MAMLAKA YA HALI YA HEWA TANZANIA (TMA) YATOA TAHADHARI MVUA ZA MASIKA ZINAZOENDELEA NCHINI


Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) inatoa taarifa kuhusu mvua za msimu wa masika (Machi – Mei) zinazoendelea hususan katika maeneo yanayopata misimu miwili ya mvua kwa mwaka, yaani (Ukanda wa Ziwa Viktoria, nyanda za juu kaskazini mashariki pamoja na pwani ya kaskazini). Mvua katika maeneo haya zimeanza vizuri kama ilivyotarajiwa katika wiki ya kwanza na ya pili ya mwezi Machi, 2020.

Katika hatua nyingine, mvua kubwa zilizojitokeza zimesababishwa na uwepo wa joto la bahari kuwa juu ya wastani mfululizo kuanzia mwezi Oktoba, 2019 hadi sasa na pia kuimarika kwa ukanda mvua (ITCZ) sambamba na kujitokeza kwa migandamizo midogo ya hewa katika Bahari ya Hindi na hivyo kumeongeza viwango vya mvua zinazonyesha katika muda mfupi.

Aidha, hali hiyo ya kuimarika kwa ukanda mvua (ITCZ) pamoja na uwepo wa mgandamizo mdogo wa hewa (Depression) Kaskazini Mashariki mwa kisiwa cha Madagascar inaendelea kusababisha ongezeko la mvua katika maeneo mengi nchini katika kipindi hiki.Sambamba na hayo, ongezeko la mvua linatarajiwa kwa kiwango cha juu katika mwezi Machi na Aprili 2020, na kutarajiwa kupungua katika mwezi Mei kwa maeneo yanayopata misimu miwili ya mvua kwa mwaka (maeneo ya kaskazini mwa nchi).

Kwa upande mwingine, mvua za MSIMU zilizoanza mwezi Novemba, 2019 katika maeneo yanayopata msimu mmoja wa mvua kwa mwaka(maeneo ya kusini, kati na magharibi mwa nchi) zinatarajiwa kuendelea hadi mwezi Aprili, 2020.

TMA inaendelea kufuatilia mifumo ya hali ya hewa na kutoa mrejesho kadri mabadiliko yatakavyokuwa yanajitokeza.

ATHARI: Wakati wa kuandaa utabiri wa msimu wa mvua za Masika, 2020, TMA iliwashirikisha wadau kwa kiasi kikubwa. Wadau hao walionesha kwamba mvua zinazoendelea kunyesha zitakuwa na athari katika sekta nyingi za kiuchumi na kijamii.

Baadhi ya athari zinazotarajiwa kutokana na vipindi vya mvua kubwa vinavyoambatana na upepo mkali ni pamoja na uharibifu wa mazao, milipuko ya magonjwa ya binadamu, wanyama na mimea, mafuriko, uharibifu wa miundo mbinu n.k. Aidha, wataalam katika sekta husika wana utaalam wa kutosha kutathmini kwa weledi zaidi athari zinazoweza kujitokeza kutokana na vipindi vya mvua kubwa vinavyoendelea kujitokeza katika msimu huu wa mvua.

USHAURI: Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania inawashauri watumiaji wa taarifa hii ikiwa ni pamoja na wakulima, wafugaji, Mamlaka za Wanyamapori, Wasafirishaji, Mamlaka za Maji na Afya kuendelea kutafuta, kupata na kufuata ushauri wa wataalam katika sekta husika. Pia kuendelea kufuatilia utabiri wa saa 24, siku 10, mwezi pamoja na tahadhari kila zinapotolewa na kuchukua hatua.

Imetolewa na;
Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527