SERIKALI YAZINDUA MWONGOZO WA MATIBABU YA SARATANI NCHINI

Na Mwandishi Wetu – Dar es Salaam
Serikali ya Tanzania imezindua mwongozo wa kitaifa wa tiba ya magonjwa ya saratani utakaoziwezesha hospitali za serikali na binafsi katika kutoa matibabu kwa usawa na kurahisisha mawasiliano kati ya madaktari bingwa na wataalamu wengine.


Kuzinduliwa kwa mwongozo huo kumefuatia baada ya hospitali za kanda kuanza kutoa tiba za saratani, kuongezeka kwa hospitali binafsi na za umma zinazotibu ugonjwa huo kwa sasa nchini, huku kwa kipindi kirefu hospitali nyingi zikitumia miongozo tofauti na ile ya nje ya nchi.

Akizindua mwongozo huo, Waziri wa Afya Ummy Mwalimu amesema huduma za saratani zinasambaa katika hospitali mbalimbali nchini kwa sasa hivyo utoaji wa huduma lazima uangaliwe ili zitoke kwa kiwango kinachopaswa.

Amesema kuwepo kwa miongozo tofauti ilisababisha kutokuwepo kwa usawa katika tiba za wagonjwa lakini pia kulikuwa na changamoto ya mgonjwa kuendelea na tiba sahihi pindi akipewa rufaa kwenda hospitali nyingine.

“Kuwepo kwa mwongozo huu kutawezesha kurahisisha mawasiliano kati ya madaktari bingwa na wataalamu wengine wa matibabu ya saratani kote nchini,

“Kurahisisha uandaaji wa maoteo na ununuzi wa dawa na vitendanishi vinavyotumika katika matibabu ya saratani, mwongozo huu pia umetoa orodha ya dawa na vifaa tiba kwa ajili ya matibabu ya saratani ambayo itatumika kama mwongozo kwa ajili ya manunuzi na matumizi nchini,” amesema Ummy Mwalimu.

Amesema mwongozo huo pia itawezesha wananchi kupata huduma bora na za viwango vya juu katika vituo vyote vya matibabu kwa kuwa tiba zote zitapangwa kwa kufuata mwongozo huo.

Waziri Ummy amesema pia utawezesha kutoa mwongozo kwa mfuko wa taifa wa bima ya afya NHIF kuhusu dawa na vipimo mbalimbali stahiki kwa wagonjwa wa saratani.

“Mfuko wa Taifa NHIF uhakikishe unatumia mwongozo huu katika kuweka vitita vya huduma za saratani hapa nchini kwani katika ile standard treatment guideline kuna baadhi ya dawa za kutibu saratani hazikuorodheshwa, na niwaambie mmeweka masharti magumu sana katika vipimo hivi CT Scan na MRI nani anapima mara kwa mara tuondoe baadhi ya vikwazo na hili NHIF mkalitekeleze,” ameagiza.

Ameagiza mwongozo huo utumike na vituo vyote vinavyotoa tiba za saratani nchini;
“Ninafahamu hospitali zote zilishiriki kuuandaa hivyo sitegemei kusikia kuna hospitali inafanya tiba nje ya mwongozo huu, ninaagiza pia wizara kufanya mapitio ili kuhakikisha dawa zote zinazotibu saratani zinakumuishwa katika mwongozo huu.”

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Saratani Ocean Road (ORCI) Dk Julius Mwaiselage amesema, “Matumizi ya mwongozo huu yamefanyiwa majaribio kwa kipindi cha miezi sita katika taasisi hii kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha St Francisco.”


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post