ASKOFU AONYA UZINZI,MIMBA KWA WANAFUNZI LIKIZO YA CORONA


Askofu David Mabushi

Na Estomine Henry - Shinyanga

Siku chache baada ya Serikali kutangaza wanafunzi wote nchini kuanzia shule za msingi, Sekondari, vyuo vya kati na vikuu kurudi majumbani kupumzika kwa mwezi mmoja (siku 30) ili kuepuka kusambaa kwa virusi vya Corona Askofu  kanisa la International Evangelical Assemblies of God Tanzania (IEAGT) la mjini Shinyanga David Mabushi ameonya ongezeko la vitendo vya uzinzi na mimba kwa wanafunzi.



Akizungumza jana Jumatatu Machi 23,2020 na waumini wa kanisa hilo askofu Mabushi alitoa tahadhari kwa wazazi na walezi na pamoja wanafunzi wa shule na vyuo kuwa makini sana kipindi hiki cha likizo maalumu ya kupisha ugonjwa wa Corona ili kuepuka mimba zisizotarajiwa hasa kwa wanafunzi wa kike.



Askofu Mabushi aliwataka wazazi na walezi kote nchini  kuongeza umakini na udhibiti kwa watoto wao ambao wamerudi nyumbani kwa mapumziko ya mwezi mmoja kuepusha kusambaa kwa virusi vya Corona, ili isije kuleta madhara zaidi kwa wanafunzi hao kutumbukia kwenye uzinzi na kuleta mimba pindi wakiwa likizo.

Aliwasihi wazazi na walezi kutowaacha  wanafunzi wakizurura hovyo mitaani na kuingia katika vishawishi mbalimbali ili muda wa shule utakapofunguliwa watoto/wanafunzi warudi shule wakiwa salama na kuendelea na masomo yao.

"Wazazi na walezi mnapoweka akili yenu kwenye Corona,tazameni pia likizo kwa wanafunzi hawa waliopo majumbani sasa. Kipindi hiki ni muhimu sana kuweka usimamizi wa kutosha kwa watoto wetu kwa kuwa wengi hawajitambui kabisa na ipo hatari ya kuingia katika janga lingine la mimba zisizotarajiwa kama tutakuwa na usimamizi hafifu kwa watoto wetu",alisema Askofu Mabushi.

"Ni vyema wazazi na walezi kila mmoja akawa makini na ratiba ya kila siku ya mtoto wake kwa kujua ni wapi anakwenda kila siku na huko anako kwenda kuna usalama wa kutosha hasa kwa watoto wa kike ili nchi isije ikajikuta kwa kipindi hiki kifupi imeathirika na janga lingine la mimba kwa wanafunzi",aliongeza Askofu Mabushi.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527