ONGEZEKO LA SANGARA ZIWA VICTORIA LAISHTUA CCM,YATOA MAAGIZO MAZITO

 Katibu wa CCM Mkoa wa Simiyu, Haula Kachwamba akibeba samaki aina ya sangara mwenye urefu wa  sentimita 90 akiwa na uzito wa kilo 15 baada ya kutembelea Mwalo wa Nyamikoma Busega Simiyu na kushangazwa na mafanikio ya Serikali ya kudhibiti uvuvi haramu
KATIBU wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Simiyu, Haula Kachwamba akikagua zana haramu zilizokamatwa katika Mwalo wa Nyamikoma wilayani Busega mkoani Simiyu wakati wa ziara ya Wajumbe wa Sekretarieti ya CCM Mkoa Simiyu kukagua utekelezaji wa Ilani ya CCM kwenye Sekta ya Uvuvi. Kulia ni Afisa Mfawidhi Ulinzi na Usimamizi wa Rasilimali za Uvuvi Kanda ya Simiyu na Magu, Samson Mboje.
 Na Mwandishi Wetu, Simiyu


CHAMA cha Mapinduzi kimeshtushwa na ongezeko kubwa la samaki aina ya Sangara ikiwa ni miaka mitatu tu tangu Serikali ya awamu ya tano kuanza operesheni za kudhibiti uvuvi haramu katika Ziwa Victoria na kutaka Serikali kuchukua hatua za haraka kutafuta masoko ya uhakika ya samaki ndani na nje ya nchi.


Wakizungumza kwenye ziara ya Wajumbe wa Sektetarieti ya Chama cha Mapinduzi Mkoa wa Simiyu baadhi ya Wavuvi katika Mwalo wa Nyamikoma wilayani Busega wamesema awali kabla ya operesheni kuanza walikuwa wakisafirisha wastani wa tani 6 za samaki kwa mwezi lakini tangu Serikali ilipoamua kuchukua hatua za kudhibiti uvuvi haramu samaki wameongezeka na sasa wanasafirisha wastani wa tani 60 kwa mwezi.

Mwenyekiti wa Kikundi cha Usimamizi wa Rasilimali za Uvuvi ‘BMU’ Mwalo wa Nyamikoma wilayani Busega mkoani Simiyu , George James alisema ongezeko hilo kubwa la samaki pia limepunguza bei ya Sangara kutoka wastani wa shilingi 9,000  kwa kilo hadi kufikia shilingi 4,000 kwa kilo.


Mbali na mafanikio hayo pia wavuvi hao wameiomba Serikali kuwasaidia kupata mtambo wa kutengeneza barafu katika eneo hilo kwani kwa sasa wanalazimika kusafiri hadi jijini Mwanza umbali wa zaidi ya kilomita 150 kufuata barafu.


Hivyo walimuomba Katibu wa CCM Mkoa wa Simiyu kumfikishia shukrani Rais wa Tanzania, Dk. John Pombe Magufuli  kwa uongozi wake imara hasa katika usimamizi wake wa rasilimali za uvuvi na kwamba sasa samaki ni wengi na kwamba ombi lao kubwa ni kusaidiwa kupata soko baada ya ongezeko hilo la samaki.

Akizungumza katika Mkutano wa hadhara uliofanyika katika Mwalo wa Nyamikoma wilayani Busega, Katibu wa CCM Mkoa wa Simiyu, Haula Kachwamba  aliitaka Serikali kupitia Dawati la Sekta Binafsi lililoko Wizara ya Mifugo na Uvuvi kufika katika mwalo huo wa Nyamikoma ili kuwaunganisha wavuvi hao na taasisi za kifedha kuweza kupata mtambo wa kutengeza barafu.


Pia ameitaka Serikali kutanua wigo wa kuwatafutia masoko ya samaki wavuvi hao ili kunufaika na fursa kubwa ya ongezeko hilo la samaki aina ya Sangara kwa kupeleka katika masoko ya mikoa ya mbali na Ziwa Victoria pamoja na nchi za jirani za Kongo, Zambia, Burundi, Rwanda, Malawi na Msumbiji.


Kuhusu vita dhidi ya uvuvi haramu, Katibu huyo alisema Ilani ya CCM imeitaka Serikali kudhibiti uvuvi ili kupata uvuvi endelevu na kuongeza kipato cha mwanchi mmoja mmoja na kuiletea fedha za kigeni Serikali kutokana na mauzo ya samaki nje ya nchi na kupongeza juhudi kubwa zilizofanywa na Rais Dk. John Magufuli katika kusimamia rasilimali hizo za uvuvi.

“Tunaishukuru Serikali kwa kuamua na kusimamia operesheni Sangara ambayo ilisimamiwa na Wizara ya Mifugo na Uvuvi operesheni hii imezaa matunda kama mlivyotoa ushuhuda kwamba operesheni hii mliipinga sana lakini sasa mnaona matokeo yake”alisema.


Aliongeza kuwa CCM inaamini katika kusimamia sheria na kwamba hatua zote zilizochukuliwa na Serikali katika kudhibiti uvuvi haramu zililenga kunufaisha watanzania wengi tofauti na hapo awali ambapo watu wachache ndio waliokuwa wakinufaika kupitia uvuvi haramu.


“Niipongeze sana Serikali yetu kwa kukubali kutukanwa, kuzuliwa maneno mengi kupata kashfa nyingi lakini bado waliendelea kusimamia msimamo wa kulinusuru ziwa letu kwenye ilani yetu tumesema tutahakikisha tunadhibiti uvuvi haramu ili tuweze kupata samaki wa kutosha kwa ajili ya watanzania sisi CCM tunaomba msiishie hapa endeleeni kudhibiti uvuvi haramu ili matunda yazidi kuongezeka siku hadi siku”alisema Katibu wa CCM


Katika hatua nyingine, Mwakilishi wa Mkuu wa Wilaya ya Busega, David Palanjo aliongoza zoezi la uteketekezaji wa shehena ya nyavu haramu zilizokamatwa kwenye operesheni hiyo katika wilaya za Magu na Busega na kutoa wito kwa wananchi kuunga mkono juhudi za Serikali katika kudhibiti uvuvi haramu.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post