WAZIRI MKUU AMSIMAMISHA KAZI MWEKA HAZINA KOROGWE NA MAAFISA WAWILI


WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amemsimamisha kazi Mweka Hazina wa Halmashauri ya Mji wa Korogwe, Subilaga Kapange pamoja na maafisa wengine wawili wanaosimamia ukusanyaji wa mapato katika kituo cha mabasi cha Korogwe baada ya kushindwa kuwasilisha mapato Serikalini.

“Mnakusanya fedha na kuziweka mfukoni hazipelekwi benki mnazitumia kwa matumizi yenu binafsi na kuna siku inaonesha hamjakusanya chochote, hatuwezi kuvumia hali hii hawa wote wakamatwe na wawekwe ndani na hii iwe funzo kwa waweka hazina wote nchini.”

Waziri Mkuu ameyasema hayo jana jioni (Alhamisi, Machi 5, 2020) wakati akizungumza na watumishi wa Halmashauri ya Mji wa Korogwe na wananchi kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika uwanja wa TTC Korogwe akiwa kwenye ziara ya kikazi mkoani Tanga. Maofisa wengine waliosimamishwa kazi ni Meneja wa kituo cha mabasi Majid Salehe na msaidizi wake Ismail.

Amesema Halmashauri hiyo ya Mji Korogwe imejenga kituo cha mabasi lakini makusanyo yake hayafikishwi Serikalini huku baadhi ya wazabuni waliopewa kazi hiyo wakiwa hawana hata mikataba jambo linalochangia Halmashauri hiyo kushindwa kufikia malengo ya ukusanyaji.  Hadi sasa imekusanya asilimia 36 tu.

“Kuna siku kituo kinakusanya sh 51, 000 tu licha ya mabasi mengi kupita, hata hivyo Februari 27, 2020 hawakukusanya kiasi chochote inamaana hakuna basi lililopita. Februari 28, 2020 walikusanya sh 785,000 na Februari 29, 2020 walikusanya mara mbili sh 500,000 na sh 990,000 lakini fedha zote hizo hazikupelekwa benki.”

“Baada ya kusikia nakuja Korogwe jana (Jumatano, Machi 4, 2020) walikusanya sh. milioni 11 na kuzipeleka benki na risiti ninazo, siku zote hakuna risiti kwa sababu fedha hazipelekwi benki na wakusanyaji wengine ni marafiki zao hivyo hata wasipokusanya hakuna wa kuwauliza.”

Waziri Mkuu amesema Serikali haiwezi kulea watumishi wa aina hiyo, hivyo amemuelekeza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Korogwe, Bw. Nocodemus Bei ahakikishe anakuwa makini katika kufuatilia zinakopelekwa fedha za mapato yanazokusanywa kwenye eneo lake.

Amesema Serikali inataka kila mtumishi wa umma nchini awajibike kwa kufanya kazi kwa bidii na kwamba Serikali ya Awamu ya Tano haitowavumilia watumishi ambao ni wezi, wabadhilifu, wavivu na haitosita kuwachukulia hatua.

Waziri Mkuu amewaeleza watumishi hao kuwa wanatakiwa wafanye kazi kwa kuzingatia sheria na kanuni za utumishi wa umma na pia watambue dhamana kubwa waliyonayo, ambayo ni kuwahudumia wananchi wote bila ya ubaguzi wa aina yoyote.

Pia, Waziri Mkuu amewataka Madiwani wa Halmashauri ya Mji wa Korogwe wahakikishe wanakuwa wakali katika usimamizi wa makusanyo ya mapato pamoja na matumizi yake.

Kwa uapande wake, Mkuu wa Tanga, Bw.Martine Shigela alisema kufuatia ubadhilifu wa fedha za makusanyo katika kituo cha mabasi Korogwe jana (Jumatano, Machi 4, 2020) aliagiza kukamatwa na kuwekwa ndani kwa Mweka Hazina.

Awali, Mbunge wa Korogwe Mjini, Mary Chatanda alimuomba Waziri Mkuu awasaidie kutatua tatizo la ubadhilifu wa fedha za mapato kwani wamejenga kituo kizuri cha mabasi lakini hakiwanufaishi. Amesema licha ya mabasi mengi kupita katika kituo hicho mapato wanayoyapa ni kidogo.

(mwisho)

IMETOLEWA NA
OFISI YA WAZIRI MKUU


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post