CCM YATANGAZA RATIBA YA MCHAKATO WA KUPATA WAGOMBEA URAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA NA ZANZIBAR


CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimetangaza kuanza rasmi kwa mchakato wa kutafuta wagombea katika kiti cha Urais, Wabunge, madiwani, wawakilishi na masheha huku kikiwaonya watia nia wote kutojihusisha na rushwa, kuwa wanyenyekevu na kufuata taratibu za chama hicho vinginevyo wataenguliwa.


Hayo yamesemwa leo leo Juni 12, 2020, na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa chama hicho, Humphrey Polepole wakati akizungumza na wanahabari katika ofisi ndogo za CCM, Lumumba jijini Dar es salaam.

Amesema, kwa upande wa mchakato wa urais wa Tanzania Bara, tukio la kwanza litakuwa ni uchukuaji wa fomu, litakaloanza tarehe 15 hadi 30 Juni 2020, huku tukio la pili ambalo litakwenda sambamba ni utafutaji wa wadhamini mikoani.

“Tukio la pili litakalofanyika kati ya tahere 15 hadi 30 Juni 2020, mgombea wa CCM atakuwa na kazi ya kutafuta wadhamini mikoani, ndani ya siku 15 akamilishe kwa pamoja kuchukua fomu na kutafuta wadhamini,” amesema Polepole.

Tukio la tatu litakuwa ni vikao vya uchujaji, ambapo tarehe 6 hadi 7 Julai mwaka huu, kitaketi kikao cha Sekretarieti ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM, kitakachoanzisha mchakato wa uchujaji, kisha tarehe 8 Julai 2020 kitaketi kikaocha Kamati ya Usalama na Madili ya chama hicho.

Tarehe 9 Julai 2020, kitaketi Kikao cha Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM, ambacho kitatoa mapendekezo yake kwa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM juu ya majina ya wanachama wasiozidi watano, wanaoomba kugombe anafasi hiyo.

Polepole amesema, tarehe 10 Julai 2020, Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM kitapendekeza kwa Mkutano Mkuu wa CCM, majina matatu ya wanachama wa chama hicho, wanaoomba kugombea urais.

“Tarehe 10 Julai 2020, kitaketi kikao cha Halmshauri Kuu ya Taifa ya CCM ambacho na chenyewe kitakuwa na kazi ya kupendekeza kwa mkutano mkuu wa CCM wa Taifa, majina yasiyozidi matatu ya wanachama wanaoomba dhamana ya kugombea urais,” amesema Polepole.

Wakati huo huo, Polepole amesema tarehe 11 hadi 12 Julai mwaka huu, Mkutano Mkuu wa CCM Taifa utachagua jina moja la mgombea wa urais wa Tanzania.

“Tarehe 11 na 12 Julai 2020, utaketi mkutano mkuu wa CCM Taifa ambao na wenyewe utakuwa na kazi ya kuchagua jina moja la mwanachama atakayesimama katika uchaguzi wa urais Tanzania kwa tiketi ya chama chetu cha CCM,” amesema Polepole.

“Tarehe 15 hadi 30 Juni, kutafuta wadhamini mikoani, baada ya hapo vitafuata vikao vya uchujaji, tarehe 1 hadi 2 Julai itaketi Sekretarieti ya Kamati Maalumu ya Halmashauri Kuu ya Taifa Zanzibar, tarehe 3 Julai kitaketi kikao cha Kamati ya Usalama na Maadili Zanzibar,” amesema Polepole.

Amesema, Kikao cha Kamati Maalumu ya Halmashauri Kuu ya CCM kitakua tarehe 4 Julai 2020 kwa ajili ya kutoa mapendekezo juu ya wanachama waliojitokeza kuomba kugombea urais wa Zanzibar.

Kikao hicho kitafuatiwa na Kikao cha Kamati Kuu ya Halmashauri ya Taifa kitakachoketi tarehe 9 Julai 2020, kwa ajili ya kupendekeza majina matatu ya wanachama wanaoomba kugombea kiti hicho. Kisha, tarehe 10 Julai mwaka huu, Halmshauri Kuu ya Taifa ya CCM kitachagua jina moja la mgombea.

Polepole amesema, tarehe 11 hadi 12 Julai, Mkutano Mkuu wa CCM taifa utaketi kwa ajili ya kuthibitisha jina la mwanachama atakayesimama katika uchaguzi wa urais Zanzibar, kupitia chama hicho.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527