BASHE : SERIKALI KUENDELEA KUFUATILIA DAWA ZA KUULIA WADUDU WANAOHARIBU PAMBA

Na Mathias Canal, Wizara ya kilimo-Dodoma

Serikali imewahakikishia wakulima wa Pamba nchini kuwa itaendelea kufuatilia upatikanaji wa viuadudu vya zao la pamba na kuhakikisha vinawafikia wakulima kwa wakati.

Naibu Waziri wa Kilimo Mhe Hussein Bashe ameyasema hayo tarehe 3 Februari 2020 wakati akijibu swali la swali la Mbunge wa Jimbo la Geita Vijijini Mhe Joseph Kasheku Msukuma aliyetaka kufahamu serikali inampango gani kupeleka dawa za kuuwa wadudu wa Pamba kwani zinazopatikana huwa ni chache.

Bashe amesema kuwa kama sehemu ya utekelezaji wa hamasa za kilimo cha Pamba, katika msimu wa kilimo wa mwaka 2017/2018 eneo la ekari 1,488,406 lililimwa na kuzalisha kiasi cha tani 132,961. Chupa milioni 4.6 za viuadudu zenye thamani ya shilingi bilioni 16.8 na vinyunyizi 15,300 vyenye thamni ya shillingi milioni 462 vilinunuliwa na kusambazwa mwaka huo.

Aidha, katika msimu wa 2018/2019 eneo la ekari 1,865,000 lililimwa na kuzalisha kiasi cha tani 222,725 ambapo chupa  milioni 6 za viuadudu vyenye thamani ya shilingi bilioni 29 na vinyunyizi 23,000 vyenye thamani ya shilling bilioni  1.8 vilinunuliwa.

Vilevile, katika msimu wa 2019/2020 eneo la ekari 1,786,890 lililimwa na kuzalisha kiasi cha tani 350,473 ambapo chupa milioni 8.2 zenye thamani ya shilingi bilioni 41 na vinyunyizi 20,000 vyenye thamani ya shillingi bilioni 1.6 vilinunuliwa.

Mhe Bashe amesema kuwa katika msimu wa 2017/2018 jumla ya ekapaki 965,300 na vinyunyizi 3,302 vilisambazwa katika Mkoa wa Geita. Aidha, jumla ya ekapaki 736,345 na vinyunyizi 3,020 vilisambazwa katika mkoa huo katika msimu wa 2018/2019. Kwa msimu wa 2019/2020 Mkoa wa Geita umekwisha kusambaziwa kiasi cha ekapaki 8,748 na usambazaji bado unaendelea.

Bashe amesema, si sahihi kusema kuwa Serikali inahamasisha kilimo cha pamba  ikiwa haina uwezo wa kupeleka sumu za kuulia wadudu na hata  zinapopatikana huwa ni chache. Serikali inaendelea kuhamasisha kilimo cha mazao likiwemo zao la pamba ili kuongeza tija na uzalishaji wa mazao kwa kushirikiana na wadau mbalimbali.

Akizungumzia uchache wa viuadudu vya zao la pamba Mhe Bashe amesema kuwa umechangiwa na baadhi ya wakulima kutumia viuadudu katika kupulizia mazao mengine kama vile mahindi na viazi vitamu ili kudhibiti viwavijeshi vamizi.

Vilevile, amesema kuwa kukosekana kwa uaminifu kwa baadhi ya viongozi wa vijiji katika baadhi ya maeneo ukiwemo Mkoa wa Geita ambapo viuadudu havikupelekwa kwa wakulima na badala yake kuuzwa katika maduka ya pembejeo kinyume na taratibu za usambazaji wa viuadudu vya zao la pamba.

Ameongeza kuwa Watu zaidi ya 12 walikamatwa na kati yao 9 walifunguliwa mashtaka ambapo watu nane (8) walihukumiwa kifungo cha miezi sita jela kila mmoja.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post