RAIS MAGUFULI AONESHA NIA YA KUFUNGUA VYUO NA MICHEZO ...ASIMULIA MWANAE ALIVYOPONA CORONA


Rais Magufuli amesema kuanzia wiki ijayo kama maambukizi ya Corona yataendelea kupungua, atafikiria kufungua Vyuo na kuruhusu michezo iendelee.

Rais Magufuli ametoa kauli hiyo leo Jumapili Mei 17,2020 wakati akitoa salamu baada ya kushiriki kwenye Kanisa la KKKT Chato, mkoani Geita, ambapo atafikia uamuzi wa kurejesha michezo kwa kuwa michezo ni burudani kwa Watanzania. 

Rais Magufuli amesema kuwa "kwa trendi hii ninavyoiona kama wiki hii inayoanza kesho hali itaendelea kupungua nimepanga kufungua Vyuo ili wanafunzi waendelee kusoma, lakini pia tumepanga kuruhusu michezo iendelee."

Rais John Magufuli amesema kuwa idadi ya wagonjwa wa Corona nchini Tanzania imepungua sana, huku baadhi ya vituo vilivyotengwa kwa ajili ya kuwahudumia wenye maambukizi vikiwa vitupu.

Akitoa takwimu hizo Rais Magufuli amesema kwa Mkoa wa Dar es Salaam;

Amana ilikuwa inalaza wagonjwa 198 leo walikuwepo watu 12 walioathirika, Mloganzila walikuwa watu 30 leo 6, Kibaha huwa wanalazwa watu zaidi ya 50 leo wamebaki watu 22 ambao hali zao ni nzuri.

Akitaja vituo vingine amesema Aga Khan wamebaki watu 31, Hindu Mandali wamebaki 16, Regency 17, TMJ wamebaki 7, Rabininsia wamebaki 14.

Katika mikoa mingine amesema, Arusha kuna vituo vitatu, Moshono kuna wagonjwa 11, Longido na Karatu hakuna mgonjwa.

Mwanza kuna vituo 10 ambapo Buswelu kuna wagonjwa 2, Misungwi 2 Ukerewe, Magu, Mkuyuni, Bachosa, Sengerema, Kwemba kote hakuna mgonjwa, huku Hospitali ya Bungando na Sékou Touré kuna wagonjwa 2 wenye uhitaji maalum.

Dodoma kuna vituo vinne ambapo mjini viko viwili kuna wagonjwa wawili huku Kongwa na Kondoa kukiwa hakuna mgonjwa. 

Hizi ni baadhi ya kauli za Rais Magufuli leo

↠Mungu ametusaidia na kwa taarifa za leo wagonjwa wamepungua sana Amana ilikuwa inalaza Watu 198, leo walikuwepo Watu 12 tu, Mlogonzila ilikuwa inalaza Watu 30 leo wamebaki 6, pale Kibaha Hospitali ilikuwa inalaza zaidi ya Watu 50 leo wamebaki Watu 22.

↠Kwa hali hii, kama wiki tunayoianza kesho itaendelea hivi nimepanga kufungua vyuo ili Wanafunzi wetu waendelee kusoma, lakini nimepanga pia kuruhusu michezo iendelee kwasababu michezo ni sehemu ya Burudani, maisha lazima yaendelee.

↠Mimi Mtoto wangu wa kumzaa amepata corona akajifungia, akajifukiza akapiga malimao, sasa hivi ni mzima kabisa anapiga push-up, msije mkadhani mimi sijapata Mtu wa karibu mwenye corona, tuondoe hofu.

↠Sijaona umuhimu wa kufunga mipaka, juzi nimezungumza na Rais Museveni ametuuzia Tani za sukari Elfu 26, tungefunga mipaka tungepata hiyo sukari ya Uganda? , unakuta Dereva anazuiliwa sijui kwenda wapi? Wakati ametoka DSM hadi huko ametembea KM Elfu moja na kitu hajaanguka! 

↠Tanzania hakuna cha lockdown, wala Baba yake lockdown, wala Ndugu yake lockdown, tunaendelea kuchapa kazi wakimaliza kujilock huko watakuja tutawasaidia chakula, na tusiwabague, ndani ya Afrika Mashariki na SADC tuko pamoja lakini kila Mtu ana njia zake za kutatua tatizo”


↠Huwezi kuwa una mji wako halafu unapangiwa la kufanya, Mzee wetu wetu Kikwete alisema la kuambiwa changanya na lako, haiwezekani ukiambiwa jifungie,unajifungia chumbani wakati hauna chakula, tutaenda tunavyotaka, hili ni Taifa huru, Taifa linalojiamini, tumepambana na mengi.
Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527