BODI YA KOROSHO YATAKIWA KULIPA TSHS. MILIONI 16 ZA KUKODI GHALA


Bodi ya Korosho yatakiwa kulipa Shilingi Milioni 16 inazodaiwa na Kijiji cha  Kimanzichana Kaskazini kilichopo Wilaya ya Mkuranga Mkoani Pwani baada ya kukodi ghala la kijiji hicho kwa ajili ya kuhifadhi pembejeo za kilimo za zao la korosho.

Akizungumza mapema wiki hii wakati wa ziara ya kutembela maendeleo ya vijiji vya Kimanzichana Kaskazini na Kilimahewa viliyopo katika wilaya hiyo, Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Mkuranga ameutaka uongozi wa bodi hiyo kuhakikisha unailipa Serikali ya kijiji cha Kimanzichana Kaskazini kiasi hicho cha fedha ili kiweze kufanya shughuli mbalimbali za maendeleo.

Aidha katika ziara hiyo Naibu Waziri Ulega amepata fursa ya kutembelea shule za msingi Kimanzichana Magharibi, Kilimahewa na Shule ya Sekondari Mkamba na kuzungumza na wanafunzi huku akiwataka kuweka bidii katika masomo yao.

Mbali na kuzungumza na wanafunzi hao Naibu Waziri Ulega ambaye ni Mbunge wa Jimbo hilo la Mkuranga ametoa zawadi ya madaftari katika shule hizo ikiwa ni sehemu ya ahadi aliyotoa ili kuongeza tija kwa wanafunzi hao waweze kufanya vizuri zaidi katika masomo yao kwa kuwa na vifaa muhimu shuleni.

Halikadhalika Mhe. Ulega ametembelea pia jengo la ofisi ya Serikali ya Kijiji cha Kilimahewa ambapo ujenzi wake hadi sasa umegharimu Shilingi Milioni 40 na kutoa mchango wa Shilingi laki Tano kwa ajili ya kuendeleza ujenzi huo na kupanda mti nje ya jengo la ofisi hiyo.

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Mkuranga Mkoani Pwani yupo katika ziara ya kikazi jimboni humo kwa ajili ya kukagua shughuli mbalimbali na miradi ya maendeleo.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post