HOSPITALI YA HALMASHAURI YA WILAYA YA SHINYANGA ILIYOPO ISELAMAGAZI YAANZA KUTUMIKA RASMIMojawapo wa majengo yanayotumika katika utoaji wa huduma za matibabu katika hospitali ya halmashauri ya wilaya ya Shinyanga eneo na Kata ya Iselamagazi.
Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga Mhe. Jasinta Mboneko, Mbunge wa Jimbo la Solwa Mh. Ahmed Salum pamoja na Viongozi wa halmashauri ya wilaya ya Shinyanga wakikata utepe kuashiria kuanza kwa utoaji wa huduma za matibabu katika hospitali hiyo.

Na Mwandishi wetu,Shinyanga Press Club Blog 
Wakazi wa halmashauri ya wilaya ya Shinyanga Mkoani humo hususani wanawake wameishukuru Serikali ya awamu ya tano chini ya Rais Dk. John Magufuli kwa kuwatatulia adha ya kutembea umbali mrefu kutafuta matibabu ya juu zaidi ambapo kwa sasa wameondokana na changamoto ya kufuata huduma umbali wa zaidi ya kilomita 100 baada ya hospitali ya halmashauri hiyo kuanza kutoa huduma. 

Wakizungumza mara baada ya uzinduzi wa utoaji wa matibabu katika hospitali hiyo juzi baadhi ya wanawake akiwemo Elizabeth Paul Mkazi wa Iselamagazi na Regina William mkazi wa Didia wamesema kuwa upatikanaji wa matibabu karibu na maeneo yao utasaidia kupunguza changamoto ya vifo vya kina mama na watoto vilivyokuwa vikitokea wakiwa njiani kuelekea mjini Shinyanga katika hospitali ya Rufaa ya Mkoa. 

Wameongeza kuwa kina mama wengi walikuwa wakipoteza maisha kutokana na ukosefu wa matibabu ya juu zaidi ikiwemo upasuaji, hali iliyokuwa ikiwalazimu kutafuta usafiri wa kuwafikisha mjini Shinyanga umbali wa zaidi ya kilomita 100 huku miundombinu ya barabara ikiwa si rafiki na kusababisha kina mama kufariki dunia wakiwa njiani kufuata matibabu. 

Awali akisoma taarifa ya Ujenzi wa hospitali hiyo Mganga Mkuu wa halmashauri ya wilaya ya Shinyanga Dkt. Mameritha Basike amesema kuwa ujenzi huo umegharimu zaidi ya Shilingi bilioni 1.5 kutoka Serikali kuu huku akisema kuwa kuanza kutoa huduma kutasaidia kupunguza vifo vya akina mama wajawazito waliokuwa wakipoteza maisha kwa kukosa huduma za matibabu karibu na maeneo yao

“Tumefanikiwa kupunguza vifo vya kina mama waliokuwa wakipoteza maisha wakati wa kujifungua ambapo kwa Mwezi January hadi December 2019 vimetokea vifo 14 na kwa kipindi cha kuanzia January hadi Mei 31 mwaka 2020 hakuna kifo hata kimoja jambo linaloonesha jitihada kubwa zinazofanywa na madaktari”,amesema Dk. Mameritha 

Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Solwa Mkoani Shinyanga Mhe. Ahmed Salum amemshukuru Rais DK. John Magufuli kwa kuridhia kutoa fedha za ujenzi wa hospitali hiyo ili kuwatatulia changamoto wakazi wa halmashauri yake ambao walikuwa wakipata usumbufu wanapougua na kuhitaji matibabu ya juu zaidi, huku akibainisha kuwa baada ya muda mfupi huduma zote za kijamii zitakuwa zimesogezwa karibu na wananchi kutokana na ofisi ya Mkurugenzi na timu yake kuhamia makao makuu ya halmashauri hiyo yaliyopo kata ya Iselamagazi.

"Kwanza napenda kumshukuru Rais Dk. John Magufuli kwa maamuzi yake yanayokwenda kugusa afya za jamii kama mnavyokumbuka tulipewa shilingi bilioni 1.5 kujenga majengo 7 lakini sisi tumeenda mbali zaidi tukaongeza majengo mawili na tunamuombea kwa Mwenyezi Mungu aendelee kumpa afya njema rais wetu ili aendelee kuwahudumia watanzania",amesema Ahmed Salum 

Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya Shinyanga Mhe. Hoja Mahiba amesema kuwa kukamilika kwa hospitali hiyo ni suluhisho licha ya kwamba bado ipo changamoto kwa wakazi wa kata za Mwakitolyo na Lyabukande ambazo ziko umbali wa zaidi ya kilomita 100 toka katika eneo hilo na kusema kuwa wameshapeleka maombi ofisi ya Rais TAMISEMI ili zahanati za maeneo hayo ziweze kupandishwa hadhi na kuwa vituo vya afya. 

Mgeni rasmi katika ufunguzi wa hospitali hiyo Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Jasinta Mboneko amewataka wahudumu wa afya na Madaktari katika hospitali hiyo, kuepuka utoaji wa lugha chafu kwa wagonjwa na kushindwa kutoa huduma huku akisisitiza kuwa hatapenda kusikia malalamiko ya wananchi wamekosa huduma ya matibabu kwa uzembe wa wahudumu. 

Mboneko amesema uwepo wa hospitali hiyo utasaidia kupunguza vifo vya wajawazito wakati wa kujifungua kutokana na kuchelewa kupata huduma,ambapo kwa sasa wananchi wamesogezewa huduma karibu na wataondokana na adha ya kusafiri umbali mrefu ambapo amewataka kuacha tabia za kuugua na kwenda kwa waganga wa kienyeji kupiga ramli badala yake watumie maeneo hayo ya huduma za afya yaliyothibitishwa na serikali. 

“Huduma za matibabu kwa wagonjwa wa nje (OPD) zimeanza kutolewa hapa ni hatua moja kubwa kwani fedha ya Serikali imetumika vizuri majengo yote yamejengwa kwa kiwango kizuri yatunzeni yadumu yawahudumie kwa muda mrefu maana hii ni mali yenu”,amesema Mboneko. 

Katika hatua nyingine Mboneko amesema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dr John Pombe Magufuli amewakumbuka wananchi wake wanyonge kwa kuboresha huduma za afya ili wananchi wapate huduma karibu na Makazi yao ili kuondoa adha ya kusafiri umbali mrefu ambapo vituo vya afya na hospitali nyingi zimejengwa maeneo mbalimbali nchini ili kutatua changamoto kwa watanzania.
Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga Jasinta Mboneko akisisitiza Jambo kwa Wananchi wa Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga juu ya kuilinda na kuithamini Hospitali yao ambayo itakuwa suluhisho.

Mbunge wa Jimbo la Solwa Mhe. Ahmed Salum akiwataka wakazi wa jimbo lake kuitumia hospital  ya Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga ambayo imesogezwa karibu yao ili kuokoa vifo vya kina mama 
Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Shinyanga Ngassa Mboje akiongea na Wananchi waliojitokeza katika uzinduzi wa hospitali hiyo.
Mkurugenzi wa halmashauri ya Shinyanga Mhe. Hoja Mahiba akizungumza na Waandishi wa habari juu ya changamoto za afya katika eneo lake 
Mganga Mkuuu wa halmashauri ya Shinyanga Dr. Mameritha Basike akisoma taarifa ya ujenzi wa hospitali iliyopo eneo la Iselamagazi iliyogharimu shilingi bilioni 1.5 
Mmoja wa wakazi wa Kata ya Iselamagazi yalipo makao makuu ya halmashauri ya wilaya ya Shinyanga Bi Elizabeth Paul akieleza hisia zake baada ya matibabu ngazi ya wilaya kuwafkia karibu 
Wa pili kulia ni Mbunge wa Jimbo la Solwa Mhe. Ahmed Salum akifuatiwa na mkuu wa wilaya ya Shinyanga  Mhe. Jasinta Mboneko pamoja na Mwenyekiti wa baraza la wazee Mkoa wa Shinyanga Mzee Sengerema wakitazama namna huduma zinavyotolewa kwa wagonjwa mbele yao ni mmoja wa wagonjwa wanaopatiwa huduma kwa mara ya kwanza 
Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga Mhe. Jasinta Mboneko  akipanda mti kuashiria kuanza kwa huduma katika hospitali hiyo 
Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Shinyanga Ngassa mboje akipanda mti wa kumbukumbu 
Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Shinyanga Mhe. Hoja Mahiba akipanda mti wa kumbukumbu siku ya uzinduzi wa utoaji wa huduma za afya katika hospitali ya wilaya.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post