WANANCHI WAASWA KUTOCHOKA KUSAFISHA MIKONO KWA SABUNI NA MAJI SAFI YANAYOTIRIRIKA ILI KUKABILIANA NA VIRUSI VYA CORONA

Na WAMJW- Tunduma Songwe

Kaimu Meneja wa forodha Mikoa ya Songwe na Mbeya Ndg. Anangisye Mtafya amewataka Wasafiri na wafanya biashara wa maeneo ya mipakani kutochoka kusafisha mikono kwa sabuni na maji safi yanayotiririka wakati wote ili kujikinga dhidi ya maambukizi ya homa kali ya mapafu inayosababishwa na virusi vya Corona.

Ameyasema hayo leo wakati akipokea vifaa vya kunawia mikono vilivyo tolewa na Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Wadau wa Project CLEAR katika ofisi za forodha zilizo katika mpaka wa Tanzania na Zambia Tunduma Songwe.

“Kunawa mikono ndio silaha yetu kubwa, ambayo tunajivunia, maji safi yanayotiririka na sabuni ndio silaha kubwa, nawa ukiwa nyumbani, nawa ukiwa katika biashara zako, nawa ukiwa kazini, nawa nawa nawa,” alisema

Aliendelea kusisitiza kuwa, baadhi ya silaha za kukabiliana na maambukizi ya ugonjwa huu haziitaji pesa nyingi ili kupambana nao, huku akisisitiza watu kuacha tabia za kusalimiana kwa kushikana mikono katika maeneo yote ya kazi, mtaani na majumbani.

Kwa upande wake Mkuu wa Kitengo cha maji na usafi wa mazingira kutoka Wizara ya Afya, Ndg. Anyitike Mwakitalima ameeleza kuwa, zaidi ya watu 121,000/ wamepoteza maisha kutokana na maambukizi ya homa kali ya mapafu inayosababishwa na virusi vya Corona, na kuweka wazi kuwa zaidi ya watu 1,900,000/ wakiwa na maambukizi ya ugonjwa huo.

“Zaidi ya watu 1,900,000 Duniani wameambukizwa na virusi hatari vya Corona, na kati ya hao watu 121,000 wamepoteza maisha, huu ni ugonjwa ambao unaua kwa idadi kubwa sana, toka tuanze karne ya hii ya 21 hakuna ugonjwa ambao umeua watu wengi kwa muda mfupi kama Corona ” alisema

Aliendelea kusema kuwa, Wataalamu wa masuala ya Afya wanashauri kuwa, kila mtu ahakikishe anasafisha mikono angalau sio chini ya mara 14 kila siku, ili kuviangamiza virusi vya ugonjwa wa Corona endapo vitakuwa katika mikono muda wowote.

“Tunasema angalau katika siku moja, unawe mikono yako sio chini ya mara 14, hii itasaidia kuacha mikono yako safi na salama muda wote” alisema

Nae Balozi wa kampeni ya Mikoni safi, Tanzania salama, Msanii Mrisho Mpoto (Mjomba) amesisitiza juu ya ushirikiano baina ya Serikali na raia wote katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa Corona, huku akiwaasa wananchi kufuata maelekezo yanayotolewa na Serikali katika kujikinga, ikiwemo kuepuka msongamano maeneo yote, kunawa mikono kwa sabuni na maji safi yanayotiririka.

Uhamasishaji huu unafanywa kupitia kampeni hii ya “Mikono safi, Tanzania salama” inaratibiwa na Wizara ya Afya, kwa kushirikiana na Shirika lisilo la kiserikali la Project CLEAR kwa kushirikiana na Msanii Mrisho Mpoto (Mjomba) kutoka Mjomba Theatre Gallery unaendelea katika Mkoa wa Songwe, kisha kuelekea Mkoa wa Rukwa.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post