WAZIRI MKUU: VYAMA VYA SIASA HAVIJAZUILIWA KUFANYA SHUGHULI ZAKE ZA KISIASA


Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema vyama vya siasa nchini havijazuiwa kufanya shughuli zake za kisiasa isipokuwa kumewekwa utaratibu wa vyama hivyo kufanya shughuli hizo kwenye maeneo yao ambayo wamepata ridhaa ya kuongoza.

Akijibu maswali ya Papo kwa Papo kwa Waziri Mkuu Bungeni jijini Dodoma, Waziri Mkuu Majaliwa amesema kuwa utaratibu uliopo sasa unaoonekana kama kuvinyima nafasi vyama vya siasa kufanya shughuli zake unalenga kuwawezesha Wanasiasa kufanya shughuli za kisiasa katika maeneo yao pasipo kubughudhiwa na Wanasiasa kutoka nje.

Waziri Mkuu Majaliwa alikua akijibu swali la Papo kwa Papo kutoka kwa Kiongozi wa Kambi rasmi ya Upinzani Bungeni Freeman Mbowe ambaye alitaka kufahamu ni lini Serikali itaviruhusu vyama vya siasa kufanya shughuli zake kama ilivyokua miaka ya nyuma.

"Ni lini mtaruhusu vyama vya siasa vifanye wajibu wake wa uenezi ili kujiandaa na Uchaguzi Mkuu na Serikali ina mpango gani wa kuwezesha taifa kuwa na Tume Huru ya Uchaguzi ili uchaguzi huu uwe wa haki na halali." -Aliuliza Freeman Mbowe

Kuhusu  suala la kuwepo kwa Tume huru ya Uchaguzi, Waziri Mkuu Majaliwa amesistiza kuwa Tume ya Taifa ya  Uchaguzi iliyopo sasa ni huru kwa kuwa imekua ikitekeleza majukumu yake kwa uhuru bila kuingiliwa na mtu yeyote awe Kiongozi ama Mwanasiasa.

Aidha Waziri Mkuu amesema kuwa si kweli kwamba nchi inaongozwa kibabe kama inavyodaiwa na baadhi ya watu, bali inaongozwa kwa kufuata misingi ya Kidemokrasia.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527