DKT. KALEMANI : TANESCO KATENI UMEME KWA WADAIWA SUGU MUONGEZE MAPATO


Waziri wa Nishati Dkt. Medard Kalemani ameliagiza Shirika la Umeme nchini( TANESCO) kuendelea kukata umeme kwa wadaiwa sugu ili kukusanya mapato zaidi na kulipa madeni ya shirika hilo.

Dkt. Kalemani alisema hayo, Aprili 30, 2020, Jijini Dodoma, alipokutana na  Wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa TANESCO, kuzungumzia tathimini ya miaka mitano ya utekelezaji wa miradi mbalimbali, baada ya kufanya ziara ya kukagua ujenzi wa upanuzi wa kutuo cha kupoza na kuzambaza umeme cha Zuzu.

Katika kikao hicho, mambo mbalimbali yalijadiliwa kuhusiana na nishati ya umeme inayozalishwa nchini kwa lengo la kuleta manufaa makubwa zaidi kiuchumi kwa nchi, Shirika na watumiaji wa umeme huo ikiwemo viwanda, wafanyabiashara na matumizi mengine.

Dkt. Kalemani aliiagiza TANESCO, kulipa madeni yote inayodaiwa na kutoongeza madeni mapya, vilevile wadaiwa sugu wakumbushwe madeni yao,na endapo hatawalipa, TANESCO iwakatie umeme, kwa kufanya hivyo kutamaliza tatizo la wadaiwa sugu.

“TANESCO inadaiwa madeni makubwa, pia ina wateja wengi sana ambao ni wadaiwa sugu wanaodaiwa fedha nyingi sana na hawalipi ,zimo Taasisi, Mashirika ya Umma na binafsi, pamoja na watumiaji wa kawaida, ninawaagiza nendeni mkawakatie umeme! narudia tena mkakate umeme! mkishaukata, wahusika watalipa na wataonyesha ushirikiano mkubwa, tofauti na kumdai kawaida tu”, alisema Dkt. Kalemani.

Kuhusu wizi na uhujumu wa miundombinu ya umeme, Dkt. Kalemani, aliitaka TANESCO, Bodi ya TANESCO na Watendaji wa Wizara ya Nishati, kushirikiana kwa pamoja kutafuta njia sahihi naya kisasa zaidi  ya kubaini wizi wa umeme,unaofanywa na watu wasiowaaminifu na kusababisha hasara kwa shirika na kupoteza mapato ya taifa.

“Wizi wa umeme upo na haukubaliki, tuweke mfumo sahihi wa kisasa kubaini wahusika, tuache na hii tabia ya kukimbizana kimbizana na wezi, pia sisi watumishi tuwe wazalendo,na wasimamizi wazuri wa miundombinu yetu,vilevile tuwe na walinzi wenye weledi katika miradi yetu bila kujali niya serikali au mtu binafsi, jukumu la ulinzi ni letu sote faida ya Taifa kwa jumla”,alisisitiza Dkt. Kalemani.

Aidha aliwataka kuendelea kufanya tathmini na uwiano wa gharama za kutengeneza nguzo za Zege na nguzo zinazotumika sasa,ili kuangalia uwezekano wa kutumia nguzo za zege katika maeneo yote nchini lakini kwa gharama nafuu, kwa lengo la kukabiliana na changamoto ya kuoza ama kuungua kwa nguzo katika maeneo mbalimbali.

Hata hivyo aliweka wazi kuwa katika baadhi ya maeneo machache ambayo ni korofi nguzo za zege zimeanza kutumika japo ni za gharama kubwa.

Vilevile alitaka kuongezeka kwa idadi ya wateja wa umeme katika kila sekta, kuharakisha uunganishaji wa umeme kwa mteja pale anapomaliza kulipia gharama husika, pamoja na kutatua changamoto za wateja kwa wakati sahihi ili kuvutia wateja wengi zaidi na kuondoa malalaliko.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu aliwataka TANESCO kuangalia uwezekano wa kutoa zawadi kubwa kwa wasamaria wema wanaotoa taarifa za siri kuhusu wanaohujumu na kuiba umeme tofauti na ile inayotolewa sasa, ambayo pia huchukuwa muda mrefu kuikabidhi kwa mhusika.

Mgalu alikitaka  kitengo husika kitunza siri za watoa taarifa,pia kifanye uchunguzi wa kina na kutoa adhabu kwa mtumishi yeyote atakayetiliwa shaka, au kuhusika na wizi pamoja na kuhujumu miundombinu ya umeme kama inavyofanywa kwa wahisika wengine wanaobainika.

Vilevile kuwe na uhamasishaji wa kuwavutia watoa taarifa ili kupata matokeo chanya kunusu wizi na uhujumu wa miundombinu ya umeme nchini.

Naye Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Mhandisi Zena Said, alieleza kuwa ili kukabiliana na changamoto ya wizi na uhujumu wa miundombinu ya umeme, watashirikiana na Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa,(TAMISEMI) kuimarisha ulinzi kuanzia ngazi za Kaya.

Mhandisi Said, alisema kwa kufanya hivyo kutasaidia sana kubaini wezi na wahujumu miundombinu ya umeme kwa kuwa watu hao wasio wazalendo huwa wanaoneka na hata kufahamika katika maeneo yao.

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa TANESCO, Dkt. Alexander Kyaruzi, aliishuruku Wizara ya Nishati kwa kuwapa ushirikiano mkubwa katika kutekeleza majukumu yao na kuyafanyia kazi yale waliokuwa wakiishauri wizara hiyo, katika kipindi chote cha miaka mitano

Dkt.Kiyarunzi, alikiri kwa kuwa kazi ya kusambaza umeme si jambo jepesi, hivyo wanajivunia kuona maendeleo makubwa katika sekta ya nishati ya kuongeza wigo wa usambazaji wa umeme vijijini, kujenga miradi mikubwa ya kuzalisha, njia za kusafirisha na kusambaza umeme pamoja na vituo vya kupoza na kusambaza umeme nchini.

Awali kabla ya kufanyika kwa kikao hicho, Uongozi wa Wizara na Wajumbe wa Bodi hiyo walifanya ziara ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa upanuzi wa Kituo kikubwa zaidi nchini cha Kupoza na kusambaza umeme cha Zuzu kilichopo jijini Dodoma.

Kwa mujibu wa Dkt. Kalemani, ujenzi wa kituo hicho utakamilika mwishoni mwa mwezi huu wa Mei, 2020 na kitakuwa na uwezo wa kuzalisha Megawati 648 tofauti na vituo vingine.

Na kituo hicho kitaimarisha upatikanaji wa umeme kwa Jijiji la Dodoma ambalo linaendelea kukuwa kwa kasi na  kitakuwa ndiyo kitovu cha vituo vyote vya kupoza kuzambaza umeme katika mikoa yote nchini na kuupeleka nchi jirani pale itakapohitajika kufanya hivyo.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post