AMUUA MKE WAKE KWA KUMKABA KABALI

Kamanda wa Polisi mkoani Rukwa, Justine Masejo

Na Israel Mwaisaka, Sumbawanga
JESHI la Polisi mkoani Rukwa linamshilia mwanaume mmoja(55), (jina limehifadhiwa) mkazi wa tarafa ya Kilyamatundu Wilayani Sumbawanga kwa tuhuma za kumkaba hadi kumuua mke wake Namsonga Bonifas(53) kutokana na kile kinachodaiwa kuwa ni mgogoro wa kifamilia.

Kamanda wa Polisi mkoani Rukwa, Justine Masejo amesema kuwa, tukio hilo lilitokea Mei 9, saa 2 asubuhi wakati wanandoa hao walopokuwa nyumbani kwao.

Imeelezwa kuwa, kabla ya tukio hilo wanandoa hao walirudi nyumbani usiku wakiwa wametoka kilabuni kunywa pombe na kisha wakaingia ndani ya nyumba yao kulala.

Asubuhi ya Mei 10, mmoja wa majirani hao alifika kwa lengo la kuwasalimia na kutaka kujua nini kilichotokea katika nyumba hiyo kwani usiku alisikia wanandoa hao wakizungumza kwa kujibizana maneno makali.

Baada ya kufika aligonga hodi na mtuhumiwa huyo aliitika lakini hakutoka nje hali iliyomlazimu jirani huyo kusukuma mlango na kuingia ndani ambapo alikuta mwili wa marehemu ukiwa umelala sakafuni na tayari amekwishafariki.

Alipoona tukio hilo, alitoa taarifa kwa uongozi wa Serikali ya Kijiji ambao nao walitoa taarifa polisi ambao walifika na kumkamata mtuhumiwa huyo ambaye kwa sasa bado wanaendelea na uchunguzi wa tukio hilo na utakapokamilika watamfikisha Mahakamani.
CHANZO - TIMES MAJIRA

Download/Pakua App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527