NIDA YAHAKIKI UPYA MAOMBI YA VITAMBULISHO VYA TAIFA VYENYE CHANGAMOTO ZA URAIA


Wafanyakazi wa NIDA wakiwa katika zoezi la kuwasajili wananchi mbalimbali wanaoomba vitambulivyo vya
Taifa.Wafanyakazi wa NIDA wakiwa katika zoezi la kuwasajili wananchi mbalimbali wanaoomba vitambulivyo vya
Taifa.
Baadhi ya wananchi wakitoka na kuingia katika ofisi moja wapo ya Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) katika zoezi linaoendelea la uhakiki wa vitambulisho vya Taifa.

**************************

Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), inaendelea kutekeleza agizo la Serikali la kuhakiki kwa kina maombi yote ya waombaji wa Vitambulisho vya Taifa yenye
changamoto na upungufu mbalimbali ukiwemo uraia wa waombaji ili kuondoa mianya ya udanganyifu unaoweza kujipenyeza na hivyo kutoa Vitambulisho vya raia
kwa watu wasio raia wa Tanzania.

Kwa mujibu wa Afisa Habari Mkuu wa NIDA Bw. Geofrey Tengeneza, NIDA kwa kushirikiana na Idara ya Uhamiaji, Kamati za Ulinzi na Usalama za Wilaya na Mikoa, Serikali za Mitaa, Idara ya Wakimbizi, Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR) wameanza kufanya uhakiki wa kina kwa kupitia maombi yote ya waombaji wa Vitambulisho vya Taifa.

Zoezi la uhakiki linakwenda sambamba na usajili wa raia, wageni wakaazi na Wakimbizi, ugawaji wa NIN na vitambulisho kwa wakazi wa mikoa iliyoko kanda ya
ziwa ambayo ni Kigoma, Kagera, Tabora, Geita, Mwanza Simiyu, Shinyanga na Mara, zoezi linaendeshwa kwa kushirikiana na wadau wengine wa mawasiliano.

Katika Kuhakikisha kuwa wanaopata Vitambulisho hivyo ni watu wanaostahili NIDA imejipanga kufanya uhakiki wa mara kwa mara kulingana na Sheria ya Usajili na
Utambuzi wa Watu ambayo inaeleza kuwa mwombaji yeyote wa Kitambulisho cha Taifa atakayebainika kutoa taarifa za uongo kuhusu uraia wake, Sheria itachukua
mkondo wake sambasamba na kunyanganywa Kitambulisho hata kama atakuwa tayari alikwishapata.

“Niwasihi wale wote wenye nia ya kutaka kujipenyeza na kupata Vitambulisho kinyume cha utaratibu, haitawasaidia kwani uhakiki unaofanywa na Mamlaka kwa kushirikiana na wadau ni endelevu na utafikia mikoa yote nchini, hivyo ni vyema kama kuna mwombaji yeyote anajua amedanganya taarifa za uraia wake akajisalimisha mapema kabla ya mkono wa sheria haujamfikia” amesema Bw. Tengeneza.

Akizungumzia sababu ya kuanza na mikoa ya Kanda ya Ziwa msemaji huyo wa NIDA amedokeza kuwa japokuwa zoezi hili litafanyika nchi nzima lakini limeanza katika
mikoa ya kanda ya ziwa kutokana na mikoa hiyo kuwa mipakani ambapo kunakuwa na mchangamano wa wakaazi kutoka nchi jirani hivyo kuwa rahisi kwa raia wa nchi
hizo kujipenyeza ili wajisajili kama raia wa Tanzania.

Sambamba na zoezi la uhakiki wa taarifa za waombaji hususan zenye mapungufu ya uraia wa waombaji, NIDA inaendelea pia kutoa huduma ya Usajili kwa wananchi wa
Kanda ya Ziwa na katika kila wilaya nchini kupitia Ofisi za Kudumu za Usajili za Mamlaka hiyo pamoja na vituo mbalimbali vya muda vilivyowekwa kwenye kata
mbalimbali kulingana na mahitaji ya wilaya husika.

Aidha, NIDA imefanikiwa kuwafikia idadi kubwa ya wananchi ambapo zaidi ya watu milioni 21,721,416 wamesajiliwa huku miongoni mwao watu milioni 17,674,812 wameshatambuliwa kwa kupatiwa Namba za Utambulisho wa Taifa na wengine Vitambulisho vya Taifa. Taarifa za waombaji wengine waliosajiliwa zinaendelea
kuchakatwa ili Namba zao za Utambulisho na Vitambulisho vyao vya Taifa vitolewe mapema iwezekanavyo.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post