ZITTO KABWE ASHINDWA KUHUDHURIA MAHAKAMANI BAADA YA KUDAIWA AMELAZWA MAREKANI


Mdhamini wa Mbunge wa Kigoma Mjini (ACT-Wazalendo),  Zitto Kabwe ameileza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwa mbunge huyo ameshindwa kufika mahakamani leo Jumatatu Februari 10, 2020 baada ya kuugua akiwa nchini Marekani.

Mdhamini huyo,  Ray Kimbita ameeleza hayo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu,  Huruma Shahidi wakati kesi hiyo ilipokuja kwa ajili ya kutolewa uamuzi kama ana kesi ya kujibu au la baada ya upande wa mashtaka kufunga ushahidi.

"Mshtakiwa yuko nje ya nchi jana niliwasiliana na Nassor Mazrui ambaye yuko naye baada ya kunipigia na kunieleza kuwa amelazwa katika hospitali ya Leesburg Marekani.”

"Alikuwa ameshakata tiketi kwa ajili yakurejea nchini ili ahudhurie kwenye kesi kutokana na kuugua kwake madaktari wamempumzisha kwa siku 10,” amedai Kimbita.

Wakili wa Serikali mwandamizi, Nassoro Katuga amedai kuwa mshtakiwa anapokuwa nje ya nchi  ni jukumu la mdhamini kujua alipo.

"Kitendo cha mdhamini huyo kupigiwa simu na mtu mwingine ina maana hajawasiliana na mshtakiwa na hajui alipo, atakaporudi aieleze Mahakama sababu za kutowasiliana na mdhamini wake pamoja na udhibitisho wa kuugua,” amedai Katuga.

Wakiki wa utetezi, Steven Mwakibolwa ameiomba Mahakama kumpa muda ili mshtakiwa huyo aje kueleza kwa nini hakuwasiliana na mdhamini pamoja na kuwasilisha nyaraka zitakazoonyesha ni mgonjwa.

Baada ya kueleza hayo Hakimu Shaidi ameahirisha kesi hiyo hadi Februari 18, 2020  na kumtaka mdhamini huyo kujitathimini kwa kuwa ameshindwa kujua mshtakiwa alipo.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post