TANGA UWASA YAWATAKA WATEJA KUCHUKUA TAHADHARI WAKATI WA KUPATA HUDUMA KWA KUEPUKA MIRUNDIKANO

 Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Jijini Tanga (Tanga Uwasa) Mhandisi Geofrey Hilly akizungumza na wakati wa mkutano wake na vyombo vya habari kuhusu maadhimisho ya wiki ya maji inayoanza Machi 16 hadi 22 mwaka huu kulia  ni Meneja wa Ruwasa Mkoa wa Tanga Mhandisi Upendo Lugongo
 Meneja wa Ruwasa Mkoa wa Tanga Mhandisi Upendo Lugongo kulia akisistiza jambo wakati wa mkutano huo kushoto ni Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Jijini Tanga (Tanga Uwasa) Mhandisi Geofrey Hilly
 Sehemu ya waandishi wa habari wakichukua matukio mbalimbali
 Mwandishi wa Gazeti la Citizen Mkoa wa Tanga George Sembony kushoto akiwa na Amina Omari wa gazeti la Mtanzania wakifuatilia mkutano huo kwa umakini


MAMLAKA ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Jijini Tanga (Tanga Uwasa) imewataka wateja wao kuchukua tahadhari na kufuata maelekezo kama watakavyoongozwa wakati wakupatiwa  huduma ikiwemo kuepuka kurundikana kwa pamoja kwenye madirisha ili kukabiliana  na maambukizi ya ugonjwa wa Corona.

Amesema tahadhari hiyo wameichukua ikiwa ni hatua mojawapo kuunga mkono juhudi serikali kuzuia kuingia nchini ugonjwa huo kwa kutoa elimu  kwa njia ya jumbe mbalimbali katika maeneo ya ofisi zao,hususani majengo ya huduma kwa wateja pamoja na kuwa na sehemu za wateja pamoja na watumishi kuosha mikono yao

Hayo yalisemwa leo na Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Jijini Tanga (Tanga Uwasa) Mhandisi Geofrey Hilly wakati wa mkutano wake na vyombo vya habari kuhusu maadhimisho ya wiki ya maji inayoanza Machi 16 hadi 22 mwaka huu.

Alisema kwamba kwa kuwa maeneo yao hususani kwenye ofisi za kutolea huduma ni mojawapo wa maeneo yenye mwingilio mkubwa wa watu hivyo ni wajibu wao kuhakikisha wanachukua tahadhari ya kukabiliana na ugonjwa huo.

“Kufuatia na maagizo mbalimbali yanayotolewa na viongozi wa nchi juu ya ugonjwa huo sisi kama mamlaka tumeona ni muhimu kuanza kuchukua hatua mapema za kukabiliana nao”Alisema Mkurugenzi huyo.

Alisema miongoni mwa tahadhari ambazo zimeanza kuchukuliwa na mamlaka ni pamoja na kuunga mkono serikali kwa kutoa elimu juu ya ugonjwa huo kwa njia ya ujumbe mbalimbali katika maeneo ya ofisi ,majengo ya huduma kwa wateja kuwa na sehemu za wateja na watumishi kwa ajili ya kuosha mikono.

“Sisi tumekuwa na madirisha ya huduma kwa wateja hivyo ndio maana tumeamua kuchukua tahadhari hivyo kutokana na kwamba wakati mwengine wateja wanakuwa na fujo wanarundikana wanataka kila mmoja asikilize kwa wakati na ndio maana tumeamua kufanya hivyo”Alisema

Mkurugenzi huyo alisema kwamba wataweka huduma ya kunawa mikono kwa sababu ugonjwa huo asilimia kubwa unatokana na kugusanagusana kwa hiyo kila wakati mtu ahakikisha amenawa mikono na sabuni.

“Tunasisitiza kuchukua tahadhari watumishi na wateja wote lakini pia tutaweka maeneo ya kunawa mikono kwenye ofisi zao kuwasaidia watu ambao wanakuja kupata huduma kunawa mikono “Alisema

Awali akizungumza wakati wa mkutano huo Meneja wa Ruwasa Mkoa wa Tanga Mhandisi Upendo Lugongo alisema upatikanaji wa maji vijijini kwa wastani ni asilimia 52 lakini kwenye mikuu ya wilaya ni asilimia 54 na Jiji la Tanga ni asilimia 89 na watu wanapata maji safi.

Alisema kwa Tanga wapo vizuri na wanajitahidi miradi yote inakwenda kutekeleza kupitia njia ya uwezo wa ndani na wakandarasi watatumika kwa uchache ili wananchi waweze kupata huduma kwa haraka ndani ya muda mfupi.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post