Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tamisemi, Selemani Jafo amemuagiza mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa mkoani Morogoro kumsimamisha kazi Daniel Elimringi ambaye video zinazosambaa katika mitandao ya kijamii zinamuonyesha akikanyaga kitabu cha dini.
Jafo ametoa agizo hilo leo Ijumaa Februari 7, 2020 mjini Dodoma wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu video hiyo iliyozua gumzo mitandaoni.
Amesema Elimringi ni ofisa biashara wa wilaya hiyo, “mtumishi huyo yupo chini ya ofisi ya Rais Tamisemi, tukio lile ukiliangalia kwenye mitandao ya kijamii halileti afya njema kwa nchi yetu ambayo ina utulivu na amani lakini wananchi wake wanaheshimiana kwa misingi ya imani mbalimbali”
“Mimi ni waziri ninayesimamia tawala za mikoa na Serikali za mitaa ambayo Halmashauri ya Kilosa ni miongoni mwa halmashauri ninazozisimamia maana yake na mtumishi huyo ni miongoni mwa watumishi walio chini ya Tamisemi. Nimemuagiza mkurugenzi kumsimamisha kazi.”
Ameongeza, “nimemuagiza mkurugenzi amsimamishe kazi na afanye uchunguzi na kamati ama mamlaka yake ya nidhamu iweze kuchukua hatua kwa kadri itakavyoona inafaa mara baada ya uchunguzi huo.”
Amesema kitendo hicho hakileti picha nzuri kwa Watanzania wanaoheshimiana.