WAJUMBE WA BODI YA SHUWASA WAKAGUA UJENZI WA MRADI WA MAJI WA NGOGWA - KITWANA..WANANCHI WAIPONGEZA SERIKALI


Na Suleiman Abeid - Kahama
WAKAZI wa Kata za Ngogwa na Busoka wilayani Kahama mkoani Shinyanga wameipongeza Serikali ya Awamu ya tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwa jinsi inavyotekeleza Ilani yake ya Uchaguzi kwa vitendo.

Pongezi hizo zimetolewa na wananchi hao mbele ya wajumbe wa Bodi ya Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Manispaa ya Shinyanga (SHUWASA) waliotembelea na kukagua utekelezaji wa Mradi wa ujenzi wa maji wa Ngogwa – Kitwana unaotekelezwa kwa mpango wa Force Account Mei 8,2020.

Wananchi hao wamesema mradi huo utakapokamilika wataondoka na kero ya ukosefu wa maji safi na salama ambayo wamedumu nayo kwa kipindi kirefu ambapo mpaka hivi sasa wanalazimika kutembea umbali mrefu kutafuta maji kwa ajili ya matumizi yao ya kila siku.

Mmoja wa wakazi hao anayejitambulisha kwa jina la Paschal Maganga mkazi wa kitongoji cha Nyandolwa kata ya Ngogwa wilayani Kahama anasema yeye binafsi anaishukuru serikali ya awamu ya tano kwa kuwaondolea kero ya muda mrefu ya ukosefu wa maji katika kata yao.

“Tunashukuru sana kwa serikali yetu kwa kutuletea mradi wa maji katika kata yetu ya Ngogwa, maana tulikuwa na ukame mkubwa wa maji katika maeneo yetu, lakini baada ya awamu hii ya tano kuanza kutekeleza mradi huu, ni wazi kero hii sasa inamalizika,”

“Tulikuwa tunapata shida kubwa ya maji, maana tulikuwa tunayafuata kule eneo la Manzese, mpaka mtu akayapate ilibidi ajidamke mapema ukifika pale saa mbili asubuhi unarudi saa nane ndiyo nyumbani wapate maji, kwa kweli tunashukuru sana,” alieleza Maganga.

Naye mkazi mwingine mkazi wa kijiji na Kata ya Ngogwa, Martha Mayila Kisandu alisema ujio wa maji kutoka Ziwa Victoria umeonesha wazi utekelezwaji wa ahadi ya Rais Dkt. Magufuli ya kuwatua ndoo vichwani akina mama ambapo anasema kabla ya maji hayo kutoka Ziwa Victoria walikuwa wanahangaika sana kutafuta maji ya matumizi yao ya kila siku.

“Tunashukuru mno, mno kwa kweli kwa mradi huu, serikali hii ya awamu ya tano imetukomboa wanawake, tunashukuru na tunasema ahsante, tulikuwa tunahangaika sana juu ya suala la maji, tulilazimika kuamka usiku kwenda kusaka maji, lakini sasa kero hii ipo mbioni kutuondokea, tunamshukuru Rais Magufuli,” alieleza Mayila.

Awali katika taarifa yake kwa wajumbe wa Bodi ya Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Manispaa ya Shinyanga (SHUWASA), Meneja wa mradi wa Maji Ngogwa – Kitwana, Mhandisi Yusuph Katopola alisema mradi huo kwa sasa unatarajiwa kutumia kiasi cha shilingi milioni 350 kwa ujenzi wa matanki mawili.

Katopola alisema mradi huo unahusisha ujenzi matanki mawili katika maeneo ya Ngogwa na Kitwana na kwamba umelenga kunufaisha watu wapatao 44,618 hadi kufikia mwaka 2033 miaka 15 tangu sasa ambapo tanki la Ngogwa litakuwa na ujazo wa lita za ujazo 680,000 na lile la Kitwana lita 135,000 ikiwemo kujenga mabirika ya kunyweshea mifugo.

“Mradi huu awali ulikadiriwa kutumia kiasi cha zaidi ya shilingi milioni 650 iwapo ungetekelezwa na wakandarasi wa ujenzi, lakini kwa hivi sasa kwa vile tumeamua kutumia wataalamu wetu wa ndani, tunakadiria ujenzi huu utatumia siyo zaidi ya shilingi milioni 350 kwa matenki yote mawili,” alieleza Katopola.

Meneja huyo alifafanua kuwa Serikali iliiteua SHUWASA kusimamia ujenzi wa mradi huo kwa vile ndiyo Mamlaka ya Maji ya Mkoa ambapo baada ya kukamilika kwa mradi, Mamlaka ya Maji ya Mji wa Kahama (KUWASA) ndiyo itakayoendelea kusimamia mradi huo.

Katika taarifa yake Mhandisi Magige Marwa, ambaye ni Mhandisi wa Mipango na Ujenzi katika Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa mazingira Kahama (KUWASA) alisema mradi huo umegawanyika katika sehemu tatu, ambazo ni ujenzi wa matanki mawili ya Ngogwa na Kitwana.

“Sehemu ya pili na ya tatu ni kuunganisha bomba kutoka katika matenki na ya tatu kujenga maeneo ya kusambaza maji pamoja na vituo vya kuchotea maji katika vijiji vyote vilivyopo katika kata za Ngogwa na Busoka na kazi kwa sasa inakwenda vizuri baada ya mvua kusimama ambazo zilitukwamisha kidogo,” alieleza Marwa.

Akizungumzia utekelezaji wa mradi huo, Mkurugenzi wa SHUWASA, Flaviana Kifizi alisema mamlaka yake ilikabidhiwa na wizara jukumu la kusimamia mradi huo wa ujenzi wa matanki mawili ya Ngogwa na Kitwana na kwamba hakuna changamoto kubwa zilizojitokeza katika utekelezaji wa mradi huo.

“Nichukue fursa hii kuwapongeza wananchi wa maeneo haya kwa jinsi walivyoupokea mradi, hatukupata matatizo yoyote kama inavyotokea katika maeneo mengine, tunawashukuru sana wananchi wa maeneo haya, mbali ya kupokea mradi lakini pia wameshiriki katika kufanya kazi ya ujenzi wa matanki haya,”

“Niendelee kuwaomba tu wananchi wa maeneo haya kwamba kwa vile bomba zimeisha wasili, tunawaomba wakati kazi ya kuzilaza itakapoanza wajitokeze kwa wingi kushiriki katika kazi hiyo ili mradi uweze kukamilika na kuanza kutoa huduma kwa wakati,” alieleza Kifizi.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya SHUWASA, Mwamvua Jilumbi alisema utekelezaji wa mradi huo upo katika hatua nzuri ukiachilia mbali changamoto za awali za mvua zilizosabisha kazi kusimama kwa muda na kwamba kwa kasi aliyoiona anaamini mradi utakamilika katika muda uliopangwa.
Wajumbe wa Bodi ya SHUWASA, kutoka kushoto, John Kisandu, Albert Msovela na Mhandisi Luhanyula Christopher wakiangalia kazi ya ujenzi wa tenki la maji katika eneo la Kitwana ambalo ni moja ya matenki mawili yanayojengwa chini ya Mradi wa Maji wa Ngogwa - Kitwana unaosimamiwa na SHUWASA.
Mjumbe wa Bodi ya SHUWASA, ambaye pia ni Katibu Tawala mkoani Shinyanga, Albert Msovela akikagua maendeleo ya ujenzi wa tenki la maji katika eneo la kata ya Ngogwa.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Shinyanga, Albert Msovela na Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga, John Kisandu ambao ni wajumbe wa Bodi ya SHUWASA wakiteremka kutoka katika kukagua ujenzi wa tenki la Maji linalojengwa eneo la Kitwana wilayani Kahama.
Baadhi ya wajumbe wa Bodi ya SHUWASA wakikagua ujenzi wa tenki lililopo eneo la kijiji na kata ya Ngogwa, tenki hilo linatarajiwa kuwa na ujazo wa maji lita 680,000.
Baadhi ya wajumbe wa Bodi ya SHUWASA wakikagua ujenzi wa tenki lililopo eneo la kijiji na kata ya Ngogwa, tenki hilo linatarajiwa kuwa na ujazo wa maji lita 680,000.
Wajumbe wa Bodi ya SHUWASA wakiwa katika picha ya pamoja mara baada ya kukagua kazi za ujenzi wa tenki la maji katika kata ya Ngogwa, wa kwanza kutoka kulia ni Mkurugenzi wa SHUWASA, Flaviana Kifizi, mjumbe, Albert Msovela, Mwenyekiti wa Bodi Mwamvua Jilumbi na John Kisandu.
Mkurugenzi wa SHUWASA, Flaviana Kifizi (wa pili kutoka kulia) akisikiliza maelekezo kutoka kwa mmoja wa wajumbe wa Bodi ya SHUWASA, Albert Msovela (wa kwanza kulia).
Afisa Mahusiano wa SHUWASA, Nsianel Gelard (kulia) na mmoja wa watumishi wa SHUWASA wakitoka eneo la mradi wa ujenzi wa Maji wa Ngogwa - Kitwana wilayani Kahama, hapa ni katika eneo la tenki la Ngogwa.
Sehemu ya mabomba yatakayotumika katika kupeleka maji kwenye matenki ya Ngongwa na Kitwana yakiwa yanateremshwa kutoka jijini Dar es Salaam, mabomba hayo yametengenezwa kwa chuma kizito na kila moja lina uzito wa kilo 160.
Wajumbe wakipata maelezo kutoka kwa mmoja wa wafanyakazi wa KUWASA (hayupo pichani) juu ya njia itakayolazwa mabomba ya maji kutoka kwenye bomba kuu linalotoka Solwa wilayani Shinyanga kwenda kwenye tenki la Ngongwa ambalo litateremsha maji yake kwenda kwenye tenki dogo la Kitwana.
 Wajumbe wa Bodi ya SHUWASA wakisikiliza maelezo juu ya utekelezaji wa Mradi wa Maji wa Ngogwa - Kitwana unaotarajiwa kutoa huduma ya maji kwa wakazi wa kata za Ngogwa na Busoka kutoka kwa Meneja wa Mradi, Yusuph Katopola (aliyesimama katikati). Mwenye gauni la bluu na mtandio mweupe ni Mwenyekiti wa Bodi, Mwamvua Jilumbi.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527