TANZANIA NI NCHI YA MFANO KATIKA KULINDA HAKI ZA WATU WENYE ULEMAVU WA NGOZI

Dodoma, 9 Machi 2020

Tanzania imetajwa kuwa ni nchi ya kupigiwa mfano na inayopaswa kuigwa kutokana na  mikakati mizuri iliyojiwekea katika kuboresha maisha ya watu wenye ulemavu wa ngozi.


Kauli hiyo imetolewa hivi karibuni na Mtaalam wa Kujitegemea anayeshughulikia haki za binadamu za watu wenye ulemavu wa ngozi, Bi. Ikponwosa Ero, alipowasilisha taarifa yake kwenye Kikao cha 43 cha Baraza la Haki za Binadamu kilichoanza mwishoni mwa mwezi Februari 2020 Geneva, Uswizi.

Bi. Ero alilieleza Baraza hilo kuwa hali ya haki za binadamu kwa watoto na wanawake wenye ulemavu wa ngozi katika maeneo mbalimbali duniani bado si nzuri. Hata hivyo, alisema kuwa kuna nchi ambazo zimefanya vizuri katika kuboresha haki za binadamu za wanawake na watoto wenye ulemavu wa ngozi na kuitaja Tanzania kuwa ni moja ya nchi hizo.

Mtaalamu huyo alianisha maeneo ambayo Tanzania imefanya vizuri kuwa ni pamoja na kuwa na mfumo mzuri wa ukusanyaji takwimu za watu wenye ulemavu wa ngozi na kuzitaka nchi nyingine ziige mfano huo wa Tanzania. Pia alieleza na kusifia Ibara ya 6 ya Katiba ya Baraza la Watoto (Junior Council) la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania linaloelezea hatua mahususi kwa ajili ya kuwajumuisha watoto wenye ulemavu katika michakato yake. 

Aidha, mtaalamu huyo alitoa mfano wa Kikundi cha Upendo wa Mama kilichoundwa kwa ajili ya kuwawezesha akinamama wenye ulemavu wa ngozi katika kujipatia kipato na kuelezea kuwa kikundi hicho kinatoa elimu ya kuwawezesha akinamama walemavu wa ngozi kujilinda na kujitambua na kusema kuwa hilo ni jambo jema.

Mambo meninge aliyoyasifia kwa Tanzania ni pamoja na mifumo mizuri iliyowekwa  katika kuhakikisha watu wenye ulemavu wa ngozi wanasikika au kushiriki kwenye vikao vya maamuzi yanayowagusa moja kwa moja, utengenezaji wa mafuta maalumu ya ngozi (sunscreen) ndani ya nchi na kuyasambaza kwa wahitaji wote nchini, uanzishwaji wa mpango jumuishi wa kitaifa ambao lengo lake ni kuhakikisha wanafunzi wenye ulemavu na hasa wenye ulemavu wa ngozi wanawekewa mazingira mazuri na rafiki ya kuwawezesha kupata haki yao ya elimu na mfumo mzuri wa mashauri/kesi za watu wenye ulemavu wa ngozi kupewa kipaumbele kwa kusikilizwa kwa haraka.

Wakati wa majadiliano, Tanzania ilitoa hotuba kuhusiana na hatua zinazochukuliwa na Serikali katika kulinda haki za watu wenye ulemavu wa ngozi. Hotuba hiyo, pamoja na mambo mengine ilieleza kuwa Serikali imetekeleza mapendekezo yaliyotolewa na Mtaalamu huyo wa Kujitegemea alipoitembelea Tanzania mwaka 2016 na kuwa Serikali itaendelea kushirikiana naye ili kuhakikisha kuwa watu wenye ulemavu wa ngozi wanapata ulinzi na kuwa haki zao zinalindwa kama raia wengine. 

Katika hatua nyingine, Mwakilishi wa Shirika lisilo la Kiserikali liitwalo World Barua Organization lenye makao makuu yake Geneva naye alitoa  hotuba kwenye Baraza la Haki za Binadamu na kuipongeza Serikali ya Tanzania kwa kuwa na mfumo mzuri wa kukusanya takwimu kuhusu watu wenye ulemavu wa ngozi.

Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post