Breaking : AJENTI WA BASI LA KISBO AFARIKI DUNIA KWA KUKANYAGWA TAIRI AKIDANDIA BASI SHINYANGA


Na Kadama Malunde - Malunde 1 blog
Wakala/Ajenti wa Basi la Kisbo Express lenye namba za usajili T192 DBZ linalofanya safari zake kutoka Mwanza kwenda Dar es Salaam Athuman Omary (38) mkazi wa Buhongwa jijini Mwanza amefariki dunia kwa kugongwa na basi akidandia basi likitoka katika Kituo Kikuu cha Mabasi mkoa wa Shinyanga.

Tukio hilo limetokea leo Ijumaa Machi 27,2020 majira ya saa mbili na dakika 20 asubuhi wakati Wakala huyo akidandia basi hilo na kisha kuanguka na kukanyagwa na basi akafariki dunia hapo hapo.

Mashuhuda waliozungumza na Malunde 1 blog wanasema Athuman Omary ni Wakala wa Basi la Kisbo alikuwa anatokea Mwanza na basi hilo alipofika Shinyanga alishuka basi lilipoanza kuondoka akawa anakimbilia hilo basi ambalo lilikuwa linatoka getini akadondoka chini akakanyagwa na tairi za basi hilo.

"Huyo Wakala huwa huwa wanasindikiza magari hayo kwa ajili ya kukusanya pesa, walipofika stendi wakasimama kupakia abiria. Wamepakia abiria walipomaliza basi likaanza kuondoka,yeye alikuwa nje ya basi sasa wakati anakimbilia hilo basi ambalo lilikuwa linatoka getini likikata kona,mlango wa basi ukacheza,akadondoka chini akakanyagwa na tairi za basi hilo.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga ACP Deborah Magiligimba amesema basi hilo lilimkanyaga Wakala huyo ambaye alikuwa anakimbilia gari baada ya kumaliza kupakia abiria ndipo akateleza na kuanguka akakanyagwa mguu wa kushoto,kiuno na tumboni na kusababisha kifo chake papo hapo.

Kamanda Magiligimba amesema basi hilo lipo kwenye kituo cha polisi na wanamshikilia dereva wa basi hilo aitwaye Jabu Dalweshi (45) mkazi wa Dar es salaam kwa mahojiano zaidi huku akiwataka madereva kuwa makini na kutumia vioo vya kuongozea magari ili kubaini watu wanaokimbilia gari waweze kuchukua tahadhari.
Mwili wa marehemu Athuman Omary ukiwa chini baada ya kukanyagwa na basi la Kisbo leo Machi 27,2020 katika stwndi ya mabasi mkoa wa Shinyanga alipokuwa anadandia basi la Kisbo Picha na Malunde 1 blog

Mwili wa marehemu Athuman Omary ukiingizwa kwenye gari la polisiDownload/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post