ALIYEKUWA WAZIRI WA ULINZI WA MAREKANI, JAMES MATTIS AMTUHUMU TRUMP KWA KUTAKA KUWAGAWA WAMAREKANI KWA MATABAKA


Aliyekuwa Waziri wa Ulinzi wa Marekani, James Mattis  ametangaza kuwaunga mkono wananchi wa Marekani wanaondamana kulaani ubaguzi wa rangi na mienendo ya polisi ya Marekani hususan dhidi ya Wamarekani wenye asili ya Afrika.


Mattis alitangaza msimamo huo katika taarifa iliyochapishwa jana Jumatano na gazeti la The Atlantic, ambapo amemtuhumu Trump kuwa anajaribu kuwagawanya Wamarekani kimatabaka.

Ameeleza bayana kuwa, "Donald Trump ni rais wa kwanza katika uhai wangu ambaye hawaunganishi Wamarekani, bali hata hajifanyi kana kwamba anajaribu kuwaunganisha." 

Amesema taifa hili linashuhudia matokeo ya jitihada za makusudi za miaka mitatu za Trump za kuwagawa wananchi wa Marekani.

James Mattis amesema ;, "tunaweza kuungana bila yeye (Trump), hili si jambo jepesi, lakini linawezekana kwa ushirikiano."

Kadhalika amekosoa hatua ya rais huyo kutumia jeshi la taifa kuzima maandamano ya kiraia, ambayo ni haki ya msingi iliyoanishwa kwenye katiba ya nchi hiyo. 

 Mattis ambaye ni jenerali mstaafu aliachia ngazi mwishoni mwa mwezi Februari mwaka 2018, baada ya kuhitalifiana na Trump

 Kama jibu lake kuhusu ukosoaji huo, Trump alituma mfululizo wa ujumbe kwenye Twitter ambapo alisema..."Sikupenda mtindo wake( James Mattis  )  wa uongozi au yeye mwenyewe sikumpenda na wengine wengi wanakubaliana na hilo, "Afadhali  aliondoka mapema"


Wananchi wa Marekani wamekuwa wakiandamana kwa zaidi ya wiki moja sasa, tangu alipouawa kikatili na polisi mweupe, George Floyd, Mmarekani mweusi katika mji wa Minneapolis jimboni Minnesota.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527