MFANYABIASHARA WA MADINI YA DHAHABU MWANZA AKAMATWA KWA TUHUMA ZA KUWAJERUHI WATU WAWILI KWA RISASI AKIWEMO MPENZI WAKE

Mfanyabiashara wa madini ya dhahabu jijini Mwanza, Salum Othuman (44) anashikiliwa na Jeshi la Polisi Mkoa wa Geita kwa tuhuma za kuwajeruhi watu wawili, akiwemo mpenzi wake Happiness Israel (32).


Anadaiwa kumpiga risasi ya mguuni mpenzi wake baada ya kutokea ugomvi wakati wakiwa chumbani kwenye hoteli ya Kilimanjaro mjini Geita.

Leo Alhamisi Februari 27, 2020 Kamanda wa Polisi mkoani Geita, Mponjoli Mwabulambo amesema tukio hilo limetokea jana Februari 26, 2020.

Amesema mtuhumiwa huyo baada ya kufanya tukio hilo, alimbeba Happiness aliyekuwa akichuruzika damu kwa lengo la kutoroka lakini meneja wa hoteli hiyo, John Maftar(43) alimuona na alipomtaka asiondoke alitishia kumpiga risasi.

Mwabulambo amesema baada ya meneja kusogea pembeni mtuhumiwa aliingia kwenye gari lake na kumgonga, kisha kugonga geti na kuondoka eneo hilo.

Amebainisha kuwa polisi walimkamata na Happiness alipewa huduma ya kwanza na kupewa rufaa kwenda Hospitali ya Bugando baada ya kubainika mfupa wake wa paja umepasuka.

Amesema Maftar amepata majeraha maeneo mbalimbali mwilini, anaendelea na matibabu katika hospitali ya Mkoa wa Geita.

Mkurugenzi wa Hoteli hiyo, Paulo Lyimo amesema mtuhumiwa ni mteja wao wa mara kwa mara.

Amesema siku hiyo asubuhi akiwa na mpenzi wake chumbani, wahudumu wa hoteli walisikia mlio wa risasi na baadaye alitoka chumbani akiwa amembeba Happiness.

“Wahudumu hao walisema alimuweka kwenye gari na alipozuiwa asiondoke alimtishia meneja kwa bastola na alipojihami, mtuhumiwa aligonga geti na kumburuza meneja kisha kukimbia hadi pale alipokamatwa kwa msaada wa polisi na madereva bodaboda waliokuwa wakifukuzia gari yake .


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post