CORONA YASHUSHA MAPATO SEKTA YA UTALII TANZANIA


Kutokana na virusi vya corona vinavyoendelea kuisumbua dunia, Wizara ya Utalii na Maliasili imesema mapato katika sekta hiyo yameshuka kutoka Sh trilioni 2.6 zilizotarajiwa kukusanywa.


Pia taasisi zilizokadiriwa kukusanya zaidi ya Sh bilioni 132.1 zinatarajia kukusanya Sh bilioni 33.5 ikiwa ni anguko la asilimia 75.

Vilevile, Serikali imesema kama hali haitatulia hadi Oktoba, ajira za moja kwa moja katika sekta ya utalii zitashuka kutoka 623,000 hadi kufikia 146,000 na watalii watashuka kutoka 1,867,000 waliotarajiwa hadi 437,000.

Kauli hiyo ilitolewa bungeni jana na Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla wakati akiwasilisha bungeni makadirio ya mapato na matumizi ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2020/21.

Dk. Kigwangalla alisema sekta ya utalii imeathirika kwa kiwango kikubwa kutokana na corona.

Alisema wizara ilifanya tathmini ya awali (rapid assessment) iliyojikita katika kipindi cha tangu ugonjwa huo uanze hadi Aprili 6, mwaka huu.

Dk. Kigwangalla alisema tathmini hiyo ilibaini kuwa madhara makubwa ya corona katika sekta ya utalii yalianza kuonekana mwanzoni mwa Machi, tofauti na Februari na Januari, mwaka huu ambapo hali ilikuwa shwari. Alisema tathmini ilibaini mashirika 13 ya ndege yalisitisha safari za kuja nchini tangu Machi 25, mwaka huu hivyo kuondoa uwezekano wa kuendelea kupata watalii kutoka nje ya nchi.

Dk. Kigwangalla alisema mashirika yaliyositisha safari zake ni pamoja ni Emirates, Swiss, Oman Air, Turkish, Egyptian Air, South African Airways, Rwandair, Qatar, Kenya Airways, Uganda Airlines, Fly Dubai na KLM

Alisema NCAA ilikadiria kukusanya Sh bilioni 162.7, kwa sasa itakusanya Sh bilioni 58, TFS ilikadiria Sh bilioni 153.6, sasa ni Sh bilioni 121 na Tawa ilikadiria Sh bilioni 58.1 sasa ni Sh bilioni 22.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527