RAIS MAGUFULI KUHUTUBIA NA KUVUNJA BUNGE KESHO

Na Jonas Kamaleki-MAELEZO

Spika wa Bunge, Mhe. Job Ndugai amesema kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli anatarajia kulihutubia na kulivunja Bunge la 11 jijini Dodoma kesho Juni 16, 2020.

Bunge hilo lilifunguliwa na Rais Magufuli Novemba 20, 2015 baada ya kuapishwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Akifungua Bunge hilo, Rais Magufuli aliainisha viapaumbele kadhaa vya Serikali yake ikiwemo kupambana na rushwa, kukusanya kodi, kupunguza urasimu katika kutoa huduma Serikalini, kuboresha huduma za afya, elimu, miundombinu ya barabara, madaraja na reli na kufufua Shirika la Ndege (ATCL).

Vile vile, Rais Magufuli alisema kuwa atashughulikia migogoro ya ardhi ikiwemo ya wakulima na wafugaji, kupambana na dawa za kulevya, kuinua sekta za madini, mifugo, kilimo na uvuvi, kuwezesha ujenzi wa viwanda na kupambana na ujangili.

Mhe. Rais kesho atakuwa na uwanja mpana wa kuzungumzia mafanikio yaliyofikiwa na Serikali ya Awamu ya Tano kwani mengi yaliyoahidiwa yametekelezwa ambapo azma ya Serikali ya kufikia uchumi wa kati unaotegemea viwanda ifikapo 2025 itafanikiwa.

Serikali ya Awamu ya Tano imefufua ATCL kwa kununua ndege 11 ambapo ndege nane zimeshaanza kazi ndani na nje ya nchi, elimu imeboreshwa kwa kujenga na kukarabati shule na vyuo mbalimbali, kujenga zaidi ya vituo 360 vya afya, ujenzi wa hospitali 70 za wilaya, kuongeza bajeti ya dawa kutoka shilingi bilioni 31 hadi bilioni 270 na kuongeza ukusanyaji wa mapato kwa njia ya kodi toka shilingi bilioni 800 kwa mwezi hadi wastani wa shilingi trilioni 1.5 kwa mwezi na kuongezeka kwa upatikanaji wa maji safi na salama mijini na vijijini.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527