MASANJA MKANDAMIZAJI AITIKIA WITO WA DC NA KUOMBA MSAMAHA


Baada ya kupewa masaa 72 awe ameripoti kwa Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Patrobas Katambi hatimaye jana mchekeshaji Emmanuel Mgaya ‘Masanja’aliitikia wito na kuomba radhi kwa watanzania kutokana video clip yake ya mahojiano na wananchi juu ya Corona.DC Katambi alimpa Masanja siku tatu kuripoti ofisini kwake ili kuhojiwa na kueleza sababu ya yeye kurekodi kipindi chake akiwahoji wananchi wa Dodoma maana ya Covid19 jambo ambalo kwa mujibu wa Mkuu wa Wilaya lililenga kupotosha kwamba wananchi wake hawana uelewa na ugonjwa huo.

Kufuatia wito huo siku hiyo hiyo Masanja aliripoti ofisi ya DC na kuelekezwa kuja jana ambapo aliripoti na kuhojiwa na Kamati ya Usalama ya Wilaya hiyo aliomba msamaha na kuahidi kutumia nafasi yake kushirikiana na serikali katika mapambano dhidi ya ugonjwa huo wa Corona.

Akizungumza na wandishi wa habari baada ya kumaliza mahojiano, Masanja amempongeza DC Katambi kwa kuwa mwepesi wa kugundua kuwa kulikuwa na shida kwenye kipindi chake alichorusha jambo linaonesha kweli yeye ni kijana na anaenda na spidi ya Rais Magufuli katika kuwatumikia watanzania.

" Niombe radhi kwa kueleweka vibaya lengo la kipindi chetu lilikuwa kuelimisha na siyo kuleta mzaha, namshukuru Mkuu kwa wito wake huu ambao umenisaidia pia kwa namna moja ama nyingine kujua wapi nilipoteleza.

"Kama Taifa tunapita kwenye kipindi kigumu kutokana na maambukizi ya ugonjwa huu hivyo tuendelee kuchukua tahadhari zote kama tunavyoelekezwa na wataalamu wetu ili tuzidi kuwa salama," Alisema Masanja.

Mchekeshaji huyo ambaye pia ni Mchungaji amemuahidi DC Katambi kuwa atatumia kipawa chake cha kuhubiri pia kuhamasisha watanzania kutumia vitakasa mikono na kufuata masharti yote ambayo yanatolewa na viongozi.

Nae DC Katambi amesema hana tatizo binafsi na Masanja wala kituo cha DW ambacho muigizaji huyo anafanyia kazi bali walimuita kwa ajili ya kuwekana sawa.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post