MUFTI MKUU ATANGAZA KUFUNGULIWA MADRASA ZILIZOKUWA ZIMEFUNGWA KISA CORONA


Mufti wa Tanzania Sheikh Abubakar Zuberi, ametangaza kufunguliwa rasmi kuanzia jana kwa madrasa, zilizofungwa kutokana na mlipuko wa virusi vya corona (Covid 19).

Sheikh Zuberi, alitoa kauli hiyo jana jijini Dodoma wakati alipokuwa akizungumza na waumini wa dini ya Kiislamu katika msikiti wa Gadafi mara baada ya swala ya Ijumaa.

Alisema kuwa madrasa zote zilizofungwa zifunguliwe na kuanza kutoa huduma kama ilivyo kuwa awali, lakini kwa kuzingatia maelekezo ya wataalam wa afya.

“Lakini katika hili madrasa zitakazorudi na kuanza kutoa huduma ni zile pekee zenye wanafunzi ambao umri wao kidogo ni mkubwa na wanaojitambua, wale wadogo kabisa zitaendelea kufungwa mpaka hapo tena tutakapo toa tamko jingine,” alisema Mufti Zuberi.

Kadhalika, alisema kuwa madrasa zitakazofunguliwa kuanza kazi zinatakiwa kuchukua tahadhari zote ambazo zinaelekezwa na Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto.

“Lazima katika madrasa hizi kuzingatia maagizo ya wataalam kama vile kuvaa barakoa, kunawa mikono kwa maji yanayotiririka na sabuni na hili sisi kama Waislamu hatutashindwa kwa kuwa Muislamu na kunawa ni jambo la kila siku,” alisema.

Alipongeza Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa kufanikisha kupitisha bajeti kuu ya serikali kwa mwaka wa fedha 2020/21.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527