifaa vya maabara na utafiti;

(b)        Kufungamanisha Ukuaji wa Uchumi na Maendeleo ya Watu: Miradi ya kipaumbele itakayotekelezwa katika mwaka 2020/21 itajielekeza katika maeneo yafuatayo:
(i)          Elimu: kuendelea kusomesha kwa wingi wataalamu kwenye fani na ujuzi adimu kama vile udaktari, mafuta na gesi, Jiolojia, Jemolojia na Uhandisi migodi; kuendelea kugharamia utoaji wa elimumsingi bila ada; ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya kujifunzia na kufundishia katika shule na vyuo vya ualimu na vya Elimu ya Juu; ujenzi wa nyumba 122 za walimu katika shule 10 za msingi na shule 20 za sekondari  katika maeneo yasiyofikika kwa urahisi; na kuendelea kutoa mikopo kwa wanafunzi wa Elimu ya Juu;

(ii)         Afya: kuendelea na ujenzi wa hospitali 71 za wilaya; kuboresha miundombinu ya kutolea huduma za afya katika Hospitali za Rufaa za mikoa, kanda na Taifa; kuimarisha usambazaji wa dawa, chanjo, vifaa, vifaa tiba na vitendanishi katika vituo vya kutolea huduma za afya; kuimarisha huduma katika Taasisi ya Saratani Ocean Road, Taasisi ya Tiba ya Moyo ya Jakaya Kikwete na Taasisi ya Mifupa Muhimbili (MOI); kujenga na kukarabati vyuo vya Maendeleo ya Jamii; kuboresha uhai na Maendeleo ya Awali ya Mtoto; na kuboresha huduma za Ustawi wa Jamii;

(iii)        Maji: kuendelea na ukamilishaji na upanuzi wa miradi ya maji katika miji mikuu ya Mikoa na Wilaya ikijumuisha Mikoa mipya ya Geita, Simiyu, Njombe, Katavi na Songwe; kuendelea na ujenzi wa miradi ya maji ya Masasi – Nachingwea, Same – Mwanga – Korogwe, ziwa Victoria – Igunga, Nzega na Tabora, ziwa Victoria – Kahama – Shinyanga; na kusimamia na kuendeleza rasilimali za maji nchini.

(c)         Uboreshaji wa Mazingira Wezeshi kwa Uendeshaji Biashara na Uwekezaji: Miradi itakayotekelezwa katika eneo hili italenga kuendeleza ujenzi na ukarabati wa miundombinu wezeshi ili kurahisisha uendeshaji biashara na uwekezaji nchini. Miradi hiyo ni pamoja na: kuendelea na ujenzi wa Reli ya Kati ya standard gauge; mradi wa kuzalisha Umeme wa Julius Nyerere Rufiji – MW 2,115; na kuboresha Shirika la Ndege Tanzania. Miradi mingine inajumuisha:

(i)          Barabara na Madaraja: kuendelea na ujenzi wa barabara ya Tabora - Ipole - Koga - Mpanda (km 370); Barabara ya Mbeya - Makongolosi - Rungwa – Itigi - Mkiwa (km 577.9); Kigoma - Kidahwe - Uvinza – Kaliua - Tabora (km 389.7); Kabingo – Kasulu – Manyovu (km 260); Mtwara – Mingoyo – Masasi – Songea – Mbamba Bay (km 1,470.9); Bagamoyo – Makurunge – Saadani - Tanga (km 246); Sumbawanga - Mpanda – Nyakanazi (km 517.4); Usagara – Geita – Buzirayombo – Kyamyorwa (km 388); ujenzi  wa barabara za mzunguko Dodoma (km 112.3); na upanuzi wa Barabara ya njia nane (8) Kimara – Kibaha (km 25.7); kuendelea na ujenzi wa madaraja ya Kigongo – Busisi (Mwanza), daraja jipya la Selander, Mangara (Manyara), New Wami (Pwani) na Kitengule (Kagera);

(ii)         Reli: kuendelea na ujenzi wa Reli ya Kati katika kiwango cha kimataifa cha standard gauge, kuendelea na ukarabati wa vichwa vya treni, mabehewa ya mizigo na abiria pamoja na njia za reli ya kati na TAZARA;

(iii)        Nishati: kuendelea na ujenzi wa bwawa la kuzalisha Umeme katika mradi wa umeme wa Julius Nyerere Rufiji – MW 2,115,  kuendelea na ujenzi wa Mradi wa Kusafirisha Umeme wa Msongo wa kV 400 - North – West Phase I, Mradi wa Njia ya Kusafirisha Umeme wa Msongo wa kV 400 kutoka Singida - Arusha – Namanga, Mradi wa Kusafirisha Umeme wa Msongo wa kV 400 Rufiji – Chalinze – Kinyerezi, Mradi wa Njia ya Kusafirisha Umeme wa Msongo wa kV 400 kutoka Chalinze - Dodoma, Mradi wa Njia ya Kusafirisha Umeme wa Msongo wa kV 220 Rusumo – Nyakanazi na kuendelea na usambazaji wa umeme vijijini kupitia mradi wa REA; na

(iv)       Bandari: kuendelea na uboreshaji wa miundombinu ya bandari za Dar es Salaam, Tanga na Mtwara pamoja na bandari za maziwa makuu; na

(v)        Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) na Viwanja vya Ndege: kuendelea kuboresha Shirika la Ndege Tanzania, uendelezaji wa viwanja vya ndege ikiwa ni pamoja na ujenzi wa Kiwanja kipya cha Ndege cha Kimataifa cha Msalato – Dodoma.

(d)        Kuimarisha Usimamizi wa Utekelezaji wa Mpango: Miradi itakayotekelezwa inalenga kuimarisha mifumo na taasisi za utekelezaji na usimamizi wa Mpango, kuongeza upatikanaji wa rasilimali fedha za kutekeleza mpango na kuweka vigezo vya upimaji  wa matokeo ya utekelezaji. Miradi hii itajumuisha maeneo ya Utawala Bora hususan utoaji haki na huduma za kisheria, kuimarisha miundombinu ya Mahakama na Bunge na kuimarisha vyombo vya ulinzi na usalama.

36.      Mheshimiwa Spika, Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2020/21 utaendelea kuzingatia umuhimu wa kuimarisha Muungano wetu. Miradi itakayotekelezwa kwa pamoja Tanzania bara na Zanzibar ni pamoja na:
(i)          Mradi wa Kikanda wa Usimamizi Shirikishi wa Rasilimali za Uvuvi Kusini Magharibi mwa Bahari ya Hindi (SWIOFish) kwa lengo la kuimarisha uvuvi wa bahari kuu;
(ii)         programu ya mabadiliko ya tabianchi kwa lengo la kulinda mazingira ya fukwe katika ukanda wa bahari kuu;
(iii)        Mpango wa Kunusuru Kaya Masikini katika Awamu ya Tatu ya Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF III) ambapo shughuli zilizopangwa ni kuendelea kuongeza maeneo ya utekelezaji kutoka 161 ya sasa hadi maeneo 187 katika Halmashauri zote Tanzania Bara na Wilaya zote Zanzibar ambapo shughuli za miradi 2,505 ya kutoa ajira za muda na kuendeleza miundombinu zitatekelezwa Tanzania Bara na miradi 204 zitatekelezwa Zanzibar; na
(iv)       Mradi wa Kupitia Mifumo ya Ikolojia kwa lengo la kuongeza uvumilivu wa kuhimili mabadiliko ya tabianchi katika jamii za vijijini kwa kuimarisha mifumo ikolojia katika Wilaya za Mvomero (Morogoro), Simanjiro (Manyara), Kishapu (Shinyanga), Mpwapwa (Dodoma) na Kaskazini A, (Kaskazini Unguja).  Shehia zitakazonufaika na mradi kutoka Kaskazini A ni pamoja na Shehia ya Matemwe Kijini, Matemwe Jugakuu na Matemwe Mbuyutende.

37.      Mheshimiwa Spika, maelezo ya kina kuhusu vipaumbele vya Mpango kwa Mwaka 2020/21 yapo katika Aya ya 35 na 36 ya hotuba yangu na Sura ya Nne ya Kitabu cha Mpango.

Ugharamiaji wa Mpango 2020/21

38.      Mheshimiwa Spika, Serikali imetenga shilingi trilioni 12.90, kwa ajili ya kugharamia utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2020/21, sawa na asilimia 37 ya bajeti yote ya mwaka 2020/21. Kati ya kiasi hicho, shilingi trilioni 10.16 ni fedha za ndani na shilingi trilioni 2.74 ni fedha za nje. Kiwango kilichotengwa kinaendana na lengo la Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano la kutenga kati ya asilimia 30 na 40 ya bajeti yote kwa ajili ya miradi ya maendeleo.

39.      Mheshimiwa Spika, maelezo ya kina kuhusu ugharamiaji wa Mpango kwa Mwaka 2020/21 yapo katika Aya ya 40 na 41 ya hotuba yangu na Sura ya Tano ya Kitabu cha Mpango.


Ufuatiliaji, Tathmini na Utoaji wa Taarifa za Utekelezaji

40.      Mheshimiwa Spika, moja ya nyenzo muhimu ya kufikia malengo ya mipango ni kuwa na mfumo madhubuti wa kufuatilia utekelezaji na matumizi ya fedha zilizopangwa. Kwa kutambua hilo, Serikali imejipanga kufanya ufuatiliaji wa karibu wa matumizi sahihi ya fedha za miradi na kukagua maendeleo ya shughuli zote za utekelezaji wa miradi kwa lengo la kujiridhisha iwapo utekelezaji unaendana na matarajio na kuhakikisha matokeo yaliyokusudiwa yanafikiwa kwa manufaa ya Taifa. Katika kuboresha utekelezaji wa miradi ya maendeleo, Serikali itaandaa Mwongozo wa Kisera wa kusimamia shughuli za ufuatiliaji na tathmini ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

41.      Mheshimiwa Spika, katika kufanikisha Ufuatiliaji na Tathmini ya Mpango, Serikali inazielekeza Wizara, Idara Zinazojitegemea, Taasisi na Wakala za Serikali kuimarisha mifumo ya ndani ya ufuatiliaji na tathmini ya miradi ya maendeleo; kutafsiri malengo na viashiria vya utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2016/17 - 2020/21 katika Mipango na Bajeti za kisekta kwa mwaka 2020/21; kufanya ufuatiliaji na tathmini ya miradi ya maendeleo kila robo mwaka; kuwajengea uwezo watumishi katika tasnia ya ufuatiliaji na tathmini; na kuandaa taarifa za ufuatiliaji na tathmini ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo pamoja na programu, na kuziwasilisha Wizara ya Fedha na Mipango. Aidha, Ofisi ya Rais – TAMISEMI itaratibu ufuatiliaji na tathmini ya miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika ngazi za Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa na kuwasilisha taarifa za utekelezaji Wizara ya Fedha na Mipango.

MAJUMUISHO

42.      Mheshimiwa Spika, utekelezaji wa Mpango huu utakuwa ni wa mwisho katika utekelezaji wa Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano wenye dhima ya kujenga uchumi wa viwanda ili kuchochea mageuzi ya kiuchumi na maendeleo ya watu. Mafanikio yanayotarajiwa kutokana na utekelezaji wa Mpango ni  pamoja na: kuongeza  kasi ya ukuaji wa uchumi na utengamavu wa viashiria vya uchumi jumla; kuimarisha utoaji wa huduma za jamii zikijumuisha maji, elimu, afya na umeme vijijini; kuimarika kwa mazingira ya biashara na uwekezaji; na kuongezeka kwa ajira na kipato cha wananchi na hatimaye kupungua kwa kiwango cha umaskini nchini.

HITIMISHO

43.      Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Serikali napenda kuwashukuru wadau mbalimbali wakiwemo Waheshimiwa Wabunge, Sekta Binafsi, Washirika wa Maendeleo na Wananchi kwa ujumla kwa michango yao katika utekelezaji wa Mpango na kujenga uchumi. Michango hiyo imewezesha kupatikana kwa mafanikio mkubwa katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

44.      Mheshimiwa Spika, naomba nitoe shukrani zangu za dhati kwa Mawaziri, Naibu Mawaziri na Makatibu Wakuu wa Wizara zote, Wakuu wa Idara Zinazojitegemea na Wakala, Taasisi na Mashirika ya Umma kwa ushirikiano wao katika  kutayarisha taarifa ya Hali ya Uchumi wa Taifa kwa mwaka 2019 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2020/21. Kipekee ninamshukuru Mheshimiwa Dkt. Ashatu  K. Kijaji (Mb), Naibu Waziri wa Fedha na Mipango kwa kunisaidia kuboresha hotuba hii. Aidha, ninawashukuru watendaji  wote wa Wizara ya Fedha na Mipango wakiongozwa na Katibu Mkuu Bw. Doto M. James kwa kusimamia kikamilifu maandalizi ya hotuba hii.

45.      Mheshimiwa Spika, kipekee niwashukuru Waheshimiwa Wabunge na Wananchi wote kwa kunisikiliza. Aidha, hotuba hii  na vitabu vya Taarifa ya Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2019 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2020/21 vinapatikana katika tovuti ya Wizara ya Fedha na Mipango ambayo ni www.mof.go.tz.

46.      Mheshimiwa Spika, baada ya maelezo hayo naomba sasa Bunge lako Tukufu lipokee na kujadili Taarifa ya Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2019 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2020/21.

47.      Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post