Picha : DC MBONEKO AONGOZA KAMPENI YA KUHAMASISHA ULIPAJI KODI YA PANGO LA ARDHI KWA WADAIWA SUGU SHINYANGA


Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Mhe. Jasinta Mboneko ameongoza Kampeni ya Kuhamasisha Ulipaji wa Kodi ya Pango la Ardhi kwa wamiliki wa viwanja vya biashara na makazi katika manispaa ya Shinyanga inayoendeshwa na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi ili kutoa elimu ya ulipaji kodi na kufuatilia wadaiwa wenye madeni makubwa na malimbikizo ya muda mrefu.Kampeni hiyo imefanyika leo Alhamis Aprili 2,2020 ambapo Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Mhe. Jasinta akiwa ameambatana na Mkuu wa Kitengo cha Kodi Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Denis Masami,Kamishna Msaidizi wa Ardhi mkoa wa Shinyanga,Hezekiel Kitilya na Maafisa wa Idara ya Ardhi Manispaa ya Shinyanga amekutana na wafanyabiashara na wananchi wanaodaiwa Kodi ya Pango la Ardhi.


Miongoni mwa wafanyabiashara waliotembelewa leo ni Kiwanda cha Machinjio ya Punda cha Fang’ Wah kinachomilikiwa na Wawekezaji kutoka China kinachodaiwa shilingi Milioni 66,Kampuni ya Gaki Investment Ltd (Milioni 120), Phantom Oil Tanzania Ltd (Milioni 105) na Mwananchi Garage (Milioni 9.3).

Akizungumza, Mboneko alisema ni wajibu wa kila mmiliki wa ardhi kuhakikisha analipia kodi ya pango la ardhi hata kama hana hati ya ardhi akibainisha kuwa kutolipa kodi ya pango la ardhi ni kuiibia serikali hivyo kuchangia kudhorotesha maendeleo ya nchi.

“Msiidanganye serikali kwa sababu serikali ina macho makubwa, ina macho marefu itawafuata popote mlipo ili mlipe kodi.Ni lazima deni lilipwe.Tutahakikisha tunawafuatilia wale wote wanaodaiwa kwani kodi zinazokusanywa ndiyo zinatumika kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo nchini”,alisema Mboneko.

“Niwashukuru na kuwapongeza wafanyabiashara na wananchi tuliowafikia leo mmeonesha kutambua umuhimu wa kulipa kodi ya pango la ardhi na mmesema mpo tayari kulipa madeni yenu.Hakikisheni mnalipa madeni yenu kabla ya mwaka wa fedha haujaisha Juni,2020.Tutaendelea kutoa elimu zaidi kwa wananchi ili kuhakikisha kila mmoja analipa kodi ya ardhi anayodaiwa”,aliongeza Mboneko.

Kwa upande wao wafanyabiashara na wananchi wanaodaiwa kodi ya pango la ardhi wameishukuru serikali kuwatembelea na kuwakumbusha wajibu wao kulipa kodi huku wakibainisha kuwa wapo tayari kulipa madeni yao.

“Mimi sikujua kuwa ukiwa na kiwanja tu bila hati ya ardhi unatakiwa ulipie kodi ya pango la ardhi.Nilijua nikipata hati ndiyo naanza kulipia.Nimejipanga kuanza kulipa deni ninalodaiwa ambapo hadi mwisho mwezi huu wa Aprili nitakuwa nimemaliza kulipa deni”,alisema Polycarp Kimario ambaye ni Mkurugenzi wa Mwananchi Garage.

Kwa upande wake, Meneja wa Kiwanda cha Fang’ Wah, Alice Mingyang Yan alisema wapo tayari kulipa deni lao wanalodaiwa kuanzia mwaka 2018 hadi mwaka 2020 muda ambao wamekuwa wakifanya shughuli zao badala ya kudaiwa kuanzia mwaka 2013 kipindi ambacho kulikuwa na wawekezaji wengine waliouza kiwanja.

Naye Mkurugenzi wa Kampuni ya Gaki Investment Ltd, Gasper Kileo alisema anatambua umuhimu wa kulipa kodi na tayari alishaanza kulipa deni analodaiwa akibainisha kuwa awali alikuwa anadaiwa shilingi Milioni 30 lakini deni lake limekuwa likiongezeka kutokana na mgogoro wa ardhi uliokuwepo katika kiwanja chake kilichopo eneo la Matanda.

Mkuu wa Kitengo cha Kodi Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Denis Masami alisema lengo la Kampeni ya Kuhamasisha Ulipaji wa Kodi ya Pango la Ardhi kwa wamiliki wa viwanja vya Biashara na makazi inayoendeshwa katika mikoa mbalimbali ni kutoa elimu ya ulipaji kodi ya pango la ardhi na kufuatilia wadaiwa wenye madeni makubwa na malimbikizo ya muda mrefu.

“Kampeni hii pia inalenga kutatua changamoto zinazowakabili walipa kodi na kuchukua hatua za kisheria kwa kusambaza hati za madai ili kuwafikisha mahakamani watakaokaidi tutawakamata mali na kuuza ili kufidia deni husika”,alisema Masami.
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Mhe. Jasinta Mboneko (kulia) akitoa elimu ya ulipaji kodi ya pango la ardhi kwa Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Kampuni ya Phantom Oil Tanzania Ltd  John Maguru (kushoto) inayodaiwa shilingi milioni 105 za pango la ardhi tangu mwaka 2007 leo Alhamis Aprili 2,2020 wakati akiongoza Kampeni ya Kuhamasisha Ulipaji wa Kodi ya Pango la Ardhi kwa wamiliki wa viwanja vya Biashara na makazi katika manispaa ya Shinyanga. Wa pili kushoto ni Mkuu wa Idara ya Ardhi na Mipango Mji Manispaa ya Shinyanga,Salu Ndongo akifuatiwa na Mkuu wa Kitengo cha Kodi Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Denis Masami. Picha zote na Kadama Malunde - Malunde 1 blog.
Kushoto ni Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Kampuni ya Phantom Oil Tanzania Ltd  John Maguru akimuahidi Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Mhe. Jasinta Mboneko kuwa Kampuni yao ipo tayari kuanza kulipa kodi ya pango la ardhi.
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Mhe. Jasinta Mboneko akiendelea kutoa elimu ya ulipaji wa kodi ya pango la ardhi. Kulia ni Kamishna Msaidizi wa Ardhi mkoa wa Shinyanga,Hezekiel Kitilya.
Mkuu wa Kitengo cha Kodi Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Denis Masami (katikati) akielezea hatua zinazochukuliwa na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa wafanyabiashara na wananchi wasiolipa kodi ya pango la ardhi kuwa ni pamoja na kuchukua hatua za kisheria kwa kusambaza hati za madai ili kuwafikisha mahakamani watakaokaidi tutawakamata mali na kuuza ili kufidia deni husika.
Mkuu wa Idara ya Ardhi na Mipango Mji Manispaa ya Shinyanga,Salu Ndongo (wa pili kushoto) akitoa elimu ya ulipaji kodi ya pango la ardhi.
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Mhe. Jasinta Mboneko akipokelewa na Meneja wa Kiwanda cha Machinjio ya Punda cha Fang’ Wah, Alice Mingyang Yan (kulia) alipotembelea kiwanda kicho kwa ajili ya kuhamasisha Ulipaji wa Kodi ya Pango la Ardhi kwa wamiliki kiwanda hicho kilichopo Ibadakuli katika manispaa ya Shinyanga.
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Mhe. Jasinta Mboneko akikagua nyaraka mbalimbali katika Kiwanda cha Machinjio ya Punda cha Fang’ Wah na kubaini kuwa Kiwanda hicho kinadaiwa shilingi milioni 66 za pango la ardhi tangu mwaka 2013 na kuwataka walipe deni hilo.
Wafanyakazi wa kiwanda cha Kiwanda cha Machinjio ya Punda cha Fang’ Wah wakijitetea mbele ya Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Mhe. Jasinta Mboneko kuwa wao walinunua kiwanda hicho mwaka 2018 kutoka kwa Mwekezaji Mwingine hivyo wapo tayari kuanza kulipa deni la kuanzia mwaka 2018 hadi 2020.
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Mhe. Jasinta Mboneko (kulia) akiwataka wamiliki wa kiwanda cha Fang’ Wah  kulipa kodi ya pango la ardhi.
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Mhe. Jasinta Mboneko akizungumza na waandishi wa habari katika Kiwanda cha Machinjio ya Punda cha  Fang’ Wah na kuhamasisha ulipaji wa kodi ya pango la ardhi.
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Mhe. Jasinta Mboneko akizungumza na waandishi wa habari katika Kiwanda cha Machinjio ya Punda cha  Fang’ Wah na kuhamasisha ulipaji wa kodi ya pango la ardhi.
Mkuu wa Kitengo cha Kodi Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Denis Masami akizungumza na waandishi wa habari katika Kiwanda cha Machinjio ya Punda cha  Fang’ Wah na kuhamasisha ulipaji wa kodi ya pango la ardhi.
Kushoto ni Mkuu wa Kitengo cha Kodi Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Denis Masami akitoa elimu ya ulipaji kodi ya pango la ardhi kwa Mkurugenzi wa Kampuni ya Gaki Investment Ltd, Gasper Kileo (wa pili kulia) ambaye pia anadaiwa deni la shilingi milioni 120 kwa ajili ya pango la ardhi katika kiwanja chake  kilichopo katika eneo la Matanda.
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Mhe. Jasinta Mboneko akimhamasisha Mkurugenzi wa Kampuni ya Gaki Investment Ltd, Gasper Kileo kumalizia kulipa kodi ya pango la ardhi anayodaiwa.
Mkurugenzi wa Kampuni ya Gaki Investment Ltd, Gasper Kileo akielezea hatua alizochukua baada ya mgogoro wa ardhi kuisha katika viwanja vyake katika eneo la Matanda ambapo kwa kutambua umuhimu wa kulipa kodi tayari alishaanza kulipa deni analodaiwa.
Kulia ni Kamishna Msaidizi wa Ardhi mkoa wa Shinyanga,Hezekiel Kitilya akimueleza jambo Mkurugenzi wa Kampuni ya Gaki Investment Ltd, Gasper Kileo
Mkurugenzi wa Kampuni ya Gaki Investment Ltd, Gasper Kileo akimweleza jambo Kamishna Msaidizi wa Ardhi mkoa wa Shinyanga,Hezekiel Kitilya.
Kushoto ni Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Mhe. Jasinta Mboneko akitoa elimu ya ulipaji kodi ya pango la ardhi kwa Mkurugenzi wa Mwananchi Garage Polycarp Kimario (kulia) ambaye anadaiwa kodi ya shilingi milioni 9.3 katika kiwanja chake ambacho anakitumia kufuga samaki.
Kulia ni Mkurugenzi wa Mwananchi Garage Polycarp Kimario akimuahidi Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Mhe. Jasinta Mboneko kuwa atalipa kodi ya pango la ardhi mwezi huu Aprili 2020.
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Mhe. Jasinta Mboneko akiwahamasisha wamiliki wa ardhi kuhakikisha wanalipa kodi ya pango la ardhi.
Picha zote na Kadama Malunde - Malunde 1 blog

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post