HOTUBA YA WAZIRI MKUU KASSIM MAJALIWA WA KUHITIMISHA SHUGHULI ZA MKUTANO WA 19 WA BUNGE JIJINI DODOMA

HOTUBA YA MHESHIMIWA KASSIM M. MAJALIWA (MB), WAZIRI MKUU WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA WAKATI WA KUHITIMISHA SHUGHULI ZA MKUTANO WA KUMI NA TISA WA BUNGE


1.           MheshimiwaSpika, naomba nitumie fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema kwa kutujaalia afya njema na kutuwezesha kufika siku hii ya leo ambayo naiita kuwa ni siku ya kihistoria kwetu.

2.           Nasema kuwa ni ya kihistoria kwa sababu Bunge lako Tukufu linahitimisha shughuli za Bunge la Kumi na Moja (11) la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pia tunahitimisha Mkutano wa Kumi na Tisa (19) wa Bunge ulioanza mwezi wa Aprili mwaka huu wa 2020.

3.           Mheshimiwa Spika,katika Mkutano huu wa Bunge, licha ya uwepo wa ugonjwa wa homa ya mapafu inayosababishwa na virusi vya Corona (COVID-19), tumeweza kukaa hapa Dodoma kwa kipindi kisichopungua miezi miwili na nusu. Aidha, katika kipindi hicho tumeweza kutekeleza majukumu yetu yote kama ilivyokuwa imepangwa.

4.           Ama kwa hakika hatuna budi kumshukuru Mwenyezi Mungu kwani tunakamilisha maisha yetu ya Kibunge kwa kipindi cha miaka mitano toka Novemba 2015. Tumeshirikiana katika maeneo mengi nje na ndani ya Bunge kwa kila mmoja kutekeleza majukumu yake.

5.           Mheshimiwa Spika, siwezi kuanza kueleza yaliyojiri kwenye majukumu yetu bila kumshukuru Mwenyezi Mungu aliyeniwezesha kuwa na afya njema na kunisimamia katika kila jambo na hasa nilipokuwa natekeleza majukumu yangu binafsi na ya umma kwa kipindi chote hadi sasa. InshaAllah, yeye ndiye msimamizi wa yote.

6.           Mheshimiwa Spika, kwa moyo mkunjufu kabisa naomba nitumie nafasi hii kumshukuru sana Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kitendo chake cha kuniamini na kuniteua kushika wadhifa wenye dhamana kubwa ya kumsaidia kazi ya utendaji ndani ya Serikali kwa kipindi chote cha miaka mitano.

7.           Kwa niaba ya Familia yangu na Wana-Ruangwa wote, namshukuru sana kwa ukarimu, imani na upendo aliouonesha kwetu, Mwenyezi Mungu aendelee kumpa nguvu, ulinzi, kheri na kila lililo jema na aendelee kuliongoza Taifa hili vyema na kwa mafanikio makubwa kama ambavyo Watanzania tumeendelea kushuhudia mafanikio makubwa katika kipindi hiki cha Uongozi wake wa Awamu ya Tano.

8.           Mheshimiwa Spika, Rais wetu ametenda mema kwa Watanzania na watamlipa mema. Ninamwombea kheri pia kwa Uchaguzi Mkuu ujao ashinde kwa ushindi wa kishindo. Amina.

9.           Mheshimiwa Spika, ninamshukuru sana pia Mheshimiwa Mama Samia Suluhu Hassan, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa ushirikiano wake mkubwa wakati wote nikitekeleza majukumu ya Waziri Mkuu. Vilevile, ninashukuru sana kwa ushirikiano mkubwa nilioupata kutoka kwa Mheshimiwa Dkt. Ali Mohamed Shein, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi na Mheshimiwa Balozi Seif Ali Iddi, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar pamoja na viongozi, watendaji na wananchi wote wa Zanzibar.

10.        Mheshimiwa Spika, nitumie nafasi hii pia kukushukuru sana wewe binafsi kwa upendo uliouonesha kwangu kipindi chote cha uhai wa Bunge la Kumi na Moja (11). Kwa uzoefu ulionao katika kuendesha Bunge, umekuwa msaada sana kwangu kwa kunipa ushauri na ushirikiano wa dhati ulionifanya nijenge imani kubwa kwenye majukumu yangu ndani ya Bunge.

11.        Mheshimiwa Spika, nami niungane na wenzangu kukutakia kheri nyingi kwenye Uchaguzi ujao, naamini Wana-Kongwa watasikiliza na kutekeleza dua zetu za kuwa upite bila kupingwa, na ukirudi hapa chukua fomu ya Uspika ili upate kura zote za ndiyo uendelee kuwa Spika wa Bunge la Kumi na Mbili (12).

12.        Mheshimiwa Spika, sitasahau tukio la tarehe 19 Novemba, 2015 siku ambayo Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alipowasilisha jina langu katika Bunge lako Tukufu na kupendekeza niwe Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

13.        Mheshimiwa Spika, nakushukuru tena wewe na Waheshimiwa Wabunge wenzangu kwa imani mlioionesha kwa kuridhia mapendekezo ya Mheshimiwa Rais na kunipigia kura nyingi za ndiyo na mkaridhia tufanye kazi kwa pamoja katika kuwatumikia Watanzania.

14.        Waheshimiwa Wabunge wenzangu, natambua, naheshimu na nathamini ushirikiano wa dhati mlionipa katika kipindi chote cha Bunge. Nami nawaombea na nawatakia ushindi wa kishindo kwenye Majimbo yenu ili mrudi tena hapa mwezi Novemba, 2020.

15.        Mheshimiwa Spika, pia, nawashukuru sana Mheshimiwa Dkt. Tulia Akson, Naibu Spika, Wenyeviti wa Bunge Mheshimiwa Mtemi Andrew Chenge, Mheshimiwa Najma Murtaza Giga na Mheshimiwa Mussa Zungu Azzan ambaye mwishoni alipata uteuzi wa Mheshimiwa Rais kuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Mazingira kwa kuliongoza Bunge hili kwa busara na umahiri mkubwa.

16.        Mheshimiwa Spika, vilevile, namshukuru Mheshimiwa Mashimba Mashauri Ndaki, Mbunge wa Maswa Magharibi na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti pamoja na Wajumbe wote wa Kamati hiyo kwa mchango wao mkubwa katika kufanikisha Bajeti ya Serikali. Pia, nawashukuru Katibu wa Bunge Ndugu Stephen Kagaigai na Watumishi wote wa Bunge kwa ushirikiano mkubwa waliotupatia katika Mkutano huu na Mikutano iliyoendeshwa kipindi chote cha miaka mitano.

17.        Mheshimiwa Spika, katika kutekeleza majukumu ya Ofisi ya Waziri Mkuu hapa Bungeni, napenda kutambua mchango wa Mheshimiwa Jenista Joakim Mhagama (Mb), Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayesimamia Sera, Uratibu, Bunge, Ajira, Kazi, Vijana na Watu wenye ulemavu. Namshukuru sana Mheshimiwa Waziri Mhagama kwa kunisaidia ipasavyo katika kutekeleza majukumu yangu sambamba na majukumu yake ya unadhimu na uratibu wa shughuli za Serikali Bungeni. Nakuombea sana kwa wananchi wa Peramiho, Maposeni, Mgazini, Mdunduwalo, wakupitishe upite bila kupingwa.

18.        Mheshimiwa Spika, vilevile, namshukuru Mheshimiwa Angela Kairuki (Mb), Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Uwekezaji kwa kufuatilia na kusimamia hatua mbalimbali za kuimarisha na kuboresha mazingira ya uwekezaji nchini. Mheshimiwa Waziri Kairuki amekuwa akitembelea maeneo mbalimbali na kukutana na Wawekezaji wadau wa sekta binafsi ili kusikiliza changamoto zao na kuzitafutia ufumbuzi. Juhudi zake hizo, zimekuwa na mchango mkubwa katika kuboresha mazingira ya biashara na kuimarisha mahusiano ya sekta binafsi na Serikali nchini. Nawe nakutakia kila la kheri huko uendako ili upate kura za kutosha.

19.        Mheshimiwa Spika, kwa upande wa masuala ya maendeleo na uwezeshaji wa vijana napenda kumshukuru Mheshimiwa Anthony Peter Mavunde, Mbunge wa Dodoma Mjini, Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu kwa msaada mkubwa katika kusimamia vizuri masuala ya vijana na ajira. Kadhalika, namshukuru Dada yangu Mheshimiwa Stella Ikupa Alex (Mb), Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kusimamia vema masuala na maslahi ya Watu Wenye Ulemavu.

20.        Nawashukuru sana Waheshimiwa Mawaziri wenzangu na Naibu Mawaziri; Professor Adelardus Kilangi, Mwanasheria Mkuu wa Serikali; Balozi Mhandisi John William Kijazi, Katibu Mkuu Kiongozi; Makatibu Wakuu na Naibu Makatibu Wakuu wakiongozwa na Bw. Tixon Tuyangine Nzunda, Andrew Wilson Massawe, na Bibi Dorothy Aidan Mwaluko kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu. Nawashukuru kwa ushirikiano wa dhati mlionipa katika kuratibu na kusimamia shughuli za Ofisi ya Waziri Mkuu. Bila kuwasahau Watendaji wote wa Ofisi ya Waziri Mkuu.

21.        Mheshimiwa Spika, nitumie fursa hii pia kuwashukuru Wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama akiwemo Jenerali Venance Mabeyo - Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama; Inspekta Jenerali wa Polisi - Simon Nyakoro Sirro; Brigedia Jenerali Suleiman Mzee -Kamishna Jenerali wa Magereza; Dkt. Anna Makakala - Kamishna Jenerali wa Uhamiaji; John William Hasunga - Kamishna Jenerali wa Zimamoto na Uokoaji; Kamishna Diwani Athumani - Mkurugenzi wa Usalama wa Taifa; Brigedia Jenerali John Mbung’o - Mkurugenzi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa; James Kaji - Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Madawa ya Kulevya.

Wakuu hao wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama wameonesha nidhamu na uzalendo mkubwa katika kuhakikisha Nchi yetu, raia wake na mali zao wanakuwa salama.

22.        Mheshimiwa Spika, nawashukuru pia Wakuu wa Taasisi, Wakurugenzi na Watendaji wote Serikalini kwa ushirikiano mzuri walioutoa na utendaji wa pamoja wenye mafanikio makubwa. Aidha, tuendelee kutakiana mema na tuchape kazi hadi hapo utumishi wetu utakapokoma.

23.        Mheshimiwa Spika, nimalizie salamu zangu za shukrani kwa Familia yangu ambayo inaniunga mkono, kunivumilia pale ambapo nawatumikia Watanzania na kunitia moyo siku hadi siku kwenye majukumu yangu. Bila kuwasahau Wana-Ruangwa ambao walinipigia kura bila kujali Vyama vyao na kuniwezesha kuingia Bungeni na hatimaye nikapata uteuzi wa Mheshimiwa Rais wetu Dkt. John Pombe Magufuli kwa ajili ya kuwatumikia Watanzania. Nataka niwahakikishie Wana-Ruangwa kuwa bado tuko pamoja katika harakati za kuleta maendeleo. Nawashukuru sana.

24.        Mheshimiwa Spika, nitakuwa mchoyo wa fadhila kama sitawashukuru wananchi na Watanzania wote kwa kuiunga mkono Serikali ya Awamu ya Tano na ushirikiano walioutoa kwa Serikali wakati wa utekelezaji wa shughuli mbalimbali za maendeleo ya Taifa kwa ujumla bila kujali tofauti zao za kiitikadi au dini. Sambamba na kuonesha uzalendo, mshikamano na kudumisha amani na utulivu uliowezesha Serikali kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi na weledi, kwa mujibu wa taarifa zinazotolewa na taasisi ya GLOBAL PEACE INDEX 2020 inayofuatilia masuala ya amani duniani. Tanzania ni nchi ya saba kwa amani na utulivu Afrika na   ni nchi ya kwanza kwa amani Afrika Mashariki. Naamini wananchi wataendelea kuiunga mkono Serikali yetu ili ifanye mambo makubwa zaidi katika kipindi cha pili cha Awamu ya Tano kwa amani na maendeleo yake.

25.        Mheshimiwa Spika, baada ya salamu za shukurani nami naungana na Waheshimiwa Wabunge wenzangu walionitangulia kumpongeza Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, Mbunge wa Iramba Magharibi kwa kuteuliwa kuwa Waziri wa Katiba na Sheria na Mheshimiwa Dkt. Godwin Aloyce Mollel, Mbunge wa Siha kwa kuteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto.

Aidha, mkiwa viongozi mlioteuliwa, tambueni kuwa mnalo jukumu kubwa la kuwahudumia Watanzania, hususan katika kipindi hiki ambacho Nchi yetu imekumbwa na changamoto mbalimbali likiwemo janga la Corona.

SALAMU ZA POLE

26.        Mheshimiwa Spika, wakati tukiendelea na Mkutano huu wa 19, Bunge lako Tukufu lilipata pigo kwa kuondokewa na Wabunge wenzetu akiwemo Mheshimiwa Mchungaji Dkt. Getrude Pangalile Rwakatare, aliyekuwa Mbunge wa Viti Maalum; Mheshimiwa Richard Mganga Ndassa aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Sumve na Mheshimiwa Balozi Dkt. Augustine Philip Mahiga, aliyekuwa Mbunge na Waziri wa Katiba na Sheria.

27.        Mheshimiwa Spika, katika kipindi hicho pia, tuliondokewa na aliyekuwa Jaji Mkuu Mstaafu, Mheshimiwa Jaji Augustino Ramadhan. Aidha, niungane na Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kuwapa pole majirani zetu, wananchi wa Burundi kwa kifo cha aliyekuwa Rais wa Nchi hiyo, Mheshimiwa Pierre Nkurunzinza. Tuendelee kumuomba Mwenyezi Mungu azipumzishe Roho za wapendwa wetu wote mahali pema. Amina.

28.        Mheshimiwa Spika, vilevile, Taifa letu lilikumbwa na majanga mbalimbali ikiwa ni pamoja na mafuriko, COVID-19 na ajali za barabarani ambazo zilisababisha vifo, majeruhi na uharibifu wa mali. Napenda kutoa salamu za pole kwa ndugu, jamaa na marafiki waliopoteza wapendwa wao na wengine kupata majeraha kutokana na matukio hayo. Tumuombe Mwenyezi Mungu aziweke Roho za marehemu mahali pema na waliopata majeraha awajalie nafuu na kupona mapema. Amina.

MAFANIKIO YA SERIKALI YA AWAMU YA TANO

29.        Mheshimiwa Spika, kwa namna ya pekee kabisa nitumie fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kutokana na fikra na uongozi makini katika ujenzi wa Taifa letu. Ni dhahiri kuwa maono yake katika kuongoza na kusimamia utekelezaji wa Ilani ya CCM ya mwaka 2015 - 2020 na mipango ya Serikali, zimeleta mafanikio makubwa ambayo hivi sasa wote tunayaona.

30.        Mheshimiwa Spika, nyote mtakubaliana nami kwamba Mheshimiwa Rais na Makamu wake Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, wamekuwa mstari wa mbele kuhakikisha wanawafikia Watanzania, wanawasikiliza na kutatua kero zao. Lengo la ziara hizo, pamoja na mambo mengine lilikuwa ni kusimamia utekelezaji wa maelekezo ya Ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2015 ikiwemo kukagua miradi ya maendeleo; kuzungumza na watumishi na kuwafahamisha kuhusu falsafa ya Serikali ya awamu ya tano ya Hapa Kazi Tu.

31.        Mheshimiwa Spika, ziara hizo zimesaidia kwa kiasi kikubwa kuimarisha utendaji wa watumishi wa umma. Hivi sasa, wananchi wanapokwenda katika ofisi za umma wanapokewa, wanasikilizwa na kuhudumiwa vizuri. Aidha, usimamizi wa miradi ya maendeleo umeimarika sambamba na kuakisi thamani halisi ya fedha katika utekelezaji wa miradi hiyo. Hapa Bungeni ninawashukuru Waheshimiwa Wabunge kwa maoni, ushauri na ushirikiano ambao mmekuwa mkiutoa wakati wa ufuatiliaji wa shughuli za maendeleo sambamba na kuisimamia Serikali yetu.

Mambo mengi ya kujivunia yamefanywa na tumekuwa tukiyaeleza katika maeneo mengi kupitia mikutano ya hadhara, vyombo vya habari, nyaraka mbalimbali, uwepo wa miradi mingi ya kimkakati hadi kwa wananchi wa kawaida.

32.        Nitaeleza majukumu na miradi michache tena kwa kifupi ili kuwakumbusha nini Serikali imefanya katika kipindi hiki cha miaka mitano.

·       Marekebisho ya nidhamu kwa utumishi wa umma na uwajibikaji Serikalini ili kuwezesha Watumishi kutambua majukumu yao na kuwatumikia Watanzania.

·       Mapambano dhidi ya rushwa ndani ya Serikali na nje ya Serikali ili kulinda mali na fedha za umma. Hatua hii ni endelevu, lengo ni kung’oa mizizi ya rushwa nchini.

·       Kuimarisha vyombo vya ulinzi na usalama, mhimili wa Bunge na Mahakama. Matakwa yetu ni kuhakikisha kuwa nchi inabaki salama na mihimili ifanye kazi yake.

·       Mapambano dhidi ya matumizi ya dawa za kulevya ili kujihakikishia kuwa tunakuwa na Taifa lenye nguvukazi inayofanya kazi. Mapambano bado yanaendelea. Tutapambana na wazalishaji, wasambazaji, wauzaji na watumiaji wa dawa za kulevya.

·       Utambuzi wa watumishi hewa waliokuwa wanalipwa fedha wakiwa hawapo. Katika zoezi hili tumepata mafanikio makubwa na kuokoa shilingi Bilioni 19.83 kwa kuwaondoa kwenye mfumo wa malipo watumishi hewa 19,708 na wenye vyeti vya kugushi 15,411.

·       Ukusanyaji wa mapato ili kuwezesha Serikali kujenga miradi na kutoa huduma muhimu. Ukusanyaji wa mapato umeongezeka kutoka wastani wa shilingi Bilioni 800 kwa mwezi mwaka 2015 hadi wastani wa shilingi trilioni 1.5 kwa mwezi katika kipindi cha Julai 2019 hadi Aprili 2020.

·       Kuimarisha uwekezaji kwa kujenga viwanda. Hadi Aprili 2020 jumla ya viwanda vipya 8,477 vikiwemo vidogo, vya kati na vikubwa vimeanzishwa katika maeneo mbalimbali nchini na hivyo kuwezesha ongezeko la ajira viwandani za viwandani zipatazo 482,601.

·       Kuimarisha kilimo na masoko. Tumeimarisha kilimo cha mazao makuu, kama vile, Korosho, Pamba, Chai, Tumbaku, Kahawa, Michikichi na Mkonge pamoja na mazao ya chakula ili kuwa na uhakika wa usalama wa chakula.

·       Kuimarisha ushirika wa kilimo na upatikanaji wa pembejeo pamoja na huduma za ugani ili kuwafanya wakulima kuzalisha kwa tija.

·       Marekebisho ya Sheria ya madini yamefanyika sambamba na kuanzisha masoko ya madini 28 na vituo 12 vya ununuzi wa madini katika maeneo ya uchimbaji na hivyo kuongeza makusanyo ya Serikali, kupungua biashara haramu na utoroshaji madini kwenda nje. Mwezi Machi hadi Septemba, 2019 jumla ya kilo za dhahabu 4,680.28 zenye thamani ya shilingi bilioni 432.49 zimezalishwa na Serikali kukusanya shilingi bilioni 30.27.

·       Kuhamishia Makao Makuu Dodoma ambapo tayari Watumishi wapatao 15,361 wamehamia Dodoma na sasa fursa za uwekezaji zimeongezeka katika Jiji la Dodoma.

·       Kuboresha miundombinu na taaluma Sekta ya Elimu kwa ngazi zote kuanzia awali hadi Elimu ya Juu ikiwemo ujenzi na ukarabati wa madarasa, maktaba, maabara, nyumba za walimu, mabweni na ukarabati wa shule kongwe ili kuziongezea uwezo wa kupokea wanafunzi wengi zaidi.

·       Sera ya Elimu bila Ada ambayo inatumia zaidi ya Shilingi Bilioni 20.8 kila mwezi kwa ajili ya fidia ya ada, posho ya madaraka kwa walimu wakuu, wakuu wa shule na waratibu kata kila mwezi toka 2016 na tutaendelea. Hii imesaidia kuongeza uandikishaji na mahudhurio shuleni.

·       Kuimarisha huduma za afya kwa kujenga Zahanati, Vituo vya Afya, kujenga Hospitali za Wilaya, Mikoa, Kanda na za Kitaifa, huduma za Madawa na Vifaa Tiba. Tumejenga Zahanati 1,198 Vituo vya Afya 487, Hospitali za Wilaya 71, Hospitali za Rufaa za Mikoa 10, na Hospitali za Kanda 03 za Kusini – Mtwara, Magharibi – Tabora na Kanda ya Ziwa - Burigi.

·       Ujenzi wa miradi ya maji Vijijini na Mijini tumefikia asilimia 84Mijini na asilimia 70.1 Vijijini.

·       Ufufuaji wa Shirika la Ndege kwa kununua ndege kumi na moja (11) ambazo zinatoa huduma mikoa yote yenye Viwanja vya Ndege na nje ya nchi.

·       Ujenzi na ukarabati wa Viwanja vya Ndege kwenye mikoa isiyo na Viwanja vya Ndege unaendelea.

·       Ununuzi wa Rada nne mpya za kuongoza Ndege za kiraia zilizo Mwanza, Mbeya, Dar-es-Salaam na Kilimanjaro.

·       Ujenzi wa mradi mkubwa wa kufua umeme (Mwalimu Nyerere Dam) utakaozalisha Mg 2115 kwa sasa umefikia asilimia 40. Ujenzi una gharama ya Shilingi Trilioni 6.5

·       Usambazaji wa umeme Vijijini kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) tumefikia Vijiji kwa asilimia 80% ambapo hadi Aprili 2020 shilingi trilioni 2.27 zimetumika na kufanikisha jumla ya vijiji 9,112 kati ya 12,268 vya Tanzania Bara kuunganishwa na umeme kutoka vijiji 2,118 mwaka 2015.

·       Ujenzi wa Mradi wa Reli ya Kimataifa (SGR) wa Kilomita 300 Dar-es-Salaam–Morogoro. Mradi umefikia asilimia 78. Kipande cha Morogoro hadi Makutupora Kilomita 422 mradi umefikia asilimia 30 ya kazi. Lengo ni kukamilisha mradi huu ifikapo Juni 2021 kwa gharama ya Shilingi Trilioni 7.5.

·       Ujenzi wa Barabara kwa kiwango cha lami zikiwemo barabara kuu, barabara za mikoa na za wilaya zenye thamani ya zaidi ya Shilingi Trilioni 7.6. Pia serikali inaendelea kujenga barabara ya njia nne kutoka kutoka Kimara hadi Kibaha (km 19.2)

·       Ujenzi wa madaraja: ujenzi wa daraja la juu la Mfugale (Dar-es- Salaam), daraja la Furahisha (Mwanza) na daraja la Magufuli (mto Kilombero) umekamilika; ujenzi wa barabara ya pete (Ubungo interchange) umefikia asilimia 77 kwa shilingi bilioni 247; Aidha,  ujenzi unaendelea kwa daraja la New Selander (Dar- es-Salaam) kwa shilingi Bilioni 270. Daraja la Kigongo- Busisi shilingi Bilioni 699.2

·       Ujenzi wa Bandari, uboreshaji na upanuzi wa Bandari za Tanga, Dar-es-Salaam na Mtwara kwa Shilingi zaidi ya Trilioni 1.2. Pia, ujenzi wa Bandari ya Kigoma na Kalema umeshatengewa fedha.

·       Ujenzi wa Meli mpya yenye uwezo wa kubeba abiria 1,200 na tani 400 za mizigo katika Ziwa Victoria na ujenzi wa chelezo; ukarabati wa meli ya MV Victoria na MV Butiama ambapo katika kipindi cha mwaka 2015/16 hadi Aprili, 2020 jumla ya shilingi bilioni 111.7 zimetumika.

Vile vile, Serikali imekamilisha ujenzi wa meli moja mpya yenye uwezo wa kubeba abiria 200 na tani 200 za mizigo katika Ziwa Nyasa; na ukarabati wa meli ya mafuta ya MT Sangara katika Ziwa Tanganyika.

·       Ujenzi wa Vivuko vya MV Kigamboni, MV Pangani, Kigongo -Busisi, MV Sengerema na Nyamisati.

·       Urejeshaji na usimamizi wa mali za Ushirika zilizokuwa zimechukuliwa kinyume na utaratibu, kama vile, NYANZA, SHIRECU, KNCU, Mamlaka ya Mkonge Tanzania, n.k.

·       Kusimamia maboresho kwenye Sekta ya Uvuvi na Mifugo kwa kuvua na kufuga kisasa, kujenga viwanda na masoko yake.

33.        Mheshimiwa Spika, Serikali ya Chama cha Mapinduzi kupitia Bunge lako Tukufu katika kipindi cha miaka minne imeidhinisha jumla ya shilingi trilioni 33.1 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo kote nchini ikiwemo miradi ya kimkakati niliyoitaja hivi punde

MVUA KUBWA ZILIZONYESHA NCHINI

34.        Mheshimiwa Spika, baadhi ya maeneo ya Nchi yetu yalikumbwa na mafuriko kufuatia mvua nyingi zilizonyesha nchini. Mafuriko hayo yalisababisha madhara mbalimbali ikiwemo uharibifu wa miundombinu, mali na vifo. Serikali imeendelea kuchukua hatua za kurejesha hali ya miundombinu iliyoharibika na zoezi hilo ni endelevu.

35.        Mheshimiwa Spika, mvua nyingi tulizopata msimu huu zimeleta neema ya mavuno lakini pia katika baadhi ya maeneo mazao yameharibika. Hivyo, niendelee kusisitiza kauli ya Waziri wa Kilimo wakati akiwasilisha Hoja ya Wizara yake kuwa hali ya chakula nchini imeendelea kuimarika. Kwa msingi huo, hatutarajii kuwa na upungufu wowote wa chakula kwa msimu ujao. Muhimu kwetu ni kuongeza umakini wa matumizi kwa kuweka akiba ya chakula ili kitosheleze mahitaji ya familia hadi msimu ujao.

MAPAMBANO DHIDI YA HOMA KALI YA MAPAFU COVID 19

36.        Mheshimiwa Spika, mwezi Machi, 2020, baada ya Shirika la Afya Duniani (WHO) kutangaza kuwa COVID 19 ni janga la dunia, ambako nchi nyingi duniani zilipata maambukizi makubwa, Tanzania tulitangaza kisa cha kwanza tarehe 15 Machi, 2020.

37.        Nchi nyingi duniani zikiwemo nchi za Bara la Afrika ugonjwa huu ulianza kuingia. Kila nchi ilichukua hatua kadhaa za kudhibiti maambukizi zikiwemo watu kutotoka ndani ya nyumba zao “Lockdown”, kuzuia mikusanyiko kwa kufunga mashule, vyuo, michezo, aina zote za usafiri wa ndani na nje, maeneo ya Ibada na shughuli za uzalishaji maeneo ya kazi, viwanda, n.k. vilifungwa.

38.        Tanzania nasi tulianza kuchukua hatua kadhaa ili kukabiliana na maambukizi kwa kuunda Kamati 3 za ngazi ya Mawaziri, Watendaji na Wataalam wa Afya kwa lengo la kufanya tathmini ya hatua za kuchukua ili kupunguza maambukizi na kulinda anguko la kiuchumi.

39.        Hatua zilizochukuliwa ni kupunguza misongamano kwa kufunga shule, vyuo, mikutano, kunawa maji, matumizi ya vitakasa mikono na kuvaa barakoa.

40.        Mheshimiwa Spika, siku ya tarehe 22 Machi, 2020 Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania akiwa Jijini Dodoma na tarehe 03 Mei, 2020 akiwa Chato aliwataka Watanzania kuwa watulivu waondoe hofu ya ugonjwa huu na ni ugonjwa kama magonjwa mengine, kama vile Malaria, UKIMWI, Kifua Kikuu, n.k. na kuwataka Watanzania kuchukua tahadhari na kuendelea na shughuli za uzalishaji mali, kufanya kazi ofisini, viwandani, mashambani na kutofunga nyumba za Ibada.

41.        Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Rais alihutubia tena Taifa tarehe 16 Aprili, 2020 kwa kutoa maelekezo na kusisitiza yafuatayo:

Mosi:           Aliwasihi Watanzania kuondoa hofu kwa kuwa Mungu yupo nasi na hivyo, waendelee kuchapa kazi ili kunusuru uchumi wa mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla na kuzingatia kanuni za afya.

Pili:              Watanzania watumie siku tatu kumuomba na kumlilia Mwenyezi Mungu kwani Mungu yu pamoja nasi na atatusikia huku akiendelea kusimamia kauli yake ya kuwataka Watanzania wafanye kazi kwa bidii na kumtegemea Mungu bila kujali kauli za kebehi na ukosoaji kutoka pande mbalimbali za dunia;

Tatu:           Alihimiza Watanzania kumtegemea Mwenyezi Mungu na kwamba Mwenyezi Mungu pekee ndiye atakayetuvusha na kutuepusha na janga hili;

Nne:            Aliwahimiza Watanzania kutopuuza umuhimu wa tiba mbadala katika mapambano dhidi ya COVID-19. Kauli hii, imekuwa chachu katika kuimarisha tafiti za dawa za asili ambazo zimekuwa na mchango mkubwa katika kupambana na maradhi mbalimbali ikiwemo COVID-19; na

Tano:           Tarehe 20 Mei, 2020 akiwa Singida, aliwaomba Watanzania watumie siku tatu kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa maajabu aliyoyafanya kwa Taifa letu kwa kutuepusha kusambaa kwa virusi vya COVID-19.


42.        Mheshimiwa Spika, hali iliyoko sasa, ni kuwa maambukizi yamepungua na wagonjwa wamepungua hospitalini. Kama kuna anayestahili sifa ni Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa msimamo wake usiotetereka na maono ya mbali aliyokuwa nayo yamekuwa chachu katika kupunguza maambukizi ya COVID-19 na kulinda uchumi wa Nchi. Mheshimiwa Rais ameifanya Tanzania kuwa ya kupigiwa mfano duniani kwa namna alivyoshughulikia ugonjwa huu.

43.        Mheshimiwa Spika, pongezi maalum kwa Viongozi wa dini kwa namna walivyoshirikiana na waumini katika mapambano ya ugonjwa wa COVID-19. Wakati wote Viongozi hao wamekuwa wakiwapatia waumini (Watanzania) faraja pia na wagonjwa kwamba Mwenyezi Mungu atawaponya. Hatua hizo zimekuwa mhimili mkubwa wa upendo, umoja, mshikamano na ujasiri miongoni mwa Watanzania. Tunawashukuru sana.

44.        Mheshimiwa Spika,taarifa iliyotolewa na Taasisi ya Ushirikiano wa Kiuchumi na Maendeleo (Organisation for Economic Cooperation and Development - OECD) inabashiri kuwa kitendo cha kuwafungia watu ndani yaani Lockdown kumesababisha vifo kwa njaa na kusinyaa kwa uchumi wa nchi zilizoendelea kwa asilimia 2 kila mwezi. 

45.        Mheshimiwa Spika,hivi sasa, nchi nyingi zinakubaliana kuwa “Lockdown” si hatua sahihi ya kukabiliana na COVID-19. Vilevile, kisayansi inakadiriwa kuwa nchi ambazo ziliwafungia watu wake na mipaka yake zipo katika hatari ya kukumbwa na madhara makubwa ya ugonjwa huo pindi utakapotokea mlipuko wa pili na hata wa tatu.

46.        Mheshimiwa Spika,kwa mantiki hiyo, mtizamo na hatua zilizochukuliwa na Tanzania katika kupambana na COVID-19 zinaonesha upekee tulionao kama nchi. Serikali, inayo kila sababu ya kuwapongeza Watanzania ambao si tu walipokea maelekezo ya Serikali lakini pia walifanya hivyo kwa uaminifu mkubwa na kwa hiari yao wenyewe bila kushurutishwa na mamlaka yoyote ya nchi.

47.        Mheshimiwa Spika, nitumie fursa hii kuwashukuru wataalamu wetu wa afya kwa kuwahudumia wagonjwa wa COVID19. Wataalamu wetu hao, walitekeleza majukumu yao bila kujali hatari ya virusi hivyo kwa maisha yao na wapendwa wao. Vievile, naishukuru sekta binafsi, mtu mmoja mmoja na wadau wote ambao waliitikia wito wa Serikali kwa kutoa michango ya hali na mali katika kufanikisha vita dhidi ya COVID19 nchini. Kipekee, niwashukuru wamiliki wa viwanda ambao waliitikia wito wa Mheshimiwa Rais na kuanza kuzalisha vifaa kinga hapa nchini badala ya kuagiza nje waende kufanya hivyo.

48.        Mheshimiwa Spika, ni matumaini yetu kwamba zile nchi zilizoondoa vizuizi sasa zinalo somo la kujifunza kutoka Tanzania. Aidha, suala la kudhibiti maambukizi ya COVID 19 litaendelea kuwa kipaumbele cha Serikali kwa sasa sambamba na malengo ya muda mrefu ya kumaliza ugonjwa huo hususan katika kipindi hiki ambacho Shirika la Afya Duniani (WHO) nalo limebainisha kwamba COVID 19 si gonjwa la kuondoka mara moja. Hivyo, watu na dunia kwa ujumla hatuna budi kujifunza namna ya kuishi na virusi hivyo kama ilivyo kwa UKIMWI na virusi vingine, huku tukifanya kazi ili kujiletea maendeleo.

49.        Mheshimiwa Spika, tarehe 9 Juni Bunge lako Tukufu lilipitisha Azimio la kumpongeza na kumuunga mkono Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa namna alivyomudu kuivusha nchi katika janga la COVID-19. Waswahili husema mnyonge mnyongeni, haki yake mpeni. Katika hili, nami naomba niseme kidogo kwa kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa hotuba zake zote zilizohusu ugonjwa huu ambapo alihimiza masuala muhimu kwa Watanzania katika kukabiliana na janga hili na zilitibu hofu kubwa iliyokuwa imetanda kwa Watanzania.

50.        Mheshimiwa Spika, leo tunaona idadi ya wagonjwa wanaougua inapungua sana. Kwa mfano, taarifa ya leo, Jumatatu tarehe 15 Juni, 2020 kutoka katika Vituo vya kutolea huduma na Hospitali za Serikali na Binafsi nchini, inaonesha kuwa tuna wagonjwa 75 katika Mikoa 12 na Mikoa 14 haina wagonjwa ikiwemo Mkoa wa Dodoma, Geita, Kagera, Katavi, Kigoma, Lindi, Mara, Manyara, Pwani, Rukwa, Ruvuma, Simiyu, Songwe na Tabora. Pamoja na mwenendo huu, ninawaomba wananchi wote kuendelea kuchukua tahadhari zote za kiafya na miongozo inayotolewa na Serikali.

51.        Nampongeza sana Mheshimiwa Ummy Mwalimu (Mb), kwa kazi kubwa aliyoifanya usiku na mchana kuhakikisha kuwa maambukizi yanapungua kwa kasi. Tumshukuru Mwenyezi Mungu kwa hatua tuliyofikia. Pia, nawashukuru Katibu Mkuu, Mganga Mkuu wa Serikali na Watendaji wote wa Wizara ya Afya kwa usimamizi wa tatizo hili na naamini mnaendelea vema. Hongereni sana.

SHUGHULI ZILIZOTEKELEZWA KATIKA BUNGE LA 11 (2015–2020)

52.        Mheshimiwa Spika, wakati Bunge la 11 likielekea kuhitimisha shughuli zake, limefanikiwa kutekeleza masuala mbalimbali ikiwemo kujibu maswali na hoja zilizowasilishwa na Waheshimiwa Wabunge; kujadili na kupitisha Miswada ya Serikali; Maazimio mbalimbali yenye kuhusisha Mikataba na Itifaki za Kikanda na Kimataifa; kupokea kauli za Serikali kuhusu ufafanuzi wa mambo mbalimbali pamoja na kuunda Tume kwa ajili ya kufuatilia masuala muhimu yenye maslahi mapana kwa Taifa letu.

Maswali na Majibu

53.         Mheshimiwa Spika, katika kipindi chote cha Bunge la 11 linaloelekea kuhitimisha uhai wake tarehe 16 Juni, 2020 jumla ya maswali ya msingi 3,962 yameulizwa na Waheshimiwa Wabunge na kujibiwa na Serikali. Aidha, maswali ya nyongeza 9,563 yameulizwa kutokana na maswali ya msingi na kujibiwa na Serikali. Vilevile, jumla ya maswali 178 ya kawaida na ya nyongeza 162 yameulizwa na Wabunge na kujibiwa na Mheshimiwa Waziri Mkuu kupitia utaratibu wa maswali ya papo kwa papo kwa Waziri Mkuu.

54.        Mheshimiwa Spika, kupitia Mkutano huu wa Kumi na Tisa, jumla ya maswali 471 ya msingi na mengine 69 ya nyongeza yaliulizwa na Waheshimiwa Wabunge na kupatiwa majibu na Serikali.

Miswada, Maazimio ya Bunge na Kauli za Serikali


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527