VIFO VYA CORONA KUCHUNGUZWA

Na WAMJW – Mwanza

Vituo vya kutolea huduma za afya nchini vyatakiwa kufanya uchunguzi juu ya kifo chochote kitakachotokana na ugonjwa wa corona ili kubaini kama mgonjwa alihudumiwa ipasavyo kabla ya kifo kutokea.

Agizo hilo limetolewa na Mganga Mkuu wa Serikali Prof. Abel Makubi akiwa Jijini Mwanza mara baada ya kuagana na uongozi wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Ziwa – Bugando alipokuwa akifanya kazi awali kama Mkurugenzi Mtendaji kabla ya kuteuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli kuwa Mganga Mkuu wa Serikali.

“Kwakweli tusingependa kuona mgonjwa anafariki kwa sababu zisizo na msingi, naagiza hospitali zote zenye kamati ya uchunguzi (Clinical Audit) kufanya uchunguzi wa vifo vinavyohusiana au kutokana na corona ili kuona kama kulikuwa na tatizo lolote katika kumpokea mgonjwa au katika kumhudumia” alisema Prof. Makubi

Prof. Makubi amewataka wananchi kuelewa kuwa sio kila kifo kinachotokea hivi sasa kinasababishwa na ugonjwa wa corona kwa kuwa yapo magonjwa mengine pia ambayo yanatushamblia binadamu. 

“Siyo kweli kwamba mgonjwa akiwa na presha, kisukari, figo au kansa akifariki iwe imesababishwa na corona, tuendelee kuwahudumia wananchi, kuepusha vifo vinavyoweza kuwa na uhusiano wa corona”. Alisema Prof. Makubi.

Aidha, Prof. Makubi ametoa rai kwa vituo vya afya kuwapokea wagonjwa wote na kuwapatia matibabu bila kuwabagua kuwa na dalili za corona.

“Serikali inapenda kuona wagonjwa wa corona wanapokelewa nakupata matibabu, tuendelee kuwapokea na kuwahudumia huku tukichukua tahadhari ya maambukizi”. Alisema Prof. Makubi.

“Watumishi wa afya wasiwe na ubaguzi wa kuchagua wagonjwa wa kuwahudumia au mpaka apimwe kipimo cha covid-19 ndio ahudumiwe, tuwapokee wote lakini wakati huo tukichukua tahadhari zote za kujikinga na ugonjwa”.  Alisisitiza Prof. Makubi.

Katika hatua nyingine Prof. Makubi amesema kuwa Serikali inaendelae kusambaza vifaa kinga kwa ajili ya kuwawezesha watoa huduma kujikinga na ugonjwa huo wakati wakitoa huduma.

“Serikali imeanza kugawa vifaa kinga kama vile PPE, masks pia sanitizer kwa ajili ya vituo vyote vya afya Tanzania, kwahiyo pasiwepo kisingizio chochote cha kushindwa kumhudumia mgonjwa wa corona kwa sababu ya vifaa kinga”


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527