CHADEMA WAJUTIA MAKOSA YA 2015.....BARAZA LA WAZEE LAMKATAA BENARD MEMBE


Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimesema kinajutia uamuzi kiliochukua wakati wa kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, kuchukua wale waliokatwa kutoka CCM ambao sasa wamerejea katika chama chao cha zamani.


Akizungumza ofisi za Makao Makuu ya Chadema jana, Mwenyekiti wa Baraza la Wazee la Chadema (Bazecha), Hashim Juma alisema pamoja na heshima aliyonayo kwa aliyekuwa mgombea wa Ukawa mwaka 2015, Edward Lowassa, lakini tathmini ya baraza hilo imeonyesha hakuwa na msaada mkubwa kwenye chama.

“Kwa kweli katika Uchaguzi Mkuu wa 2015 tuliweka mgombea dhaifu ambaye kwanza alishindwa kulinda kura zetu kwa sababu ya u-CCM wake ambao hakuuvua wakati huo.

“Lakini pia ndani ya Ukawa tulisimamisha mgombea mwenza ambaye pia hakuwa mwana Chadema, hivyo hakuwa na uchungu na chama chetu.

“Kwa hiyo, hatutaki kuona makosa tuliyoyafanya mwaka 2015 yakijirudia mwaka huu, hasa baada ya kukijenga chama nchi nzima kuanzia ngazi ya chini kabisa, kazi tuliyoifanya kwa miaka miwili.

“Ni wazi kwamba tayari kuna mmoja wa viongozi wakuu wa chama, ambaye ana uchungu na chama, aliyeko nje ya nchi kwa sasa, ambaye ameshaeleza utayari wake wa kuwania urais iwapo atateuliwa na chama kwa hiyo huyo ndiye tunayemuunga mkono,” alisema Juma.

Mwenyekiti huyo wa Bazecha alisisitiza kuwa kwa sasa hawako tayari kutumika kama njia ya baadhi ya wanasiasa kutaka kutimiza mahitaji yao binafsi kwa kuingia katika chama hicho na wakikosa wanachokihitaji wanarejea kule walikotoka, kama walivyofanya baadhi ya wanasiasa walioingia Chadema kisha kurejea CCM baada ya kushindwa kutimiza malengo yao binafsi.

Alisema japokuwa baraza hilo halina mamlaka ya Kamati Kuu ya chama, wala ya mkutano mkuu, baraza hilo linatamka wazi kwamba haliko tayari kuona uongozi wa chama hicho ukizungumza suala la kumpokea Bernard Membe, aliyekuwa mwanachama wa CCM ambaye Kamati Kuu ya chama chake imeridhia kwa kauli moja kumvua uanachama.


“Sisi kama wazee tumemridhia na tunampa baraka zetu zote Lissu, kwa hivyo Mheshimiwa Membe tunamtakia kila la kheri na kama atakwenda chama kingine, tutashukuru na tutafurahi kwa sababu kwa vyovyote vile anakwenda kuzigawa kura za CCM.

“Ni kwa sababu, Membe hawezi kuchukua kura hata moja ya Chadema, ataondoka na kundi kubwa la CCM kama Lowasa hivyo atapata kura za chama atachoenda pamoja na za CCM.” amesema Mzee Hashimu. 


Wakati huo huo Mzee Hashimu ameeleza, msimamo wa baraza hilo ni kupigania Tume Huru ya Uchaguzi ili uchaguzi wa tarehe 25 Oktoba 2020 uwe wa huru na haki.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post