TUME YA KUREKEBISHA SHERIA YAKABIDHI TAARIFA KUHUSU MAPITIO YA SHERIA ZINAZOSIMAMIA UTATUZI WA MIGOGORO YA ARDHI

Na Munir Shemweta, WANMM DODOMA

Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania imekabidhi Taarifa ya Mapitio ya Sheria Zinazosimammia Utatuzi wa Migogoro ya Ardhi nchini kwa Waziri wa Katiba ba Sheria Dkt  Balozi Augustine Mahiga.

Taarifa hiyo imekabidhiwa kufuatia Tume ya Kurekebisha Sheria kufanya utafiti baada ya kupokea maelekezo ya Wizara ya Katiba na Sheria yakitaka kupitia Mfumo wa Utatuzi wa Migogoro ya Ardhi Tanzania.

Makabidhiano hayo yamefanyika leo tarehe 20 Aprili 2020 katika ofisi za Wizara ya Katiba na Sheria zilizopo Mji wa Serikali eneo la Mtumba jijini Dodoma ambapo Mwenyekiti wa Tume ya Kurekebisha Sheria Jaji Mstaafu Januari Msofe alimkabidhi Waziri wa Katiba na Sheria Dkt  Balozi Augustine Mahiga.

Akielezea Utafiti wa Mapitio ya Sheria hiyo wakati wa makabidhaino ya Taarifa hiyo, Jaji Mstaafu Msofe alisema, katika kukamilisha mapitio ya sheria hiyo Tume ilikusanya maoni ya wadau mbalimbali kwenye mikoa ya Shinyanga, Mwanza, Tanga, Kilimanjaro, Arusha, Dodoma, Iringa , Mbeya , Songwe na Dar es Salaaam.

‘’Baada ya Tume kukusanya maoni ya wadau wakiwemo Majaji, Mawakili, Wasajili wa Mabaraza ya Ardhi, Wenyeviti wa Mabaraza  na  Wajumbe wa Kata na Wazee wa Mabaraza  Tume imebaini changamoto mbalimbali  zilizosababisha kutofikiwa malengo yaliyokusudiwa  ambayo ni mfumo wa utatuzi wa migogoro ya ardhi  wa haraka , haki  na unaofikika kwa urahisi’’ alisema Jaji Mstaafu Msofe.

Alizitaja baadhi ya changamoto kuwa ni pamoja na Mamlaka za Kipekee za Mahakama za Ardhi ambazo utafiti wake ulionesha lengo kutofikiwa kutokana na kukosekana rasilimali fedha, watu na vitendea kazi sambamba na idadi ndogo ya mabaraza ya ardhi na nyumba ya wilaya.

Aidha, Mwenyekiti wa Tume, ameeleza Uhuru wa Mahakama za Ardhi kuwa ni changamoto yenye kasoro kutokana na baadhi ya mahakama hizo kuwa chini ya mhimili wa serikali  na kutolea mfano wa Mabaraza ya  Ardhi ya Vijiji, Kata na Wilaya.

Hata hivyo, Jaji Mstaafu Msofe amezitaja changamoto nyingine kuwa ni kufikika kwa mabaraza ya kata na ya wilaya, Ada zitolewazo na mahakama za ardhi, lugha inayotumika kwenye mahakama za ardhi, vigezo vya wajumbe wa baraza la ardhi  la kijiji na kata, Uharaka katika kusikiliza na kuamua mashauri, Wazee wa Baraza katika mabaraza ya nyumba ya wilaya, miongozo katika utatuzi migogoro, utozaji ushuru wa hati za madai ya gharama na muongozo wa mwenendo wa maadili ya wajumbe wa mabaraza ya ardhi ya kijiji na mabaraza ya kata.

Kwa upande wake waziri wa Katiba na Sheria Dkt Balozi Augustine Mahiga aliipongeza Tume ya Kurekebisha sheria kwa kutekeleza kazi ya utafiti kuhusiana na sheria ya utatuzi wa migogoro ya ardhi na kubainisha kuwa kazi hiyo ni moja ya masuala mengi ambayo Tume inatakiwa kuyafanyia kazi huku Tume hiyo ikiwa na mzigo mkubwa wa kazi mbalimbali za mapitio ya sheria.

‘’Kama kuna sehemu ambayo Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania inahitaji msaada basi ni katika eneo la Mapitio mbalimbali ya sheria ambazo nyingi zimepitwa na wakati na zinahitaji kupitiwa upya’’ alisema Dkt. Balozi Mahiga.

Naye Katibu Mkuu wa Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania Casmir Kyuki alisema kati ya ripoti ambazo tume imezifanyia kazi , Ripoti ya Utafiti Kuhusiana na Mapitio ya Sheria Zinazosimamia Utatuzi wa Migogoro ya Ardhi imefanyika kwa haraka na kasi kubwa kufuatia mhimu wa sheria yenyewe sambamba na kutekeleza matakwa ya sheria kama inavyoelekeza.

Utafiti uliofanywa na Tume ni utekelezaji wa majukumu yake kama yalivyoanishwa katika kifungu cha 4 (1), (2) na (4) cha Tume ya Kurekebisha Sheria kinachotamka kuwa jukumu kubwa la Tume ni kufanya Mapitio, Utafiti na Kutathmini maeneo yote ya sheria zote za Tanzania Bara na kutoa mapendekezo serikalini ya namna ya kuboresha sheria hizo ili ziakisi mabadiliko yanayotokea.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527