AUA MKE WAKE KWA KUMKATA PANGA KICHWANI

Picha haihusiani na habari hapa chini

Na Damian Masyenene – Shinyanga Press Club Blog
Watu wawili ambao ni mme na mke wakazi wa Kijiji na Kata ya Igunda tarafa ya Dakama wilaya ya kipolisi Ushetu mkoani Shinyanga wamefariki baada ya kuzuka ugomvi unaoelezwa kutokana na wivu wa kimapenzi.
 
Katika tukio hilo mwanamke aitwaye Christina Jakobo (41) akiwa chumbani aliuawa kwa kukatwa na panga kichwani na shingoni na mume wake aitwaye John Chumila (42).
 
Kwa mujibu wa taarifa kwa vyombo vya habari leo Juni 23, 2020 iliyotolewa na Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, ACP  Joseph Paul amesema baada ya tukio hilo mwanaume huyo na yeye alijinyonga kwa kutumia kamba ya katani juu ya kenchi chumbani humo.

Kamanda Paul amesema kuwa tukio hilo lilitokea Juni 21, mwaka huu saa 3:00 usiku ambapo mauaji hayo yalitokea chumbani kwa kile kinachodaiwa kuwa ni wivu wa mapenzi kwani mme aligundua kuwa mke wake anatoka nje ya ndoa enzi za uhai wake.

Ameeleza kuwa marehemu hao walikutwa wamejifungia chumbani, ambapo miili yao imekabidhiwa kwa ndugu kwa ajili ya taratibu za mazishi.

Kaimu Kamanda huyo wa Polisi, ACP Paul ametoa wito kwa wanandoa kuacha tabia za kujichukulia sheria mikononi hivyo wafuate taratibu za kuwapeleka wenza wao kwenye madawati yaliyopo ofisi za ustawi wa jamii pamoja na vituo vya polisi ili kupata ufumbuzi pindi wapatapo matatizo katika ndoa zao.

Download/Pakua App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527