KENYA YAFUNGA MIPAKA YAKE KATI YA TANZANIA NA SOMALIA ILI KUKABILIANA NA CORONA


Kenya imefunga kwa muda wa siku 30 mipaka yake ya kimataifa kwenda Tanzania na Somalia kuanzia saa sita usiku wa Jumamosi Mei 16,2020.

Katika hotuba yake kwa taifa Rais Uhuru Kenyatta amesema hatua hiyo inajumuisha udhibiti usafiri wa watu kutoka mataifa hayo kuingia nchini Kenya.

Hata hivyo usafirishaji wa mizigo utaendelea kati ya Kenya na mataifa hayo mawili.

Marufuku hiyo ya kuzuia watu kutoka Tanzania na kuingia nchini Kenya inaanza usiku wa leo saa 6 na kuruhusu mizigo tu kupita. Na kwa upande wa Somalia masharti ni hayo hayo, mizigo peke yake ndio itaruhusiwa.

“Katika wiki moja iliyopita Maambukizi ya Watu 43 hapa Kenya yalikuwa ni kutoka nje ya Nchi, hii inaleta wasiwasi, tumeamua sasa kuanzia saa sita usiku wa leo tunafunga mipaka yetu ya Kenya-Tanzania na Kenya-Somalia, watakaoruhusiwa kuingia ni Madereva wa mizigo pekee”

Aidha madereva watakaoingia nchini Kenya kupeleka mizigo watatakiwa kupima corona kwanza.

Kenya imeongeza tena muda wa marufuku ya kutoka nje kwa muda wa siku 21.

Kufikia sasa idadi ya watu walioambukizwa  virusi vya corona nchini Kenya imeongezeka hadi 830 baada wagonjwa wapya 49 kuthibitishwa kuwa na ugonjwa huo.

Waliofariki kutokana na corona ni watu 50 baada ya wengine watano kufariki.

“Watu wengine watano wamefariki baada ya kuugua corona na kufanya idadi ya waliofariki na corona kufikia 50,  tuna wagonjwa wapya 49 pia na hii inafanya maambukizi ya corona kufikia 830 Kenya, wagonjwa 17 wamepona na kufanya waliopona kufikia 301”- Amesema Kenyatta


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527