LIUNDI : MIFUMO YA UWAJIBIKAJI NA UWAJIBISHAJI BADO HAIJAKAA VIZURI KUSUKUMA MBELE ZAIDI MASUALA YA JINSIA TANZANIA

Mkurugenzi Mtendaji wa Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP),Lilian Liundi akizungumza kwenye Kongamano la Kuadhimisha na Kusherehekea Siku ya Wanawake Duniani na Miaka 25 baada ya Mkutano wa Beijing Machi 4,2020.


Na Kadama Malunde - Malunde 1 blog

Imeelezwa kuwa bado mifumo ya uwajibikaji na uwajibishaji nchini Tanzania haijakaa vizuri kuwezesha kusukuma mbele zaidi masuala ya jinsia hali inayosababisha sekta mbalimbali kutotilia mkazo suala la kupanga bajeti kwa mrengo wa kijinsia.

Hayo yamesemwa Machi 4,2020 na Mkurugenzi Mtendaji wa Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP),Lilian Liundi wakati akizungumza kwenye Kongamano la Kuadhimisha na Kusherehekea Siku ya Wanawake Duniani na Miaka 25 baada ya Mkutano wa Beijing linalofanyika katika Ukumbi wa Hyatt Regency Hotel Jijini Dar es salaam ambapo mgeni rasmi alikuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan.

Liundi alisema licha ya kazi kubwa iliyofanywa na wanaharakati kudai bajeti yenye mrengo wa kijinsia ambayo inafanya uchambuzi wa kina wa makundi mbalimbali ya kijamii,mahitaji yao na mgawanyo wa rasilimali lakini changamoto iliyopo ni uwajibikaji na uwajishaji kwa serikali,Asasi za Kiraia na wadau mbalimbali.

“Tatizo kubwa lililopo ni mifumo ya uwajibikaji na uwajibishaji haijakaa vizuri kwetu sisi wenyewe,kwa serikali na kwa viongozi mbalimbali. Katika sera zilizopo kulitakiwa kuwe na mifumo mahsusi ya ufuatiliaji na utoaji taarifa tuone tumefika wapi,tatizo liko wapi na tufanye nini?”,alisema Liundi.

“Lakini kwa uchambuzi tulioufanya kuhusu masuala ya haki za kiuchumi, TGNP tumegundua kwamba hakuna huo mfumo ambao unaingia kwenye sekta mbalimbali,unafuatilia na unatoa maelekezo ya kutoa taarifa ili tujue tumefika wapi na tunaelekea wapi na tutatue vipi hizo changamoto, hilo ni tatizo kubwa”,aliongeza Liundi.

Aliziomba Asasi za Kiraia kutonyamaza bali ziwe mstari wa mbele kufuatilia utekelezaji wa sera mbalimbali kuhusu masuala ya jinsia.

“Kutokana na kazi za Asasi za kiraia nguvu ilifanyika. Kuna baadhi ya sekta zilianza kubajeti kwa mrengo wa kijinsia,tulitengeneza kitita cha muongozo ili Wizara ya Fedha iweze kutoa maelekezo na hata sasa TAMISEMI kuna mwongozo wa kuweka bajeti katika mrengo wa kijinsia lakini kuna tatizo la utekelezaji.

Katika huu utekelezaji kuna tatizo kubwa la uwekezaji wa rasilimali kutekeleza masuala ya kijinsia,Rasilimali fedha,rasilimali ujuzi,teknolojia na rasilimali watu wenye uwezo hilo ni tatizo kubwa ambalo linahitaji mkakati mkubwa ili kulitekeleza”,alieleza Liundi.

“Na sisi asasi za kiraia tulinyamaza ,tunapoona hizo Commitment zipo,hizo sera zipo pia ni wajibu wetu kuangalia na kufuatilia. Tuna wajibu,serikali inawajibu mpaka hata kwenye ngazi za serikali ya mtaa kuna wajibu wa kufuatilia”,alisema.

Aidha alishauri asasi za kiraia kwenda hadi kwa wanajamii kuwajengea uwezo kuhakikisha wanaweza kufanya uwajibikaji na uwajibishaji kwenye masuala ya kijinsia.

“Tukiweka nguvu zetu inawezekana sisi TGNP tumefanya kwenye zaidi ya wilaya 8,tumefanya kwa kupitia vituo vya taarifa na maarifa na bajeti zimebadilika.Sasa hivi ni wilaya tano kati ya 8 tunazofanya nazo kazi wanatenga bajeti kwenye Pedi za wanafunzi wa kike na ni nguvu za wananchi wa kawaida kabisa”,alisema Liundi.

“Lakini pia ili kuleta msukumo wa sekta kwa wenzetu Mawaziri wanapotoa taarifa za bajeti watoe tamko la jinsi gani wametekeleza masuala ya kijinsia kwenye sekta zao hii inaongeza hali ya uwajibikaji. Kuna haja ya kuwa na takwimu zenye uchambuzi wa kijinsia ili kufanya maamuzi yenye mrengo wa kijinsia hili eneo linatuhitaji sote japo sasa NBS inafanya kazi nzuri”,alisema. 

Alisema pia ipo haja kila mwaka kuwa na ripoti ya utekelezaji wa masuala ya wanawake na takwimu zenye mrengo wa kijinsia katika maeneo mbalimbali huku akishauri wanawake kutumia Teknolojia na ubunifu,kupata kupata mapinduzi ya kiuchumi.

“Teknolojia na ubunifu ni muhimu sana. Wanawake tuhakikishe tunatumia Teknolojia na mbinu bunifu katika kupata taarifa na maarifa ya kuboresha jitihada zetu za kujiwezesha kiuchumi. Pia nitoe rai kwa wanahabari kusaidia upatikanaji wa taarifa zenye mrengo wa kijinsia",alisema Liundi.

“Tunapozungumzia haki za kiuchumi na uwezeshaji kiuchumi,tusizungumzie kama kitu kinachosimama peke yake.Tunapokuwa na viongozi wanawake pia katika masuala ya kiuchumi,mwanamke mwenye uchumi mzuri ni rahisi kuwa kiongozi”,aliongeza.

Kongamano la Kuadhimisha na Kusherehekea Siku ya Wanawake Duniani na Miaka 25 baada ya Mkutano wa Beijing likiongozwa na Kauli mbiu ya ''Uwajibikaji wa uongozi kwenye kujenga kizazi cha usawa wa jinsia'' limeandaliwa na Mtandao wa Wanawake na katiba, Uchaguzi na Uongozi kwa ufadhili wa Women Fund Tanzania, Global Affairs Canada, Embassy of Ireland, High Commission of Canada na WiLDAF. 


Mkurugenzi Mtendaji wa Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP),Lilian Liundi akizungumza kwenye Kongamano la Kuadhimisha na Kusherehekea Siku ya Wanawake Duniani na Miaka 25 baada ya Mkutano wa Beijing Machi 4,2020.Picha na Kadama Malunde - Malunde 1 blog
Mkurugenzi Mtendaji wa Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP),Lilian Liundi wakati akizungumza kwenye Kongamano la Kuadhimisha na Kusherehekea Siku ya Wanawake Duniani na Miaka 25 baada ya Mkutano wa Beijing Machi 4,2020.
Picha na Kadama Malunde - Malunde 1 blog

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post