SERIKALI YATAJA SABABU ZA SUKARI KUADIMIKA NCHINI


Serikali imetaja sababu tatu ambazo zimesababisha kuadimika kwa sukari nchini, huku ikitoa msimamo wake kuhusu bihaa hiyo muhimu.


Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga alisema bungeni jana kuwa sababu hizo ni ugonjwa wa corona, baadhi ya wanunuzi kuficha sukari, meli nyingi zimekuwa zikifaulisha mizigo kwenye meli nyingine hivyo kusababisha kuchelewa kufika kwa wakati nchini.

Hasunga alisema hayo jana bungeni, alipokuwa akiwasilisha bajeti ya wizara yake ya mwaka wa fedha 2020/21 jijini Dodoma, ambapo aliomba Bunge liwaidhibishie zaidi ya Sh bilioni 229.8.

Kutokana na hali hiyo, alisema kuwa ili kukabiliana na na changamoto ya ukosefu wa sukari, Serikali ilitoa vibali vya kuagiza sukari tani 40,000 kutoka nje ya nchi.

Alisema kikao cha pamoja na wawakilishi wa uzalishaji, Serikali na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) pamoja na Bodi ya Sukari chini ya usimamizi wa Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, walikubaliana kutokupandishwa kwa bei za sukari.

“Hata hivyo kumejitokeza kuchelewa kuingia nchini kutokana na Covid-19 , baadhi ya wanunuzi kuficha sukari imekuwa ni tatizo. Wizara kupitia Bodi ya Sukari ilifanya uchunguzi wa kina na kwa kutumia sheria ya tasnia ya sukari ilichukua hatua ya kutangaza bei elekezi ya jumla na rejareja katika mikoa yote ya Tanzania Bara kwa lengo la kukabiliana na wafanyabiashara wasio waaminifu.

“Sasa hivi ni kweli katika maeneo mbalimbali kuna upungufu wa Sukari, ni kutokana na meli nyingi zimekuwa zikifaulisha kwenye meli nyingine hivyo haiji kadri unavyotakiwa,” alisema Hasunga.

Hasunga alisema mpaka kufikia Mei 10 mwaka huu tani zilizokuwa zimewasili nchini ni 4,000 huku tani 21,000 zikitarajiwa kuwasili mwezi huu.

“Tani 500 zimetoka Afrika ya Kusini zimeshafika hivyo hatutegemei kuwa na upungufu wa sukari, mahitaji ni tani 35,000 kwa mwezi hivyo ilivyoingizwa ni tani 40,000 na waliamini itatosha maana viwanda ilikuwa vianze uzalishaji Mei mwishoni.

“Lakini kutokana na mvua kuendelea kunyesha na kiwanda kimoja tu kimeonyesha dalili ya kuanza uzalishaji mwisho wa mwezi,” alisema Hasunga.

Aidha Waziri huyo wa Kilimo, aliwatoa hofu Watanzania kwa kudai kwamba Sukari ipo ya kutosha.

“Niwahakikishie Watanzania kuwa Sukari iliyoingia na hatua zilizochukuliwa kwani sukari inatosha kabisa na hatuhitaji kuwa na upungufu. Niwaombe wenzangu wanaohusika wahakikishe sukari iliyofika wanaiotoa na kusimamia usambazaji katika mikoa yote nchini.

“Tumekokotoa bei ya sukari inayotoka nje mpaka inafika Dar es Dalaam ni Dola 350 (zaidi ya Sh 800,000), mpaka nchi za mbali kama Brazil ni dola 500 (zaidi ya Sh milioni moja) , tukikikokotoa kwa bei ya Tanzania Sukari haitakiwi kuzidi bei tulizotangaza,” alisema.

Waziri Hasunga alisema walikaa kikao na Waziri Mkuu na waagizaji wa Sukari nchini ambapo wagizaji hao walikubali kutopandisha bei ya sukari.

“Na tumekaa jana (juzi) chini ya Waziri Mkuu na waagizaji wa Sukari wametuahidi kabisa bei haitakiwi kupanda hivyo katika sukari inayokuja itauzwa kwa bei ile tuliyoizoea,” alisema.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post