KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA ARDHI , MALIASI NA UTALII YAKATAA MILIONI 150 KUKARABATI JENGO LA UTAWALA

NA TIGANYA VINCENT

WAJUMBE wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi , Maliasi na Utalii wameagiza kujengwa kwa Jengo la Utawala katika Chuo cha Mafunzo ya ufagaji nyuki (BTI) badala ya kukarabati lilipo kwa gharama ya shilingi milioni 150.

Ilisema fedha hizo zinaweza kujenga jengo jipya kwa fedha kidogo na zitakazobaki zikatumika katika shughuli nyingine.

Kamati hiyo imetoa kauli hiyo leo wakati wajumbe wake walipotembelea Chuo hicho kwa ajili ya kukagua jengo linatotaka kukarabatiwa na kukagua shughuli nyingine za mafunzo ya ufugaji nyuki mkoani Tabora.

Mbunge wa Jimbo la Mbulu Vijijini Flatei Massay alisema matumizi ya milioni 150 kwa ajili ya ukarabati ni kinyume na mipango ya Serikali ya awamu ya Tano ya matumizi kidogo ya fedha matokeo makubwa ya mradi.

Aliiomba Wizara ya Maliasili na Utalii kusimamisha matumizi ya fedha hizo ili ziliekelezwe katika ujenzi wa jengo jipya na la kisasa.

Naye Mbunge wa Jimbo la Longido Dkt. Steven Kiruswa alisema ni vema utaratibu wa utekelezaji wa mradi huo utatumia ujenzi kwa kutumia mafundi wa ndani( force account) ili kuwezesha sehemu ya fedha zikabaki na kuelekekwa kujenga miundo mbinu mingine. 

Mbunge Jimbo la Chambani Yussuf Salim Hussein alimwomba Mkuu wa Mkoa wa Tabora kuhakikisha anasimamia ili utaratibu wa ujenzi uwezo wa kutumia mafundi ya ndani ya Taasisi kwa ajili ya kuhakikisha matumizi sahihi.

Kwa upande wa Mbunge wa Jimbo la Kaliua  Magdalena Sakaya alisema utendaji kazi wa Wakala wa Majengo nchini (TBA) sio mzuri na ndio miradi yao mingi inakuwa na gharama kubwa.

Alisema kuwa pamoja na kuwa ni Taasisi ya umma ni vema Serikali ikatumia utaratibu mwingine kuliko kuwapa miradi ambayo wanashindwa kuikamirisha kwa wakati na wakati mwingine ubora wake hauridhishi.

Aidha alisema badala ya kujenga jengo la utawala ni vema fedha hizo zikatumika kujenga Maabara kwa ajili kutoa mafunzo ya uzalishaji asali bora.

Mwenyekiti wa Kamati hiyo Kemirembe Lwota aliitaka Wizara hiyo kubadili mpango wa awali wa kutumia fedha hizo ili zielekezwe kwenye ujenzi wa jengo jipya la utawala.

Naye  Naibu Katibu wa Wizara ya Maliasili na Utalii Dkt. Aloyce Nzuki amesimamisha zabuni ya ukarabati wa jengo hilo ambayo ilikuwa ifunguliwe wiki ijayo.

Alisema wamekubaliana na ushauri wa Kamati wa kutumia fedha hizo kwa ajili ya ujenzi wa jengo jipya na sio ukarabati.

Mwisho


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post