MWILI WA MZEE CHARLES KANUMBA KUAGWA KESHO SHINYANGA, KUZIKWA KESHO KUTWA BUSEGA


Mwili wa Baba wa aliyekuwa msanii wa Bongo Movies marehemu Stephen Kanumba, mzee Charles Kanumba (73), aliyefariki dunia Jana Machi 8,2020 majira ya saa 4 asubuhi hospitali ya rufaa ya mkoa wa Shinyanga, unatarajiwa kuzikwa siku ya Jumatano Machi 11,2020 kijijini kwao Nyakaboja Busega mkoani Simiyu.

Mtoto wa marehemu Mjanael Kanumba, amesema mwili wa marehemu baba yake umehifadhiwa kwenye chumba cha maiti katika hospitali ya rufaa  mkoan wa Shinyanga, ambapo kesho Jumanne Machi 10,2020 utaagwa na wakazi wa Shinyanga nyumbani kwake mtaa wa Magadula Kata ya Ngokolo, na kisha utasafirishwa kupelekwa kijiji cha Nyakaboja Busega Simiyu kwa ajili ya mazishi.

“Baba yangu amefariki jana majira ya saa 4 asubuhi, katika Hositali ya Rufani ya Mkoa wa Shinyanga alipokuwa akipatiwa matibabu ya nyonga, magoti, pamoja na kibovu cha mkojo ambacho alifanyiwa upasuaji mara mbili, na pia alikuwa na uzito uliokithiri,”amesema Mjanael.

“Mzee alikuwa akisumbuliwa na magonjwa hayo zaidi ya miaka mitatu, na ametuacha tukiwa watoto wanne, na mwili wake tutausafirisha kwenda kijiji kwao alipozaliwa huko Nyakaboja Busega mkoani Simiyu, kwa ajili ya kumstiri kwenye makazi yake ya milele,”ameongeza.

Mzee Charles Kanumba alikuwa akisumbuliwa na ugonjwa wa nyonga, magoti, pamoja na kibofu cha mkojo kwa muda wa miaka mitatu hadi umauti ulipomfika.

Mzee Charles Kanumba, ni baba mzazi wa marehemu Stephen Kanumba, ambaye alikuwa msanii mkubwa wa filamu za kuigiza hapa nchini ( Bongo Movies), aliyefariki dunia mwaka 2012 na alikuwa msaada mkubwa katika familia yake.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post