MTOTO WA MIAKA MIWILI AFARIKI DUNIA KWA KUNG'ATWA NA FISI SHINYANGA


Picha ya Fisi

Na Kadama Malunde - Malunde 1 blog
Mtoto aliyejulikana kwa jina la Charles Christian Makilika mwenye umri wa miaka miwili na nusu amefariki dunia baada ya kung’atwa na fisi akicheza na wenzake nje ya nyumba yao katika kitongoji cha Mwagala maeneo ya Ugweto kata ya Ibadakuli Manispaa ya Shinyanga.

Kamanda wa Polisi mkoa wa Shinyanga ACP Debora Magiligimba tukio hilo limetokea jana Jumatatu Juni 1,2020 majira ya saa moja jioni (1: 00) huko kitongoji cha Mwagala, maeneo ya Ugweto katika Manispaa ya Shinyanga. 

“Mtoto aitwaye Charles Christian Makilika, mwenye umri wa miaka miwili na nusu, mkazi wa Ugweto akiwa anacheza na watoto wenzake nje ya nyumba yao alijeruhiwa kwa kung'atwa na fisi sehemu za usoni kisha kuburuzwa umbali wa mita 50 ambapo fisi huyo alimuachia baada ya kusikia kelele za wananchi waliokuwa wakimfukuza”,amesema Kamanda Magiligimba.

Kamanda Magiligimba amesema mtoto huyo alifariki dunia akiwa njiani akisafirishwa kwenda hospitali ya rufaa ya Bugando mkoani Mwanza kwa matibabu na mwili wa marehemu umehifadhiwa katika hospitali ya rufaa mkoa wa Shinyanga. 

"Natoa wito kwa wazazi na walezi kuhakikisha kwamba watoto wako mazingira salama muda wote, wasiachwe peke yao , wananchi wanatakiwa kuchukua tahadhari hasa kwa kipindi hiki ambacho fisi wamekuwa wakionekana maeneo mbalimbali ya mkoa wetu wa Shinyanga",amesema Kamanda Magiligimba.

Download/Pakua App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527