NEC YAKUTANA VYAMA VYA SIASA KUJADILI NA KUPITISHA KANUNI NA MAADILI KWA UCHAGUZI MKUU 2020

Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imejizatiti na imejipanga kuhakikisha kuwa inatekeleza majukumu yake kwa mujibu wa Katiba, Sheria, Kanuni pamoja na kuzingatia masharti ya Kanuni za Maadili ya Uchaguzi.


Hayo yamesemwa jana  Jijini Dar es Salaam na Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi (NEC), Mhe.Jaji Semistocles Kaijage katika kikao na vyama vua Siasa na Wadau wengine wa Uchaguzi kujadili na kupitisha Maadili ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani ya Mwaka 2020.

Akizungumza katika kikao hicho Jaji Kaijage alisema kuwa NEC kwa kushirikiana na vyama vya Siasa na Serikali huandaa Maadili ya Uchaguzi kwa shabaha ya kuwa na Uchaguzi ulio huru, wa haki, wa wazi na wa kuaminika.

“Maadili yatasaidia kuwa na uwanja sawa wa ushindani katika Uchaguzi.Maadili hayo huandaliwa kwa mujibu wa kifungu Cha 124A Cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, Sura ya 343 ya sheria za Tanzania kwa kuzingatia mahitaji yaliyopo”. Alisema Jaji Kaijage.

Jaji amesema kuwa ni muda mwafaka tena kwa vyama vya siasa, Tume na Serikali kama wadau wa Uchaguzi kuandaa Maadili hayo kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020.

“Natambua kuwa vyama na Serikali mlipewa Rasimu ya Maadili ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani ya mwaka 2020 ambapo mlipata fursa ya kupitia na kutoa maoni na mapendekezo yenu ambayo yamezingatiwa katika Rasimu hii ya Maadili”. Alisema Jaji Kaijage.

Pamoja na hayo Mhe.Kaijage aliwaaomba Wadau mbalimbali wa Uchaguzi baada ya majadiliano hayo na kuridhiwa kwa Maadili,wahusika wataweka saini ya kuyakubali, kuyaheshimu na kuyatekeleza kuanzia wakati was kampeni za Uchaguzi Mkuu wa Mwaka huu na chaguzi ndogo zitakazofuata.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post