SHIRIKA LA DOCTORS WITH AFRICA LATOA ELIMU YA CORONA KWA WATOA HUDUMA ZA AFYA NGAZI YA JAMII SHINYANGA



 Mganga Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Dr. Yudas Ndungile akisisitiza jambo kwa washiriki wa mafunzo ya namna ya utoaji wa elimu na  kukabiliana na ugonjwa wa Corona.

Na Damian Masyenene - Shinyanga Press Club Blog

JUMLA ya watoa huduma za Afya  ngazi ya jamii 109  kutoka Wilaya ya Shinyanga Mkoani Shinyangawamepewa mafunzo na  mbinu mbalimbali za namna ya kukabiliana na homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona (COVID-19).

Mafunzo hayo yametolewa kwa watoa huduma hao 53 kutoka halmashauri ya Shinyanga na 56 kutoka Manispaa hiyo yakiratibiwa na Shirika la Doctors with Africa /CUAMM kwa kushirikiana na Serikali pamoja na idara ya afya mkoa wa Shinyanga.

Akifungua mafunzo hayo ya Siku tatu kwa watoa huduma za Afya ngazi ya jamii 53 kutoka halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga yaliyofanyika leo Mei 23 katika ukumbi wa Liga Hotel iliyopo Mjini Shinyanga, Mganga Mkuu wa Mkoa huo (RMO), Dk. Yudas Ndungile amewataka wahudumua hao kupeleka  taarifa na elimu kwa jamii kwa kutumia mbinu mbalimbali na siyo kukariri kwenda nyumba kwa nyumba
.
Dk. Ndungile amesema taifa liko kwenye kipindi cha kutekeleza na kuendeleza mapambano dhidi ya Corona hivyo wadau wasilale na kubweteka.

“Tuko hapa kuelezana wajibu wetu katika mapambano dhidi ya Corona na nini tunatakiwa kufanya katika maeneo yetu, tuwe wabunifu tunapokuwa tunatekeleza majukumu yetu kwa mbinu mbalimbali siyo lazima mpite nyumba kwa nyumba tusome kwanza mazingira ya maeneo yetu na tufanye kazi kwa kushirikiana na maofisa afya, watendaji wa kata,vijiji na viongozi wa wafanyabiashara katika maeneo ya minada, masoko, nyumba na vibanda vya kukatisha tiketi,” amesema Dk. Ndungile.

Katika hatua nyingine, Dk. Ndungile amewataka wadau na wataalam wa afya kuhakikisha kwamba wanaendelea kuwaelimisha na kuwasisitiza wananchi kuendelea kupata huduma na matibabu katika magonjwa mengine huku wakiendelea  kuchukua tahadhari dhidi ya Covid 19.

“Mbali na Corona sisitizeni pia wagonjwa waendelee kwenda hospitali kupata matibabu mfano wajawazito kwenda kliniki, watoto wapate chanjo, wenye VVU, kifua kikuu na Malaria kwahiyo wadau warudi kazini wananchi waendelee kukumbushwa na kusisitizwa namna ya kufuata matibabu kwa tahadhari,” amesema.

Kwa upande wake Mratibu shughuli za kijamii mradi wa upimaji na matibabu kutoka Shirika la Doctors with Africa/ CUAMM, Gasaya Msira ameeleza kuwa kutokana na shughuli mbalimbali kuathiriwa na janga la Corona waliona umuhimu wa kushiriki kuisaidia jamii kupata elimu licha ya wao kujihusisha zaidi na masuala ya Virusi Vya Ukimwi (VVU).

Msira amesema kuwa mafunzo hayo ni sehemu ya kwanza ya  jitihada zao kwani wamepanga kuyafanya kuwa endelevu kulingana na miongozo itakayokuwa inatolewa na Wizara ya Afya kuhakikisha kuwa wanatoa taarifa kila inapohitajika na kuwa na uwezo mkubwa wa kuisaidia jamii.

“Tunapenda kuona wahudumu wengi zaidi wanafikiwa na mafunzo haya, tuko tayari kuendelea kupanua wigo na kuwafikia watoa huduma ngazi ya jamii wengi zaidi kwa sababu mbali na mafunzo tunawapa barakoa na tunashirikiana na mkoa kutoa vifaa kinga,” amesema Msira.

Msira ameongeza kuwa wao kama Shirika lisilo la kiserikali ni wajibu wao kuhakikihsa wanashirikiana na Serikali  katika Mapambano mbalimbali ndani ya sekta ya afya ili jamii iweze kuelimika sambamba na kuchukua tahadhari katika suala zima la Magonjwa yanayoikumba jamii.

Nao baadhi ya  washiriki ambao wamehudhuria mafunzo hayo, akiwemo Rafael Kamuli kutoka Kijiji cha Jomu Kata ya Tinde wamesema kuwa watayatumia mafunzo na elimu waliyoipata kuisaidia jamii inayowazunguka hasa  kwa kuzingatia kwamba maeneo yao kuna Shughuli mbalimbali za Kijamii ikiwemo, Minada,Masoko,biashara mbalimbali  hivyo mafunzo hayo ni muafaka kwa kuinusuru jamii yao.

Mafunzo hayo yameanza kutolewa Jumatano hadi Ijumaa kwa watoa huduma ngazi ya jamii 56 kutoka Manispaa ya Shinyanga  na kuendelea tena leo Mei 23 hadi Mei 25 kwa watoa huduma 53 kutoka halmashauri ya wilaya ya  Shinyanga ambao baada ya mafunzo hayo watakwenda kusaidia kutoa elimu na taarifa  kwa jamii.

Mganga Mkuu wa Mkoa huo (RMO), Dk. Yudas Ndungile Akifungua mafunzo kuhusu Corona kwa watoa huduma za Afya ngazi ya jamii 53 kutoka halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga yaliyofanyika leo Mei 23 katika ukumbi wa Liga Hotel iliyopo Mjini Shinyanga.

Washiriki wa mafunzo hayo wakimsikiliza Mganga Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Dkt. Yudas Ndungile

Mratibu wa shughuli za kijamii mradi wa upimaji na matibabu kutoka Shirika la Doctors with Africa(CUAMM),Bw. Gasaya Msira akizungumza wakati wa mafunzo hayo.


Mratibu wa Kijamii kutoka Doctors with Africa(CUAMM) Bi Hilder Maginga akitoa neno kwa Washiriki wa mafunzo.
Meneja Miradi wa Shirika la Doctors with Africa CUAMM Bi Veronica Censi anayemaliza muda wake wa utumishi nchini Tanzania akiwaaga washiriki wa Mafunzo hayo na kuwatakia Maisha mema.
Mratibu wa shughuli za kijamii mradi wa upimaji na matibabu kutoka Shirika la Doctors with Africa Bw Gasaya Msira  akitoa neno kwa washiriki wa Mafunzo wahudumu wa afya ngazi ya jamii toka halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga. 
Mratibu wa elimu ya Magonjwa ya mlipuko Mkoa wa Shinyanga,Mwita Thomas akiendelea kutoa elimu kwa washiriki.
Afisa Afya Mkoa wa Shinyanga Bi  Neema Simba akiendelea na utoaji wa elimu ya namna ya kukabiliana na Covid 19 kwa watoa huduma ngazi ya Jamii halmashauri ya wilaya ya Shinyanga.
Washiriki wakiendelea na Darasa 
 Baadhi ya Washirki wa Mafunzo wakiendelea kufuatilia kwa ukaribu toka kwa watoa elimu.
 Mwandishi wa habari wa Shinyanga Press Club Blog Damian Masyenene akimhoji mmoja wa Washiriki na kufahamu namna  watakavyokwenda kuisaidia jamii katika kipindi hiki cha Covidi 19.

  TAZAMA ZAIDI PICHA ZA MATUKIO MBALIMBALI WAKATI WA MAFUNZO HAYO.
 

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527