MOTISHA YA MBUNGE ILIVYOCHOCHEA UFAULU SEKONDARI ZA MADABA



Mbunge jimbo la Madaba Mhe. Joseph Mhagama  akikagua ujenzi wa darasa Ifinga
Mwanafunzi shule ya secondary Wino Gaston Ndimbo akielekeza namna ya kuchanganya kemikali mbele ya Mbunge wa jimbo la Madaba Joseph Mhagama (wa kwanza kushoto)wakati alipotembelea shuleni hapo
Mwananchi akimshukuru mgeni rasmi Mbunge wa jimbo la Madaba Joseph Kizito Mhagama wakati wa mahafali ya shule ya sekondari Magingo.

****
Motisha inayotolewa kwa Walimu na wanafunzi  imekuwa chachu ya maendeleo ya elimu katika Jimbo la Madaba hapa mkoani Ruvuma; na hali hii imeongeza ufaulu  na kutuinua kimkoa na kitaifa.

Anasema Ofisa Elimu (Sekondari) wa Halmashauri ya Madaba, Michael Hadu, anapozungumzia kiwango cha ufaulu katika shule za halmashauri hiyo iliyo katika Jimbo la Madaba mkoani Ruvuma.

“Tangu Mbunge wa Jimbo hili (Joseph Mhagama) aanze kutoa motisha kwa walimu na wanafunzi wa shule za sekondari ili kuhamasisha na kuchochea ari ya walimu kufundisha na wanafunzi kujifunza sambamba na kusaidia wananchi kujenga mabweni na vyumba vya madarasa, kiwango cha ufaulu kwa wanafunzi  wa shule za sekondari na msingi katika jimbo hili kimepaa,” anasema Ofisa Elimu huyo.

Hadu anaongeza: “Ndiyo maana maana unaona tangu mbunge alipoanza kuweka msukumo huu kwa manufaa ya watoto wa halmashauri na jimbo hili, sambamba na kuhakikisha kunakuwapo ongezeko la viti, meza, vitabu na vifaa vingine vya kufundishia na kujifunzia, shule wanafunzi wameongeza ufaulu sana.”

Anatoa mfano akisema ufaulu wa wanafunzi katika Mtihani wa Taifa wa Kidato cha Pili umepanda kutoka nafasi ya 104 mwaka 2018 hadi nafasi ya 24 mwaka 2019 na kushika nafasi ya kwanza kimkoa.

Katika kuelezea matunda ya kujitoa na kuwajibika kwa mbunge huyo wa Madaba kwa wnaanchi wake, Ofisa Elimu huyo anasema hata katika mtihani wa taifa wa kidato cha nne, halmashauri ya madaba imefanya vizuri na kushika nafasi ya 23 kitaifa mwaka 2019  huku ikiwa ya kwanza kimkoa.

“Haya ni mafanikio ya kutoka nafasi ya 121 kitaifa mwaka 2018  na hii yote imechangiwa na juhudi za Mbunge (Mhagama) kupita na kuzungumza na walimu, kusikiliza kero zao na kuwatia moyo huku akiwasisiza kuwafundisha watoto kwa upendo na kufanya kazi kwa bidii...” anasema na kuongeza: “Kweli walimu walimwelewa vizuri; wakabadilika na sasa wanafundisha kwa bidii ndiyo maana ufaulu unazidi kupanda siku hadi siku.”

“Siyo siri, Ofisi ya Mbunge imekuwa  na mchango mkubwa kwa Idara ya Elimu katika jimbo na halmashauri hii.”

“Mheshimiwa Joseph Mhagama amesaidia sana hata kufuatilia na kutuletea Sh milioni 240 kwa ajili ya ujenzi wa maabara na amekuwa karibu sana na walimu na ofisi yake imekuwa ikitoa sukari ya mwaka mzima kwa ajili ya walimu,” anafahamisha.

Kwa mujibu wa uchunguzi wa makala haya, tangu mwaka 2017, mbunge huyo wa Jimbo la Madaba amekuwa akitoa Sh 500,000 kwa kila shule kwa ajili ya chai kuwasaidia walimu kupata chai shuleni na hivyo, kuokoa muda.

“Hata kile kitendo chake cha kusikiliza shida binafsi za walimu na kuwasaidia hata kwa kutoa fedha zake binafsi mwalimu anapokuwa na shida, kimewatia moyo sana walimu ndiyo maana wanasema ni mlezi mzuri kwa walimu na wanafunzi,” anasema Ofisa Elimu huyo

“Mbunge huyu ni msaada mkubwa maana amesaidia sana kuinua elimu hata ‘form six’ (kidato cha Sita) mwaka 2019 katika Shule ya sekondari ya Madaba, wanafunzi 23 wamepata  daraja la kwanza, hivyo tumeshika nafasi ya 7 kati ya shule 26 za Mkoa wa Ruvuma”

“Nayo Sekondari ya Wilma imeshika nafasi ya 8, hivyo tumeingiza shule zetu mbili za ‘A Level’ katika kumi bora kitu ambacho hakijawahi kutokea na hii ni kutokana na ufatiliaji mzuri wa wataalamu kwa kushirikiana na Mbunge wa Madaba ambaye alizungumza na walimu na kuwazawadia Sh 200,000,” anasema.

Mmoja wa wanawake ambaye ni ofisa katika Halmashauri ya Madaba aliyekataa jina na idara yake kutajwa gazetini, anasema anaijua miradi mingi ya elimu iliyowezeshwa na Mbunge huyo ukiwamo ujenzi wa hosteli na vyoo vya  wanafunzi wa kike katika shule mbalimbali.

Anazitaja baadhi ya shule hizo kuwa ni pamoja na sekondari za Nguluma na Lipupuma alipokarabati jengo la utawala na na kukarabati choo cha wasichana katika Shule ya Sekondari ya Magingo na kuweka umeme katika madarasa ikisemekana pia kuwa, ametumia Sh 7,000,000 kuezeka madarasa katika shule ya Mateteleka.

Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Mahanje, Makoye Richard, anasema motisha kwa walimu zimeongeza ari ya ufundishaji kwa walimu na kuongeza ufaulu  shuleni kwake.

Makoye anasema: “Ufaulu wa   daraja la kwanza na la pili ulikuwa ndoto kwa shule yetu, lakini tunashukuru maana kwa mara ya kwanza, wanafunzi 48 waliofanya mtihani wa taifa wa kidato cha nne  mmoja alipata  daraja la kwanza na wanafunzi sita wakapata ‘division two’ wanafunzi 14 walipata ‘division three’ na  wanafunzi 26 wakapata ‘division four.” 4.

Anaupongeza ushirikiano uliopo baina ya wazazi, walimu na mbunge wao akisema umewafanya vijana kuongeza bidii na umakini kiasi kwamba, sasa karibu nusu ya darasa wanafaulu na kujiunga na kidato cha tano. Hata wengine wanaobaki, nao wanaenda katika vyuo.

Kwa mujibu wa Mkuu wa Shule huyo, ufaulu huo umechangiwa kwa kiasi kikubwa na juhudi za Mbunge Mhagama kutembelea shule mbalimbali na kuzungumza na walimu na wanafunzi. Anasema: “Hapa kwetu kwa mwaka anaweza kuja mara mbili hadi tatu.”

Makoye anafahamisha kuwa, Mbunge huyo amekuwa akitoa motisha kwa walimu wanaofanya vizuri na wanafunzi hata Sh 300,000 kwa kila mmoja sambamba na vifaa vya kujifunzia na kufundishia.

“Hapa shuleni, amewasupport wanafunzi wa kike kwa kuhakikisha wanapata pedi, hivyo wawanafunzi hao kuongeza mahudhurio katika vipindi vyote vya masomo hata wakati wakiwa kwenye hedhi. Hali hii inawafanya waongeze umakini na ufaulu katika masomo...” anasema

Daud Mgaya Mwanafunzi wa kidato cha nne Mahanje sekondari anasema, mbunge amefanya kazi kubwa kuwajenga kisaikolojia na kuwatia matumaini pale wanapopitia wakati mgumu wakiwa shule kwa kuwapa motisha hivyo kuwafanya wasome kwa bidii zaidi hali iliyoongeza ufauhulu.

“Tunamshukuru sana Mbunge kwa kujitoa kwake kwetu na kwa walimu kwani mara kwa mara amekuwa bega kwa bega na sisi na ametusupport sana kwenye miradi midogo midogo ya hapa shuleni zikiwemo club za wanafunzi,” anasema Mgaya

Mzazi na mkazi wa Kijiji cha Mateteleka anasema, Allan Mwenda, anasema amekuwa akivutiwa na jitihada zinazofanywa na Mbunge Mhagama katika suala la elimu ya watoto wao.

“Amejitoa kwa hali na mali kuwasaidia watoto wa wanyonge. Binafsi huwa najivunia sana mtu anayependa elimu na huyu Mbunge ni miongoni mwa viongozi wanaopenda sana elimu ndiyo maana ameweza kutambua mchango wa walimu na kuwasaidia kwa kuwapa zawadi na kuwachangia sukari kwa mwaka mzima; ni viongozi wachache sana wenye upendo kama huo. Tunamwombea kwa Mungu aendelee kutusaidia wananchi wa Madaba,” anasema Mwenda.

Alipoulizwa anavyochangia kuinua kiwango cha elimu jimboni Madaba, mbunge huyo anasema amekuwa na utaratibu wa kutoa motisha na hamasa kwa walimu na wanafunzi wa sekondari kwa kuwatembelea kila mwaka, kuzungumza nao, kushiriki nao chakula, na kuwapa zawadi.

“Katika kipindi hicho, nimetumiatakriban Sh 11,700,000 kama zawadi kwa wanafunzi wanaofanya vizuri na chai ya walimu wetu wa Sekondari katika shule zetu zote”

Anasema:“Kwa mfano, kutokana na kufanya vizuri, wanafunzi Sekondari ya Wino walipewa zawadi ya TV ya Sh 1,000,000 wanayotumia kupata habari na burudani mbalimbali.”

Mintarafu motisha kwa walimu, wanafunzi na wafanyakazi katika Shule ya Sekondari ya Wilma anasema zilitumika Sh 1,200,000. 

“Jitihada hizi zimechangia sana kuongezeka kwa ufaulu kwa watoto wetu ambapo katika matokeo ya Kidato cha Nne 2019 Madaba imeshika nafasi ya kwanza  kimkoa na nafasi ya 24 kitaifa; asante sana walimu, wanafunzi na wazazi!  Jumla Sh. 13,550,000 zimetumika kulipa motisha”.anasema Mhagama.

Kuhusu maendeleo ya elimu kwa shule za msingi anasema: “Kama mbunge wao, pia nimekuwa na utaratibu kama huo wa kuhamasisha na kutoa motisha kwa walimu na wanafunzi wa shule zetu za msingi kwa kuwatembelea kila mwaka, kuzungumza nao, na kuwapa zawadi.”

“ Katika kipindi hiki, takriban Sh 3,700,000 zimetumika kama zawadi kwa walimu, na ununuzi wa chaki kwa shule zote. Mpaka sasa bado chaki zinasambazwa.  Jitihada hizi zinachangia sana kuongezeka kwa ufaulu,“ anasema Mhagama. 

Anasema ukamilishaji wa maabara moja katika Shule ya Sekondari ya  Wino umegharimu  Sh 4,505,500  na kazi inaendelea  na kadhgalika, ukarabati wa vyoo katika Shule ya Sekondari Ifinga ulifanyika na kukamilika kwa Sh. 1,000,000 kutoka Mfuko wa Jimbo 2019/20.

Anasema mbali na ujenzi wa madarasa mawili na ofisi ya walimu katika Sekondari ya Wino zilipotumika takriban Sh 30,000,000, pia kumekuwa na usambazaji wa madawati katika shule za msingi na sekondari kupitia mfuko maalum wa Bunge.

“Serikali imetuletea madawati 251 yaliyosambazwa katika shule zetu wa msingi na chache za sekondari... Gharama za kusafirishia madawati hayo takriban Sh 534,000 zilitolewa na mbunge,” anasema Mhagama.

Uchunguzi umebaini kuwa Mhagama pia amesaidia kupatikana kwa fedha za miradi mbalimbali ikiwemo ya ujenzi wa madarasa, nyumba za walimu, ofisi na vyoo. Katika Shule ya Msingi Matetereka, wamefanikiwa kukamilisha ujenzi wa madarasa mawili yaliyogharimu  Sh 25,500,000.

Imebainika pia kuwa, katika kutatua changamoto ya ukosefu wa mabweni katika Shule ya Sekondari Mahanje iliyowaathiri zaidi kimasomo wanafunzi wa kike,  alitafuta na kupata Sh 196,600,000 (P4R 2017/18 awamu ya kwanza).mradi wa kulipa kulingana na matokeo.

“Kwa kushirikiana na wananchi, tumejenga mabweni makubwa mawili moja la wanafunzi wa kike na moja la wavulana,” kinasema chanzo kimoja jimboni humo na kufafanua kuwa, kila bweni lina vyumba 20 vyenye vitanda 4 kila chumba.

 Mikakati yake ni kuendelea kutoa motisha zaidi kwa walimu na wanafunzi na kusaidia vifaa vya kufundishia na kujifunzia ili kupunguza kero zinazowatatiza walimu

Anawashauri wadau wa Elimu halmashauri ya Madaba kuendelea kusaidia elimu ilikuweza kupandisha ufaulu katika Halmashauri hiyo.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527